Afrika katika Magazeti ya Ujerumani
18 Novemba 2022Handelsblatt
Gazeti la Handelsblatt. Gazeti hili limeandika juu ya kuongezeka kwa umuhimu wa bara la Afrika kiuchumi duniani. Na linasema tangu kuanza kwa vita vya nchini Ukraine bara la Afrika linajitokeza kuwa chanzo mbadala cha nishati zinazohitajika duniani. Linasema wajasirimali wa Ujerumani wanaweza kuona jinsi fursa zinavyoongezeka. Hata hivyo linatilia maanani kwamba mshindani mkubwa ni China. Gazeti la Handelsblatt linaeleza kuwa urari wa mahusiano sasa hauko wazi kama jinsi ilivyokuwa hapo awali. Linasema China ni mshiriki mkuu wa nchi za Afrika. Handelsblatt linasema China imejijenga barani Afrika kwa muda mrefu kutokana na kuwekeza mabilioni katika miradi mbalimbali siyo tu ya miundombinu bali pia katika malighafi. Na ndiyo sababu Ujerumani inashauriwa kufikiria upya sera zake juu ya bara la Afrika.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linazungumzia juu ya hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Linasema hali iliyotokea miaka 10 iliyopita inatishia kujirudia kwenye sehemu hiyo. Gazeti hilo linaeleza kwamba wakati huo, waasi wa kundi la M23 waliuteka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma baada ya wanajeshi wa serikali kuukimbia. Gazeti la die tageszeitung linaarifu kwamba hali ya wasiwasi imetanda miongoni mwa raia na maalfu kwa maalfu wameshakimbia kutoka kwenye maeneo ya mapigano na kuelekea kwenye mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma kutokana na mashambulio yanayofanywa na waasi wa kundi la M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Gazeti la die tageszeizung linasema mapambano sasa yanaendelea kwenye eneo la kilometa 10 kati ya majeshi ya serikali na waasi wa M23. Na kwa mujibu wa taarifa zilizokaririwa na gazeti hilo, waasi wanasonga mbele. Hata hivyo kiongozi wa waasi hao bwana Bertrand Bisimwa ameliambia gazeti la die tageszeitung kwamba nia yao si kuyakalia maeneo wanayoyateka bali ni kufanya mazungumzo na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Gazeti la die tageszeitung linaarifu kwamba rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta amewasili nchini Kongo katika juhudi za kupatanisha. Hata hivyo gazeti hilo linasema serikali ya Kongo imekataa kufanya mazungumzo na waasi wa kundi hilo la M23. Wajumbe wa makundi kadhaa ya waasi wanapaswa kushiriki kwenye mazungumzo na serikali ya Kongo chini ya upatanishi wa Uhuru Kenyatta ambaye ametoa wito wa kuvimaliza vita kwanza na baadae kuanza mazungumzo.
Neue Zürcher
Gazeti la Neue Zürcher wiki hii limeandika juu ya janga la maradhi ya Ebola nchini Uganda. Linasema nchi hiyo sasa imeanza majaribio ya chanjo. Linaarifu kwamba miezi miwili baada ya janga hilo kuzuka majaribio ya chanjo yameanza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus dozi za kwanza zinatarajiwa wiki ijayo. Gazeti la Neue Zürcher limekariri taarifa ya shirika la WHO zinazosema kuwa watu 22 wameshakufa kutokana na maambukizi ya virusi vya Ebola nchini Uganda wengine zaidi ya 140 wameambukizwa na 22 miongoni mwao wamelazwa hospitalini. Hata hivyo gazeti linasema wagonjwa wapatao 73 wamepona.
Kölnische Rundschau
Gazeti la Kölnische Rundschau linatuarifu kwamba serikali ya Ujerumani imeamua kuyaondoa majeshi yake kutoka Mali hadi hapo itakapofika mwishoni mwa mwaka ujao. Gazeti hilo linaeleza kwamba uamuzi huo umefikiwa baada ya mazungumzo ya siri ya viongozi wa serikali. Mazungumzo hayo bado yanaendelea na uamuzi kamili utatangazwa punde tu.
Gazeti la Kölnische Rundschau linafahamisha kwamba majeshi ya Ujerumani yalipelekwa nchini Mali kuwa sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini humo. Hata hivyo linasema nchi kadhaa zimeshayaondoa majeshi yao kutoka Mali. Gazeti linaeleza kwamba tangu wanajeshi kutwaa mamlaka nchini Mali mnamo mwaka 2021 ushirikiano na majeshi ya Umoja wa Mataifa umezidi kuwa mgumu.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen