Afrika katika magazeti ya Ujerumani
14 Februari 2025Die Tageszeitung
Die Tageszeitung limeandika kuhusu mzozo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Linaeleza kuwa, kuna sababu zinazoeleweka za vita vya M 23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Sababu hizi hazina budi kushughulikiwa ili kurejesha amani nchini humo baada ya miaka 30 ya machafuko.
Linakumbusha kuwa, mwishoni mwa mwezi Januari waasi wa M23 waliudhibiti mji wa mashariki mwa Kongo wa Goma. Jeshi la nchi hiyo, vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, wanajeshi wa Afrika Kusini, wapiganaji mamluki wa Romania na Ufaransa pamoja na wanamgambo wa ndani wa FDLR wote kwa ujumla, hakuna walioweza kusimama dhidi ya waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda na Uganda.
die tageszeitung limeandika, vita vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo havikuanza miaka mitatu iliyopita pekee kwa mashambulizi ya waasi wa M23. Vilianza karibu miaka 30 wakati muungano wa waasi wa Kongo AFDL ulioungwa mkono na nchi nyingi za Afrika ulipoidhibiti nchi nzima na kumweka Laurent Desire Kabila madarakani.
Katika miaka karibu 30 tangu wakati huo, hakuna siku inayopita Kongo bila kusikia milio ya risasi, watu kulazimika kuyahama makazi yao, mikasa ya ubakaji na mauaji. Kulingana na tafiti, mamilioni ya watu wameuwawa kutokana na matokeo ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja ya vita hivyo. Gazeti hili limehitimisha kwa kuandika kuwa ni wakati muafaka sasa wa kutafuta suluhisho la kudumu, na zaidi kulitekeleza, ili kurejesha amani Kongo.
Neuer Zürcher
Mwanzoni mwa wiki hii baadhi ya magazeti ya Ujerumani yalikuwa na taarifa za kusikitisha juu ya kifo cha mpigania uhuru na Baba wa taifa la Namibia; Sam Nujoma aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita akiwa na miaka 95.
Gazeti la Neuer Zürcher linaeleza kuwa msiba huo ulitangazwa na serikali ya Namibia. Linabainisha kwamba taarifa hiyo ya serikali haikueleza chanzo cha kifo cha kiongozi huyo wa zamani lakini imeweka wazi kuwa alikuwa amelazwa hospitali kwa kipindi cha wiki tatu na afya yake haikutengamaa.
Limerejea historia kuwa, Sam Nujoma alikuwa rais wa vuguvugu la kupigania uhuru lililokuja kufahamika kama chama cha SWAPO. Alichaguliwa kuwa rais wa Namibia mwaka 1990 baada ya Namibia kupata uhuru wake.
Neuer Zücher limeandika Nujoma hakuwa dikteta. Alichaguliwa tena kuongoza nchi yake mwaka 1994. Aliombea tena urais kwa muhula wa tatu mwaka 1999 na kuhitimisha kipindi cha uongozi wake mwaka 2005 na leo hii nchi yake, Namibia ni moja ya mataifa yenye demokrasia thabiti barani Afrika.
Die Zeit
Die Zeit liliiangazia hatua ya Misri ya kutangaza mpango wake wa kuujenga upya Ukanda wa Gaza. Limeanza kwa kuandika kuwa, wakati kukiwa na shinikizo kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump, Misri imeweka wazi mpango wake wa kuufanyia ukarabati ukanda huo ulioharibiwa vibaya kwa vita, kama ilivyotangazwa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Misri.
Tangazo hilo linasema mpango huo umedhamiria kuhakikisha kuwa Wapalestina wanasalia kwenye ardhi yao na haki zao zinaheshimiwa.Tamko la Misri liliweka wazi kwamba, serikali yake inataka kufanya kazi na Trump kuhakikisha kuna amani yenye kuzingatia haki katika eneo hilo. Lilieleza pia kuwa, suluhisho la kuwa na nchi mbili, yaani Palestina na Israel ndiyo njia pekee ya kuwa na utulivu katika kanda hiyo.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Rais Donald Trumo alitishia kusitisha misaada kwa Misri na Jordan kama nchi hizo zingekataa kuwapokea Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.
Hata hivyo, Jordan na Misri zilipinga vikali pendekezo la kuwahamisha Wapalestina wanaoishi Ukanda wa Gaza kinyume na matakwa yao. Die zeit linaandika, hadi sasa haifahamiki wazi ni Wapalestina wangapi Trump anaotaka kuwahamishia mahali gani, kwa wakati upi na mchakato wenyewe pia haufahamiki. Pia haijulikani ni kwa namna gani Rais huyo anataka Marekani iwe na udhibiti katika ukanda wa Gaza.
die tageszeitung
Kuhusu yanayoendelea kwenye vita vya Sudan, die tageszeitung limeandika kuwa, karibu miaka miwili baada ya kuanza kwa vita nchini Sudan ambako kuna tatizo kubwa zaidi la wakimbizi na baa baya zaidi la njaa duniani, huenda muafaka ukawa karibu kufikiwa.
Majeshi ya serikali ya Sudan yakiongozwa na Jenerali Abdelfattah al-Burhan yanakaribia kuwashinda wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa Rais Mohamed Hamdan Daglo, na kuwaondoa kabisa kutoka mji mkuu Khartoum. Kama hili likifanikiwa, basi serikali itakuwa imeshinda vita.
Hata hivyo, mafanikio ya jeshi la Sudan ya hivi karibuni likisaidiwa na wanamgambo wa ndani ya Sudan, dhidi ya RSF yanajiri wakati pia kukiwa na mashambulizi yanayowalenga raia wasio na hatia.
Serikali ya Sudan imeanzisha pia vita vya kiuchumi dhidi ya RSF vinavyowagharimu pia raia. Mwezi Desemba ilizitambuisha noti mpya za fedha zinazotolewa katika baadhi ya benki zilizoidhinishwa pekee na zinatolewa kwa kiwango maalumu, pauni 200,000 za Sudan sawa na dola 80 za kimarekani kwa kila mteja.