Ahadi za wagombea Tanzania na uhalisia wa maisha ya raia
2 Septemba 2025Kampeni za uchaguzi wa urais nchini Tanzania zimeingia katika hatua muhimu huku wagombea 17 kutoka vyama tofauti wakisambaa katika mikoa yote ya nchi hiyo wakitangaza ilani na sera zao. Ikiwa ni kipindi ambacho wapiga kura wanatafuta majibu ya changamoto zao za kila siku, wachambuzi wanahoji kama kweli kile kinachonadiwa majukwaani kinaendana na mahitaji ya wananchi.
Tanzania, taifa lenye ukubwa wa kilomita za mraba 947,303 na idadi ya watu takribani milioni 67.5, linaendelea kukabiliana na changamoto za kiuchumi ambazo ni msingi wa ustawi wa wapiga kura.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira kinatarajiwa kuwa karibu asilimia 9 mwaka 2025, kikiongezeka kidogo kutoka asilimia 8.9 mwaka 2024. Hata hivyo vyanzo vingine vinaelezea takwimu tofauti, mfano ripoti ya mwaka 2024 ilionyesha kiwango cha asilimia 2.5 hali inayoweza kuashiria ukosefu wa ajira katika maeneo rasmi au tafsiri tofauti za maana kati ya vyanzo mbalimbali. Changamoto za ajira bado ni kubwa hasa kwa vijana na wakazi wa vijijini.
Gharama za maisha na huduma za afya
Kwa familia ya watu wanne gharama za maisha bila kodi zinafikia takribani shilingi milioni 4.1 kwa mwezi. Taarifa nyingine zinaonyesha gharama hiyo inaweza kufika shilingi milioni 5.1, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam. Jiji hilo ndilo lenye gharama kubwa zaidi ambapo mtu mmoja anahitaji karibu dola 782 kwa mwezi na familia ya wanne dola 1979, huku wastani wa mshahara ukiwa dola 406 baada ya kodi jambo linalofanya mapato ya kawaida yasitoshe hata kwa nusu ya mwezi.
Tanzania inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari. Kuna wastani wa daktari mmoja tu kwa kila watu 100,000, kiwango ambacho ni chini sana ya kiwango cha Shirika la Afya Duniani. Ingawa serikali imeanzisha sheria ya bima ya afya ya kitaifa bado upatikanaji wa huduma na ufanisi wa mifumo kama NHIF ni changamoto kubwa hasa kutokana na upungufu wa rasilimali za kifedha na mikopo inayodaiwa.
Wagombea urais wamekuwa wakisafiri nchi nzima wakipiga kampeni na kutangaza ahadi zao kupitia mikutano ya hadhara, redio, televisheni na mitandao ya kijamii. Ratiba iliyopangwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa INEC inawapa nafasi ya kuzungumza na wapiga kura katika kila eneo.
Doyo Hassan Doyo, mgombea wa chama cha National League for Democracy NLD, ameahidi adhabu ya kifo kwa wala rushwa. Kunje Ngombale Mwiru wa chama cha AAFP, ameahidi kunyonga mafisadi hadharani. David Mwaijojele wa chama cha CCK ameahidi kubadilisha mfumo wa mikopo inayowakandamiza wananchi na kuanzisha mikopo rafiki anayoita ongeza damu. Saumu Rashid wa chama cha UDP naye ameahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Masuala yaliosahaulika
Ripoti ya mwaka 2021 ya taasisi ya Twaweza inaonyesha matatizo makubwa yanayowaumiza Watanzania wengi. Gharama kubwa za maisha zilionekana kuwa kero kwa asilimia 56 ya wananchi, ukosefu wa ajira na fursa za kipato ulilalamikiwa na asilimia 50 huku asilimia 27 wakilalamikia uhaba wa chakula. Wengi walitaka serikali kushughulikia gharama za maisha, huduma za afya na huduma za usafiri.
Licha ya mazungumzo ya kila siku mitaani na mitandaoni kuhusu upoteaji wa watu utekaji na mauaji ya kiholela, masuala haya hayajapewa kipaumbele majukwaani. Wagombea wengi hawajatoa mpango wa kurejesha imani kwa familia zilizoathirika, jambo linaloongeza pengo kati ya viongozi na wananchi.
Wachambuzi wa siasa wanasema pengo kati ya ahadi za kisiasa na mahitaji ya wananchi ni dalili kwamba vyama havina tafiti za kina za kimaeneo. Profesa Michael Nyerembe, mchambuzi wa masuala ya siasa anashauri vyama kuwekeza katika tafiti na kusikiliza maoni ya wananchi badala ya kutegemea mitazamo ya mitandaoni pekee.
Kadri kampeni zinavyokaribia tamati swali kubwa linabaki ni nani kati ya wagombea hawa atakayebadilisha ahadi kuwa vitendo na kushughulikia changamoto zinazowakandamiza Watanzania kila siku. Wapiga kura wengi wanatarajia kuona suluhisho za kweli katika maeneo ya ajira gharama za maisha, huduma bora za afya na upatikanaji wa chakula. Ahadi hizi ndizo zitakazopima uhalisia wa kiongozi ajaye kama kweli ana nia ya kuwatumikia wananchi au la.