Afrika Kusini: Taifa moja, lugha rasmi 11
21 Julai 2025Lakini je, utajiri huu wa lugha ni ishara ya umoja na ushirikishwaji? Au ni vazi linalofunika mgawanyiko wa kisiasa, kijamii na kiutambulisho? Nini maana ya kuwa na lugha nyingi rasmi katika taifa moja, pamoja na athari zake katika ujenzi wa umoja wa kitaifa?
Mwaka 1996, katiba mpya ya Afrika Kusini ilizinduliwa. Katiba hii ilizitambua lugha 11 rasmi, ambazo ni Kizulu, Xhosa, Afrikaans, Sepedi, Setswana, Sesotho, Tsonga, Swati, Venda, Ndebele, na Kiingereza.
Uamuzi wa kihistoria
Profesa Thandiwe Mokoena, Mtaalamu wa Isimu, katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Afrika Kusini, anasema uamuzi huu ulikuwa wa kihistoria. ''Uamuzi huu ulionyesha nia ya serikali mpya kuondokana na urithi wa ubaguzi wa lugha na kutoa nafasi sawa kwa kila jamii ya lugha,'' alisema Profesa Mokoena.
Lugha hizi si tu njia ya mawasiliano, bali ni sehemu ya utambulisho, historia, na utamaduni wa mamilioni ya watu. Padri Musa Malome, Mtanzania anayeishi Afrika Kusini na kufanya kazi ya umisionari kupitia Kanisa Katoliki, yeye katika huduma yake, anahubiri Injili kwa lugha tatu tofauti, ambazo ni Setswana, Kiingereza na Sesotho. Anaamini kwamba kujua lugha nyingi kunamsaidia mtu kuelewana na watu wa tamaduni tofauti, kujenga urafiki mpya, na kupata maarifa mapya.
''Ni muhimu sana kujifunza lugha nyingi, mtu lazima awe na uwezo wa kuongea lugha mbalimbali, inasaidia pia kupanua uwezo wako wa kukutana na watu wenye uzoefu tofauti za lugha,'' alifafanua Padri Musa Malome.
Mpho Ramovha ni mkazi wa Soshanguve nje kidogo ya jiji la Pretoria, anasema kwa jamii nyingi, lugha yao ya asili ni nguzo ya fahari. Katika shule nyingi, sasa kuna juhudi za kufundisha kwa lugha za nyumbani. Pia, idhaa mbalimbali za redio na televisheni hutangaza kwa lugha tofauti, jambo linalofungua fursa za ajira na uhuru wa kujieleza. ''Mimi ni mzaliwa wa Limpopo. Kupitia lugha yangu ya Tshivenda, najihisi kuonekana na kuthaminiwa,'' alibainisha Ramovha.
Kujumuishwa kwa Kiingereza au Afrikaans
Kwa wengi, hii ni fursa ya kuishi bila kufichwa chini ya kivuli cha Kiingereza au Afrikaans kama ilivyokuwa zamani. Lakini Jerry Sosteness ni Mtanzania na wakili jijini Pretoria, anasema sio kila kitu ni rahisi.
Anasema ingawa katiba inatambua lugha 11 rasmi, ukweli ni kwamba si zote zinatumika kwa usawa katika maisha ya kila siku, hasa katika ofisi za serikali, mahakama, na biashara. ''Mahakama nyingi bado zinatumia Kiingereza au Afrikaans. Hii inawanyima haki wale wasioweza kuelewa lugha hizo vizuri,'' alisisitiza Sostenes.
Lungile Mshengu, mwanafunzi wa uhasibu katika Chuo Kikuu cha Johannesburg anasema vivyo hivyo, katika nyanja za ajira, lugha ya Kiingereza bado imebaki kuwa kigezo kikuu. Hali hii huleta ubaguzi wa kimya kimya dhidi ya wanaozungumza lugha nyingine. ''Nikiwa mzaliwa wa Eastern Cape, nilihitaji kujifunza Kiingereza kwa haraka ili nipate kazi. Lugha ya Xhosa haiwezi kunipeleka mbali,'' alifafanua Mshengu.
Lugha zinaweza kuwaunganisha watu au kuwagawa. Kulingana na Padri Malome, katika taifa lenye historia ya ubaguzi kama Afrika Kusini, lugha nyingi zinaweza kuchukuliwa kama daraja la usawa, lakini pia, kama kuta zinazotenganisha. ''Kama hatutajenga mfumo unaoendeleza usawa wa lugha zote, basi tutakuwa tumetengeneza mgawanyiko wa kimya kimya,” alifafanua Padri Malome.
Lakini pia kuna matumaini. Mashirika mengi ya kijamii, wasanii na vijana, wamekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya lugha zote kama chombo cha kujenga mshikamano.
Harakati za kuziendeleza lugha zote
Katika juhudi za kuhakikisha kila lugha inasikika na kuthaminiwa, serikali ya Afrika Kusini inaendelea kutumia Bodi ya Lugha ya Afrika Kusini, kuendeleza lugha zote 11 rasmi za taifa. Taasisi hiyo si tu inahamasisha matumizi ya lugha hizi katika ofisi za umma, bali pia inaendeleza lugha za ishara, na hata zile za kikanda kama vile Koi na San, ambazo zilikuwa katika hatari ya kutoweka.
Kupitia tafsiri, uchapishaji wa vitabu vya shule kwa lugha mbalimbali, na kampeni za mitandaoni, serikali inalenga kujenga taifa lenye usawa wa kiutamaduni na kilugha, na kuhakikisha kuwa hakuna lugha inayobaguliwa.
Lugha si maneno tu ya kutamkwa bali ni sauti ya utambulisho, chombo cha mawasiliano, na daraja la kujenga jamii jumuishi. Afrika Kusini, kwa kutambua lugha 11 rasmi, imeweka msingi wa usawa wa kitamaduni na kijamii.
Lakini kama tulivyosikia kutoka kwa wananchi na wataalamu, bado kuna changamoto kubwa za utekelezaji, hasa kwenye mfumo wa haki, elimu, na ajira.
Aidha, lugha mbalimbali sio tu faida binafsi, bali ni nyenzo ya kuvuka mipaka ya ubaguzi, kuleta mshikamano na kuimarisha maelewano miongoni mwa watu wa jamii tofauti.
Hivyo basi, kazi bado ipo kuhakikisha kuwa lugha hizi zote zinapewa nafasi sawa, si kwa maandishi tu bali kwa vitendo. Kwa sasa, swali linabaki je, Afrika Kusini itaweza kutumia urithi huu wa lugha kama chombo cha kuunganisha, au itaendelea kushuhudia mgawanyiko unaovaa joho la usawa?