Afrika Kusini yalikemea kundi la kuwapinga wageni
13 Agosti 2025Wizara hiyo imesema haiwezi kuwabaguwa wenyeji na wageni kwenye huduma za afya na ikitaka kuheshimiwa kwa sheria za nchi.
Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Dkt. Aaron Motsoaledi, amejibu kwa ukali madai na shinikizo kutoka kwa wanachama wa vuguvugu la Operation Dudula, wanaodai kuwa wageni wasio raia wa Afrika Kusini wazuiliwe kupata huduma za afya katika hospitali za umma.
"Hawawezi kutarajia tuwafukuze watu wanapokuwa wagonjwa. Uraia hauruhusiwi kutumika kama kigezo cha kuzuia huduma za afya," alisema Motsoaledi.
Kampeni ya kuwanyima wahamiaji huduma muhimu
Ili kuhakikisha sheria zinafuatwa, polisi wamesambazwa katika hospitali kadhaa za umma, kuhakikisha hakuna mgeni anayezuiwa kuingia kupata matibabu. Hata hivyo, wafuasi wa Operation Dudula wanasisitiza kuendelea na kampeni zao, kama anavyofafanua Foste Mpho mwanachama wa Dudula.
"Kuna mambo mengi tunayopambana nayo kupitia operesheni hii. Sio huduma hizi za afya pekee, mwakani tutapambana pia na shule kuhakikisha watoto wetu wanapewa kipaumbele," alisema Mpho.
Kundi la Operation Dudula linaendesha kampeni zinazolenga kuwanyima wakimbizi na wahamiaji, wasiokuwa na vibali au walio na vibali, huduma muhimu ikiwemo matibabu. Kutokana na kampeni hiyo, baadhi yao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani wiki hii. Kampeni hii pia imeanza kuleta athari kubwa miongoni mwa wageni, kama anavyofafanua Elmi Abdi, raia wa kigeni kutoka Somalia.
"Wanawazuia wazazi na akina mama wanaotaka kujifungua kupata tiba, na watoto wa wahamiaji pia wanazuiwa kwenda shule. Hakuna UNHCR au shirika lolote la kutetea haki za binadamu lililoweza kukemea hao watu," alisema Abdi.
Huduma bila malipo kwa raia wote
Kwa kawaida, huduma za afya nchini Afrika Kusini hutolewa bure kwa raia wote. Zaidi ya hayo, watoto wa wakimbizi na wahamiaji wenye umri chini ya miaka sita pamoja na wanawake wajawazito pia wanapata huduma hizi bure. Sera hii ilitangazwa rasmi mwaka 1995 na Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, kama anavyobainisha Waziri wa Afya, Dkt. Aaron Motsoaledi.
"Hilo lilitangazwa na Rais wetu wa kwanza, Nelson Mandela, mwaka 1995, na ndiyo maana tunatoa huduma za afya bure kwa wanawake wajawazito na watoto walio chini ya miaka sita bila kujali uraia wao," alisema Motsoaledi.
Wakati wanachama wa vuguvugu la Operation Dudula wakiendelea na kampeni za kuwatenga wageni, serikali ya Afrika Kusini inasisitiza wazi afya ni haki ya kila mtu, bila kujali uraia.