Afrika na Marekani wajadili ushirikiano wa kiuchumi
24 Juni 2025Viongozi hao aidha wamegusia changamoto za kisiasa na mwelekeo mpya wa kiuchumi.
Mkutano wa kilele wa biashara kati ya Marekani na Afrika unaoendelea mjini Luanda, Angola, umewakutanisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka sekta mbalimbali, lengo kuu likiwa ni kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili, katika zama ambazo China inaendelea kuwa mshirika mkubwa wa Afrika.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Rais wa Angola João Lourenço alisema Afrika inahitaji zaidi ya mitaji, na kusisitiza umuhimu wa uwekezaji unaoheshimu mamlaka ya mataifa, kuhamisha maarifa, kukuza ajira zenye ujuzi na kutumia rasilimali za ndani.
Balozi Troy Fitrell kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alieleza kuwa zaidi ya kampuni 300,000 za Kimarekani zinaonyesha nia ya kufanya biashara Afrika, ingawa bado hazijaingia sokoni. Alisema ni muhimu kuwaelimisha wawekezaji hao kuhusu fursa zilizopo barani Afrika.
Miongoni mwa miradi mikubwa inayojadiliwa ni mradi wa Lobito Corridor, ambao ni reli ya kilomita 530 itakayounganisha eneo la Chingola nchini Zambia na reli ya Benguela nchini . Mradi huu unalenga kuongeza uwezo wa usafirishaji wa madini ya shaba na mazao ya kilimo kuelekea pwani ya Atlantiki.
Waziri wa Uratibu wa Uchumi wa Angola, José Massano, amesema serikali yake haitatoa ufadhili wa moja kwa moja, bali itategemea uwekezaji wa sekta binafsi kupitia mikataba ya makubaliano.
Kwa mtazamo wa Flávio Inocêncio, mtaalamu wa mafuta na gesi, ushiriki wa Marekani katika mkutano huu unaweza kuashiria mwanzo wa mwelekeo mpya wa ushirikiano, hasa kwa kuzingatia mtindo wa uongozi wa Rais Trump unaotanguliza mahusiano ya kibinafsi kuliko ya kiserikali.
Mkutano huu umeonesha mwelekeo mpya wa Marekani barani Afrika, ukihamasisha sekta binafsi kuchukua nafasi ya mbele. Pamoja na changamoto za kisiasa, matarajio ni makubwa kuhusu ushirikiano wa muda mrefu, hasa kuelekea mkutano mwingine wa Afrika na Umoja wa Ulaya uliopangwa kufanyika Angola Novemba mwaka huu.