AFRIKA KATIKA MAGEZETI YA UJERUMANI
31 Oktoba 2003
AFRIKA KATIKA MAGEZETI YA UJERUMANI leo imewakusanyia mada kuhusu juhudi za amani kunusuriwa Ivory Coast, UU kuchangia kifedha juhudi za amani barani Afrika na ziara ya Waziri wa Nje wa Ujerumani barani Afrika. Ahmed Mohamed anaendelea kusimulia: Ili kuzinusuru juhudi za amani katika Ivory Coast, nchi za Afrika ya Magharibi zimesema zinataka kupeleka kikosi cha kuingilia kati. Serikali ya mpito mjini Abidjan iliyowashirikisha waasi wa zamani ilivunjika mwishoni mwa Septemba. Kuhusu juhudi za amani nchini Ivory Coast, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeripoti:
"Mwishoni mwa Septemba waasi wa zamani walijitoa katika serikali ya mpito baada ya kishirikishwa kwao katika mkataba wa amani kufuatana na mapatano yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Ufaransa. Waasi walikataa pia yale mawafikiano ya kusalimisha silaha zao yaliyofikiwa mwisho wa Oktoba. Wamemlaumu Rais Laurent Gbagbo kuwakatalia Mawaziri wao kibali cha kuendesha nyadhifa zao. Pamoja na hayo walimlaumu kuwa amewateuwa Mawaziri wa Mambo ya Ulinzi na Ndani bila ya ushauri wao. Mkuu wa waasi Soro aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Mawasiliano katika serikali ya mpito, ametishi kuanzisha tena vita vya ndani. Katibu wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi, ECOWAS, Shambas, alisema Rais Laurent Gbangbo anadai kuiendesha nchi kufuatana na katiba iliyokuweko kabla ya kufanyika mapatano hayo ya amani. Upande wa pili waasi wanashikilia kuwa yaheshimiwe mapatano hayo ya amani yenye kiini cha kuundwa serikali ya mpito ambayo Waziri wake Mkuu alikuwa Seydou Diarra. Bwana Shambas alisema kuwa kutokana na harakati zake nchini Liberia ECOWAS imeupuuza mgogoro wa Ivory Coast. Vikosi vya ECOWAS vikiendesha harakati za hifadhi ya amani Liberia tangu ajiuzulu Rais wa zamani Charles Taylor."
Kwa kulingana na gazeti la FRANKFUTER RUNDSCHAU.
UU unataka kusaidia kifedha harakati za vikosi vya Kiafrika vya kuhifadhi amani barani Afrika. UU umeahidi kutoa EURO miliyoni 250 hapo mwakani, kama vile ilivyoshauriwa na Halmashauri ya UU mjini Brussels. Shabaha ya uamuzi huo ni kuhakikisha msingi madhubuti wa kifedha wa vikosi vya hifadhi ya amani vya Kiafrika. Lakini pesa hizo hazitoweza kutumiwa kununulia silaha au kuwalipa wanajeshi, alisema msemaji wa Halmashauri ya UU. Pendekezo la kupewa msaada wa kifedha vikosi vya Kiafrika vya kuhifadhi amani barani Afrika lilitolewa na viongozi wa serikali na taifa wa nchi za Kiafrika katika mkutano wao wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Maputo mwezi wa Julai mwaka huu.
Fischer aiahidi misaada Naimbia wakati wa ziara yake. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani asema Ujerumani inatambua historia yake ya ukoloni lakini amekataa kuiomba radhi Nambia, kilikuwa kichwa cha maneno katika gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.
Gazeti hilo liliandika: "Historia ya Ukoloni hadi hii leo inaendelea kuutatiza uhusiano kati ya Ujerumani na Namibia. Baina ya 1904 na 1907, inakisiwa wanajeshi wa Kijerumani wamewauwa Waherero wapatao 65,000. Kwa muda wa miaka mingi jamaa za wahanga hao wanadai Ujerumani iwalipe pesa za fidia. Wanadai jumla ya Dollar biliyoni nne. Lakini serikali ya Ujerumani inachukua msimamo kuwa matendo hayo ya kikatili kutoka enzi ya Ukoloni hayawezi kufidiwa kifedha. Pia Waziri wa Nje Fischer amekataa kuomba msamaha rasmi mjini Windhuk. Pia serikali ya Namibia haiungi mkono madai hayo ya kabila hilo la walio haba la Waherero," lilimaliza kuripoti gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.
Gazeti la DIE TAGESZEITUNG lilituwama ripoti yake juu ya ziara ya Waziri Fischer katika nchi tatu za Kiafrika. Gazeti hilo liliendelea kuandika: "
"Ziara ya wiki kama moja ya Waziri wa Nje wa Ujerumani Joschka Fischer katika Mali, Namibia na Afrika ya Kusini, inaonyesha kuwa harakati za kidiplomasia barani Afrika si lazime zituwame juu ya maeneo ya migogoro. Nchi hizo tatu ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zenye utulivu mkubwa wa siasa ya ndani na marekibisho ya kidemokrasi. Tangu azizuru hapo 2000 Angola na Rwanda zilizoshiriki katika mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, , Waziri wa Nje wa Ujerumani hii leo anahiyari kuwaachilia wanasiasa wengine maeneo ya migogoro barani Afrika. Badala yake Fischer hii anautembelea upande wa mwangaza barani Afrika. Nchini Mali alitoa shukurani kwa niaba ya serikali ya Ujerumani kwa msaada uliotolewa na nchi hiyo katika kusaidia kuachwa huru watalii wa nchi za Magharibi kutoka hatamu za waasi waliokuwa na maskani yao ya kujificha katika jangwa la Sahara karibu ya mpaka wa Algeria. Haikushangaza kuwa Bwana Fischer ameizuru pia Afrika ya Kusini ambayo ni mshirika muhimu kabisa wa kibiashara wa Ujerumani barani Afrika," gazeti la DIE TAGESZEITUNG, lilikamilisha makala hii ya AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA KIJERUMANI.