Afrika katika magazeti ya Ujerumani
31 Januari 2025Berliner Zeitung
Karibu magazeti yote ya Ujerumani juma hili yameumulika mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Berliner Zeitung limeandika, baada ya siku kadhaa za mapambano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo, waasi walifanikiwa kuingia Goma mji mkuu wa Kivu Kaskazini ulio katika eneo tajiri zaidi kwa rasilimali nchini Kongo, linalopakana na Rwanda.
Ripoti ya Ofisi ya kuratibu misaada ya dharura ya Umoja wa Mataifa OCHA imearifu kuwa katika mji huo ambao ni makazi ya zaidi ya watu 300,000, kuna wanaokimbia pia kutoka kwenye kambi za watu waliiolazimika kuyahama makazi kutokana na mzozo. Wafanyakazi wa ofisi hiyo wameripoti kuwa walishudia miili ya watu waliouwawa ikiwa imetapakaa mitaani. Nalo Shirika la Afya duniani WHO limebainisha kwamba hospitali mjini Goma zimefurika majeruhi.
Süddeusche Zeitung
Kuhusu mzozo huouo, Süddeusche linaandika, usiku wa kuamkia Jumatano, kwa mara ya kwanza Rais wa Rwanda Paul Kagame alizungumzia hali ya mji wa Goma ulio kwenye mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mpakani na Rwanda.
Kupitia ukurasa wake wa jukwaa la mtandao wa kijamii wa X, alibainisha kuhusu "mazungumzo yenye tija ” aliyoyafanya na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio. Wawili hao walizungumza kuhusu umuhimu wa kupata makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kushughulikia kiini cha mzozo huo. Süddeutsche zeitung linaongeza kuwa, hata hivyo Kagame hakusema lolote kuhusu mchango wake katika inachoendelea Goma.
Kulingana na gazeti hili, kwa muda mrefu Kagame amekuwa akikanusha kuhusika kuwapatia msaada wa kijeshi waasi wa M23, lakini hajawahi kufanya siri ukweli kuwa, yuko katika upande wa waasi hao kwenye mzozo huo wa mashariki mwa Kongo.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine lenyewe limeandika kuhusu uhusiano unaozidi kuzorota kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na bara la Afrika. Mhariri ameanza kwa kueleza kwamba, Donald Trump, hakuonesha nia yoyote ya kujihusisha na Afrika hata wakati wa muhula wake wa kwanza wa Urais. Aliwahi kujitungia jina la nchi ya Kiafrika aliyoiita "Nambia", katika moja ya hotuba zake. Aliwahi pia kuitaja kimakosa Uhispania kama mwanachama wa kundi jipya la nchi zinazoinukia kiuchumi la BRICCS badala ya Afrika Kusini.
Baadhi ya amri na maagizo aliyotoa baada ya kuapishwa kwake kama Rais wa Marekani, yamesababisha mkanganyiko katika bara la Afrika, hasa katika sekta ya afya. Moja wapo ni baada ya kutangaza kujitoa katika Shirika la Afya duniani WHO hasa ikizingatiwa kuwa Marekani ndiyo mchangiaji mkubwa katika bajeti ya shirika hilo ambapo inatoa humusi ya bajeti nzima.
Takriban watu milioni 400 hasa wa Afrika hawapati huduma muhimu za Afya na wanategemea sana mashirika ya kimataifa kama vile WHO kama anavyosema Mkurugenzi wa kituo cha usimamizi wa Afya barani Afrika katika Chuo kikuu cha Stellenbosch Munya Saruchera. Kujitoa kwa Marekani kwenye shirika hilo ni kitisho kikubwa kwa mifumo dhaifu ya afya barani humo. Hata hivyo hatua hiyo ya Marekani inatoa nafasi kwa Afrika kuwa huru zaidi na kuzidisha ushirikiano wa kikanda ili kujenga mifumo imara ya huduma za afya.
Süddeutsche Zeitung
Süddeutsche lenyewe lilikuwa na kichwa cha habari Kinachouliza Bolle Jos anafanya nini Sierra Leone?
Jos Leijdekkers almaarufu "Bolle Jos" ni mmoja wa wahalifu wanaotafutwa zaidi Uholanzi na mmoja wa vinara wa kimataifa wa biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya coccaine. Polisi ya Uholanzi ilitangaza dau la Euro 200,000 kwa atakayetoa taarifa zozote zitakazosaidia kukamatwa kwake. Mwaka uliopita alishtakiwa Uholanzi kwa ulanguzi wa dawa za kulevya, ujambazi kwa kutumia silana na kwa kuagiza watu kufanya mauaji kwa niaba yake lakini kila mara alifanikiwa kukwepa mkono wa sheria.
Kwa muda mrefu, wapelelezi walihisi kuwa Leijdekkers alikuwa Uturuki. Mwishoni mwa juma, vyombo viwili vya habari viliporipoti kuhusu mhalifu huyo kuonekana Sierra Leone. Huko, inadaiwa alijitambulisha kama mfanyabiashara mwenye uraia wa Uturuki na Norway. Shirika la habari la Reuters lilichapisha picha mnato na video ikimuonesha Mholanzi huyo mwenye miaka 33 akiwa amesimama katika mstari wa tatu nyuma ya Maada Bio karibu na mtoto wa kike wa Rais, anayehisiwa kuwa naye kweye uhusiano wa kimapenzi. Alionekana akiwa amefuga ndevu, na fulana yenye rangi ya njano na nyeusi akiwa mzungu pekee kwenye picha hizo. Hapo ndipo teknolojia ya kutambua uso ilipothibitisha kumtambua bila mashaka yoyote.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Uholanzi inasema inafanya kila liwezekanalo kupata kibali cha kumrejesha mhalifu huyo nchini mwake ili afikishwe mbele ya sheria. Hii haitokuwa kazi rahisi kwani kulingana na vyombo vya habar vya Uholanzi, uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Sierra Leone ni dhaifu sana au hata haupo kabisa . Wapelelezi hawasemi kuhusu hatua zozote ambazo zimeshachukuliwa katika miezi ya hivi karibuni na kwa sasa Jos Leijdekkers anaonekana kujihisi yuko salama Sierra Leone