Afrika Kusini kuondoa vikosi vyake Kongo mwezi huu
5 Mei 2025Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Afrika Kusini, Jenerali Rudzani Maphwanya, alisema hatua ya kuwaondoa wanajeshi hao inafanyika kwa awamu, ikiwa imeanza rasmi Aprili 29. Kulingana na ratiba hiyo, wanajeshi hao wanatoka DRC kwa njia ya barabara kupitia Rwanda na kuingia Tanzania kabla ya kurejea Afrika Kusini kwa njia ya anga na bahari.
Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilichopelekwa mashariki mwa DRC mwezi Desemba 2023 kukabiliana na kuibuka upya kwa waasi wa M23 wanaodhibiti maeneo kadhaa yenye utajiri wa madini.
Soma pia:Tshisekedi atetea mkataba wa amani kati ya Kongo na Rwanda
Mapema wiki iliyopita, malori 13 yaliyobeba wanajeshi 57 wa kikosi cha SADC (kilichofahamika kama SAMIDRC) yalikuwa tayari yamewasili katika kituo cha mkusanyiko nchini Tanzania. Kundi linalofuata linatarajiwa kuondolewa wiki hii, alisema Maphwanya.
Aliweka wazi kuwa usafirishaji kutoka Tanzania hadi Afrika Kusini utafanyika kwa njia ya ndege kwa wanajeshi, huku mizigo na vifaa vya kijeshi vikisafirishwa kwa meli.
Alisisitiza kuwa wanajeshi wote watakuwa wamerejea nchini kabla ya mwisho wa Mei, isipokuwa wale wachache watakaosimamia vifaa vya usafirishaji.
Kuondoka si kushindwa, ni nafasi ya kupatikana kwa amani
Mkutano wa SADC mwezi Machi uliazimia kumaliza rasmi operesheni ya SAMIDRC baada ya wanajeshi 17 — wengi wao wakiwa Waafrika Kusini — kuuawa na waasi wa M23 mwezi Januari. Tangu wakati huo, vikosi hivyo vimekuwa vikisubiri kuondolewa.
SADC ilithibitisha kuanza kwa mchakato wa kuondoka wiki iliyopita, lakini haikutoa maelezo ya kina. Aidha, Aprili 30, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilianza mchakato tofauti wa kuwaondoa mamia ya polisi na wanajeshi wa DRC waliokuwa wamekwama kwa miezi kadhaa kwenye kambi za Umoja wa Mataifa mjini Goma baada ya mji huo kutekwa na M23.
Maphwanya alisema wakuu wa ulinzi wa SADC waliliarifu kundi la M23 kuwa watayaondoa majeshi na vifaa vyao "bila masharti yoyote.” Alisisitiza kuwa, "SADC haiachi hata sindano moja Mashariki mwa DRC.”
Soma pia:Jumuiya ya SADC yaamua kuondoa vikosi vyake mashariki mwa DRC
Ingawa idadi rasmi ya wanajeshi wa SAMIDRC haikutajwa, inakadiriwa kuwa Afrika Kusini ilituma wanajeshi wasiopungua 1,300. Wengi walihusika katika operesheni hiyo tofauti na wale walioko DRC chini ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO).
Maphwanya alisisitiza kuwa hatua ya kuondoa majeshi si dalili ya udhaifu au kuwasaliti raia waliokwama katikati ya mapigano, bali ni "hatua ya kiufundi inayotoa nafasi kwa mchakato wa amani na upatanisho kuendelea."
Marekani na Umoja wa Mataifa wameishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imeyakanusha.