Afrika katika magazeti ya Ujerumani
28 Februari 2025Bild Online
Gazeti la Bild Online wiki hii limeandika kuhusu kuibuka kwa ugonjwa wa ajabu ulioripotiwa Kaskazini magharibi mwa Kongo. Kulingana na gazeti hili watu 419 wameripotiwa kuwa wameambukizwa maradhi hayo katika kipindi cha wiki tano. Watu 53 tayari wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo usiofahamika.
Ugonjwa huo ulianza Januari 21 kwenye Kijiji cha Boloko baada ya watoto watatu kumuuwa popo na kumla. Wote watatu walikufa ndani ya saa 48 kulingana na tamko la Shirika la afya duniani WHO lililotolewa Jumatatu.
Tangu hapo, watu wengine zaidi walipata maambukizi, na wengi wao walikufa ndani ya saa 48 za mlipuko wa maradhi hayo. Mkurugenzi wa Hospitali ya Bikoro nchini Kongo, Serge Ngalebato amesema wataalamu wa afya wana hofu kubwa juu ya maradhi hayo. Dalili zake ni pamoja na homa, kutapika na kuvuja damu ndani kwa ndani.
Magonjwa yanayosambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu yamekuwa yakiibua wasiwasi katika maeneo ambako watu wake wanakula wanyama wa mwituni. Idadi ya milipuko ya magonjwa ya aina hiyo barani Afrika, imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 katika miaka kumi iliyopita kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 za Shirika la Afya duniani WHO.
Die Zeit
Die Zeit limeimulika hatua ya Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WPF ya kusitisha kupeleka misaada katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam inayokabiliwa na njaa huko Sudan.
Gazeti hili limemnukuu mkurugenzi wa kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika hilo Laurent Bukera aliyesema maelfu ya familia za watu wanaoishi kwenye kambi ya Zamzam wako katika hatari ya kufa kwa njaa kama misaada haitopelekwa mara moja. Hadi sasa, WFP limeshawahudumia karibu watu 300,000 waliolazimika kuhamia kwenye kambi hiyo katika eneo la Darfur Kaskazini.
Kutokana na mashambulizi yanayoendelea shirika la mpano wa chakula na washirika wake walifanikiwa kuwafikia wakaazi 60,000 pekee wa kambi hiyo katika mwezi wa pili pekee. Katika shambulio mojawapo, soko kuu la Zamzam liliharibiwa vibaya. WFP linasema, matokeo yake watu wamekuwa na hofu ya kwenda ya kutafuta mahitaji muhimu ya chakula na bidhaa nyingine. Kwa sababu za kiusalama mashirika ambayo ni washirika wa WFP yamelazimika kuondoka kambini hapo katika muda wa wiki mbili zilizopita kutokana na mapigano kati ya jeshi rasmi la serikali ya Sudan dhidi ya kikosi cha wanamgambo wa RSF.
Afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la kuratibu misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa Edem Wosornu anasema zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo wakati nusu ya idadi jumla ya watu nchini humo ikikabiliwa na njaa kali.
Die tageszeitung
Die tagesszeitung limeutupia jicho mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo likiwa na kichwa kinachosomeka, M23 yawaruhusu Waafrika Kusini kuondoka. Linaeleza kuwa, juhudi za kikosi cha mataifa ya Kusini mwa Afrika za kulinda amani, zimekwama mjini Goma tangu waasi wa M23 walipoutwaa mji huo.
Na sasa Afrika Kusini imeruhusiwa kuwasafirisha kwa ndege majeruhi na wanawake wajawazito walioathiriwa na machafuko ya eneo hilo la mashariki mwa Kongo kupitia Rwanda. Taarifa hiyo imethibitishwa na msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo aliyesema shughuli ya kuondolewa kwa majeruhi na wajawazito inaratibiwa na Ujumbe wa Kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo na kuungwa mkono na serikali ya Rwanda.
Gazeti hili linakumbusha kuwa, jumla ya wapiganaji 2,600 wa kikosi maalumu cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika walipelekwa Goma wakati mji huo ulipokuwa chini ya udhibiti wa serikali ya Kongo na baadhi yao walipelekwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma. Wengine walikuwa kwenye kambi kubwa ya jeshi ya Mubambiro magharibi mwa mji huo.
Mapambano dhidi ya M23 yalipopamba moto, wanajeshi wa SADC waliishiwa na silaha, suala lililothibitishwa baadaye na Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini. Hawakuwa hata na vesti maalumu za kuzuia risasi. Hivyo, wanajeshi hao wa Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika walifanya mipango ya kusitisha vita na waasi.
Jumla ya wanajeshi 16 wa ujumbe huo walikufa katika mapambano. Wawili walikuwa Watanzania. Wanajeshi 14 wa Afrika Kusini waliouwawa walishasafirishwa kurejeshwa nyumbani wiki mbili zilizopita kupitia Uganda.
Wanajeshi wa SADC waliosalia wanaendelea kushikiliwa kama wafungwa wa vita katika uwanja wa ndege wa Goma wakiwa wamezingirwa na waasi.
Die Zeit
Die Zeit; safari hii limeandika kuhusu mwandishi mahiri wa vitabu Boualem Sansal mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Algeria, aliyekamatwa Novemba 16 2024 nchini Algeria. Mwanasheria wa Sansal François Zimeray amesema bado hajaruhusiwa kulipata jalada la uhalifu la Sansal. Zimeray ameliambia gazeti la die zeit kuwa mteja wake ameshtakiwa chini ya kifungu cha 87 cha sheria ya Algeria cha makosa dhidi ya usalama wa taifa.
Habari za kushtusha kuhusu mwandishi huyo wa vitabu mwenye miaka 80 anayesumbuliwa na saratani ni kuwa amegoma kula chakula. Kutokana na hilo, matibabu yake ya mionzi yamesitishwa katika hospitali ya gereza la Mustapha mjini Algiers. Inasemekana kuwa kwa sasa amerejeshwa gerezani. Sababu ya kugoma kula inatajwa kuwa ni kupinga shinikizo la kumtaka ambadilishe mwanasheria wake ambaye ni myahudi, kulingana na jarida la Le Figaro la Ufaransa.