Afrika katika magazeti ya Ujerumani
2 Desemba 2022Frankfurter Allgemeine
Gazeti la Frankfurter Allgemeine juu ya kushambuliwa kwa mtu aliyemuua Chris Hani aliyekuwa mpinga utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini. Janusz Walus aliyekuwa anatumikia kifungo cha maisha jela alishambuliwa baada ya kupatikana habari kwamba ataachiwa huru. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema uamuzi wa kuachiwa huru kwa muuaji huyo umesababisha maandamano makubwa kwenye mji wa Pretoria.
Gazeti linatilia maanani kwamba maandamano hayo yaliitishwa kwa pamoja na chama tawala cha ANC, chama ndugu cha kikomunisti na jumuiya ya wafanyakazi. Gazeti hilo linakumbusha kwamba muuaji huyo mhamiaji kutoka Poland alimpiga risasi mpigania uhuru Chris Hani mnamo mwaka 1993. Janusz Walus alishambuliwa na mfungwa mwingine Jumanne iliyopita. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limekariri habari zinasosmea kuwa mtu aliyemshambulia Janusz Walus kwa kisu ni shabiki mkubwa wa chama tawala cha ANC. Gazeti hilo linafahamisha kwamba mahakama ya katiba ya Afrika Kusini iliamua kumwachia huru Janusz Walus baada ya kusota jela kwa miaka 30. Gazeti limemnukulu mjane wa Chris Hani akisema kuwa uamuzi huo ni kitendo cha usaliti.
Der Tagesspiegel
Gazeti la Der Tagesspiegel limeandika juu ya harakati za ulinzi wa mazingira nchini Uganda. Linaeleza kwamba baada ya mafuta kugudunduliwa nchini humo mnamo mwaka 2006 makampuni makubwa ya kimataifa kutoka Ulaya na China yalianza kukaa mkao wa kula. Gazeti la Der Tagesspiegel linasema serikali ya Uganda imeahidi neema ya kiuchumi kwa watu wa nchi hiyo. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba kabla ya neema hiyo kuonekana baadhi ya wananchi watapaswa kuhamishwa kutoka kwenye maskani zao.
Asasi ya ulinzi wa mazingira inayosimamia nishati na utawala bora inapinga mipango hiyo na kwa ajili hiyo imetunukiwa nishani mbadala ya kutambua na kuunga mkono juhudi za kutatua matatizo makubwa ya wakati huu. Gazeti linafahamisha kuwa harakati za asasi hiyo zinaelekezwa dhidi ya mradi wa bomba la mafuta la kilometa 1443 la kupeleka mafuta Tanzania kutoka Uganda. Msemaji wa asasi hiyo ya ulinzi wa mazingira Diana Nabirima amekaririwa na gazeti la Der Tagesspiegel akisema wanaendesha harakati zao katika hali ya wasi wasi. Amesema hakubaliani na ahadi iliyotolewa na serikali ya Uganda kuwa mradi huo wa bomba la mafuta utaleta neema kwa watu wa Uganda.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linazungumzia juu ya mashambulio ya ndege yaliyofanywa kwenye mji wa kaskazini wa Bossangoa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati. die tageszeitung linaita mashambulio hayo kuwa ni hadithi. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya nchi hiyo mashambulio hayo yaliwalenga washirika wake mamluki wa Urusi. Gazeti hilo limekariri taarifa ya serikali ikisema kuwa makao makuu ya jeshi pamoja na washirika wa Jamhuri ya Afrika ya Kati walilengwa katika mashambulio hayo. Linasema serikali imelalamika juu ya madhara makubwa yaliyosababishwa na mashambulio hayo. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyokaririwa na na gazeti die tageszeitung ndege iliyofanya mashambulio hayo ilitoweka kuelekea kaskazini.
Gazeti la die tageszeitung linaeleza kwamba wanaoitwa washirika wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ni wanajeshi na washauri wa kijeshi wa Urusi waliopo katika nchi hiyo ya Afrika ya kati. Gazeti hilo linafahamisha kwamba katika nchi jirani ya Tchad pana kituo cha kikosi cha anga cha Ufaransa.Gazeti linasema Ufaransa na Urusi zinashindana katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwamba hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati imezidi kuwa mbaya tangu mwezi Oktoba wakati ambapo rais Mahamat Idriss alipotumia mabavu kuwazima waandamanaji.
Neue Zürcher Zeitung
Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya mgogoro wa nchini Ehtiopia na linauliza iwapo nchi jirani ya Eritrea inajaribu kuhujumu amani nchini humo. Gazeti hilo linaeleza kwamba waasi wa Tigray na serikali kuu wametia saini hati mbili juu ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa matumaini ya kuutatua mgogoro wa nchini Ethiopia. Lakini gazeti la Neue Zürcher linasema hata baada ya miezi miwili tangu makubaliano hayo kufikiwa majeshi ya nchi jirani ya Eritrea bado yameendelea kuwamo kwenye jimbo la Tigray.
Miongoni mwa masharti ya kusimamisha mapigano ni kuondolewa kwa majeshi ya nchi za nje ambayo ni majeshi ya Eritrea, Hata hivyo gazeti la Neue Zürcher linasema waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anapaswa kulipa deni. Gazeti linasema majeshi ya Eritrea yalimsaidia Abiy Ahmed katika vita vyake dhidi ya waasi wa Tigray.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen