Afrika Kusini yawarejesha wanajeshi 127 kutoka DR Kongo
27 Februari 2025Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na jeshi la Afrika Kusini, wanajeshi 21 walirejea nyumbani siku ya Jumanne (Februari 25) na wengine 106 walirudi Jumatano (Februari 26).
Msemaji wa jeshi hilo, Prince Tshabalala, amesema wanajeshi wao walikuwa wakihudumu kwenye kikosi kilichotumwa na mataifa 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2023 kuisaidia serikali ya Kongo upande wa mashariki, ambako kundi la waasi wanaoungwa mkono na Rwanda, M23, wamepiga hatua kubwa.
Soma zaidi: Mzozo wa Kongo kutawala mkutano wa kilele wa AU
Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kuwarejesha wanajeshi wake nyumbani, tangu kuuawa kwa wanajeshi wake 14 mwishoni mwa mwezi Januari.
Afrika Kusini ilikuwa imetuma wanajeshi zaidi ya 1,000 nchini Kongo, ikiongoza kikosi hicho cha SADC chenye wanajeshi pia kutoka Malawi na Tanzania.