A.Kusini yafadhaishwa balozi wake kufukuzwa Marekani
15 Machi 2025Ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa imesema uamuzi wa Marekani wa kumfukuza balozi wa Afrika Kusini ni wa kufadhaisha na imetoa wito wa kufuata taratibu za kidiplomasia katika kulishughulikia suala hilo. Taarifa hiyo imeeleza kuwa Afrika kusini itaendelea na nia yake ya kujenga uhusiano wenye manufaa na Marekani .
Jana Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio alitangaza kuwa Balozi wa Afrika Kusini Ebrahim Rasool, hatakiwi tena Marekani kwakuwa ni mwanasiasa mbabe anayemchukia Rais Donald Trump.
Soma zaidi: Kwa nini Marekani inaiadhibu Afrika Kusini kwa kuifutia misaada?
Kufukuzwa kwa Rasool aliyewahi kuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, kumezidisha mvutano unaozidi kushika kasi kati ya nchi hizo mbili. Juma lililopita Trump alizidi kuupa sura mpya mvutano huo kwa kusema kuwa wakulima wa Afrika Kusini wanakaribishwa Marekani baada ya kurudia madai kuwa serikali ya Afrika Kusini inawanyang'anya ardhi wakulima hao ambao ni weupe.