Afrika kukusanya trilioni 2 ifikapo 2030 kutokana na AI
3 Aprili 2025Mkutano huu ambao unafanyika kwa mara ya kwanza katika bara la Afrika una lenga kujadili changamoto na faida za matumizi ya akili mnemba hasa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
Mkutano huu umeandaliwa na serikali ya Rwanda kwa ushirikiano na jukwaa la kimataifa kuhusu uchumi WEF na kituo cha kimataifa kuhusu maendeleo ya teknolojia na digitali.
Wataalam wa ngazi za juu kuhusu teknolojia na digital pamoja na matumizi ya akili mnemba wanazungumzia jinsi uvumbuzi huu ambao unaonekana kuitawala dunia sasa unavyoweza kulisaidia bara la Afrika katika kupiga hatua ya maendeleo hasa kuwasaidia vijana kubuni ajira.
Teknolojia ya akili mnemba kwa sasa inatumiwa katika kila sekta ya maisha na Afrika haina budi kwenda na wakati kwa kuziangalia fursa zinazotokana na teknolojia hii.
Soma pia:Taarifa za uongo za AI zinaweza kuathiri uchaguzi Afrika
Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema teknolojia pamoja na matumizi ya akili-mnemba vimekuwa ni sehemu ya maisha na kwa mantiki hiyo Afrika haina sababu yoyote ya kusalia nyuma
Akili-mnemba kwa sasa ndiyo inaendesha ubunifu mkubwa na wa hali ya juu ulimwenguni, na inazidi kuleta mapinduzi katika maendeleo ya kidigitali.
Akili Mnemba viwandani
Katika viwanda vingi ulimwenguni faida ya matumizi ya akili mnemba inaonekana na jinsi inavyosaidia katika kuchukua maamuzi makubwa lakini pia kupunguza makosa ya kibidanamu katika kufanya mambo.
Hata hivyo kwa bahati mbaya kuongezeka kwa teknolojia hii kunakabiliwa na tatizo la ushindani wa kikanda kiasi kwamba,kwa sasa maendeleo ya teknolojia hii yamejikita katika nchi chache. Afrika haiwezi kuvumilia kubaki nyuma tena na kuanza kufukuzia tu.
Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi wakuu katika nchi za kiafrika pamoja na wakuu wa mashariki mbalimbali ya kimataifa kuhusu teknolojia, uchumi na fedha.
Viongozi hawa wamesema kwamba sekta hii ya matumizi ya akili mnemba inahitaji utashi wa kisiasa na uwekezaji mkubwa maana kwa kufanya hivyo kutasaidia nchi za kiafrika kujikwamua kiuchumi.
Soma pia:Mkutano wa Paris washindwa kufikia tamko la pamoja kuhusu AI
Takwimu katika mkutano huu zimeonyesha mwaka 2030 bara la Afrika litapata faida ya kiuchumi inayokadiriwa kufikia dola za Marekani trillion 2.9.
Lakini hilo litawezekana ikiwa changamoto hizi zitatafutiwa ufumbuzi kama anavyofafanua Rais Togo Faure Gnassingbe anayehudhuria mkutano huu.
Huu ni muda wetu sisi kushirikiana kwa kuzingatia jinsi ilivyo kwa sasa ulimwenguni, isingekuwa busara sisi kama waafrika kuendelea kutegemea uhisani kwa washirika wetu wa nje na ndiyo maana ninasema kwamba kwa haraka tunahitaji maeneo ambayo tunatakiwa kuyapa kipa umbele tena haraka bila kudhani tutafanya kila kitu kwa ujumla wake.
Mchango wa AI katika maendeleo ya dunia
Akili mnemba imetajwa kuleta mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali hasa katika sekta za afya,elimu, usalama na maeneo mengine muhimu.
Viongozi hawa wanasema kutumia akili-mnemba katika huduma mbalimbali kunaweza kuifanya Afrika kuruka hatua nyingi za ukuaji wa kiuchumi hasa kwa sababu Afrika ni bara ambalo lina wakazi wengi vijana.
Mwenyekiti wa kamisheni ya umoja wa Afrika Mahmoud Ali Yousouf akazitaka serikali za kiafrika kuweka sera madhubuti za kulifikia hilo.
Soma pia:Marekani yaonya kuhusu udhibiti wa Akili Mnemba
Tunatakiwa kupiga hatua zaidi kuhakikisha bara la Afrika linaanzisha sera hizi kuhusu matumizi ya akili mnemba katika sekta mbalimbali,kwa mfano Marekani inawekeza zaidi ya dola bilioni 285 kila mwaka.
China ikiwekeza dola billion 95 katika uwekezaji kwenya matumizi ya akili mnemba, tunachotakiwa kufanya barani afrika ni kuhamasisha uwezo wa kifedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye eneo hili.
Watalaam na viongozi hawa wameazimia katika mkutano huu kuwa wataanzisha mfuko maalum ambao hatimaye utahamasisha kuweka juhudi zao pamoja kama waafrika na kukusanya pesa zitakazosaidia kubuni miradi ya uwekezaji katika matumizi ya akili mnemba.