Al Sisi na Mfalme Abdullah wajadili ujenzi mpya wa Gaza
13 Februari 2025Viongozi hao wawili kama ilivyo kwa wengine wa mataifa ya kiarabu, wanaupinga mpango uliotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani wa kutaka kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza na Washington kulichukua eneo hilo.
Mazungumzo yao yamefanyika siku moja baada ya Mfalme Abdullah kukutana na Trump mjini Washington ambapo alimweleza upinzani wake dhidi ya pendekezo la kuwahamisha Wapalestina kutoka ardhi ya Gaza.
Ikulu ya Misri imesema Rais Al Sisi na Mfalme Abdullah pia wametoa rai ya kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya kusitisha kati ya Israel na kundi la Hamas, kuendelea kuachiwa huru kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina na kupelekwa misaada zaidi ya kiutu ndani ya Gaza.
Mfalme Abdullah alizungumza pia jana kwa njia ya simu na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kujadili hali aloitaja kuwa ya "wasiwasi kwenye Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi"