Ahmed Al-Sharaa ateuliwa rais wa mpito Syria
30 Januari 2025Mamlaka mpya ya Syria imetangaza Jumatano kwamba Ahmed al-Sharaa, aliyechukua usukani baada ya kuondolewa kwa Bashar al-Assad mwezi uliopita, ameteuliwa kuwa rais wa mpito na kupewa jukumu la kuunda bunge la mpito.
Muungano wa waasi unaoongozwa na kundi la Sharaa la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), ulimtimua Assad mnamo Desemba 8 baada ya mashambulizi ya haraka, na kumaliza miongo mitano ya utawala wa familia yake.
Waasi waliweka serikali ya mpito chini ya Mohammad al-Bashirkuongoza nchi hadi Machi 1. Shirika la habari la serikali la Syria limeripoti kuwa Al-Sharaa amepewa jukumu la kuunda baraza la kutunga sheria hadi katiba ya kudumu itakapokubaliwa, huku bunge la Assad likivunjwa na katiba ya 2012 ikisimamishwa.
Soma pia: Watawala wapya Syria wateua waziri wao wa mambo ya nje
Makundi yote ya kijeshi yamevunjwa na kuunganishwa katika taasisi za serikali, pamoja na kuvunjwa kwa jeshi la Assad na mashirika ya usalama. Chama cha Baath kilichotawala Syria kwa miongo kadhaa pia kilivunjwa.