Afrika katika magazeti ya Ujerumani
11 Februari 2022Süddeutsche Zeitung
Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya kimataifa ya mjini the Hague inayoitaka Uganda iilipe Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo fidia ya dola milioni 325. Gazeti linafahamisha kuwa Uganda inatakiwa ilipe fidia hiyo kutokana athari ilizosababisha kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa vita.
Gazeti linaeleza kuwa mahakama imeweza kuthibitisha kwamba Uganda ilipeleka majeshi mashariki mwa Kongo na kwamba wanajeshi wake walisababisha vifo vya maalfu ya watu na madhara mengine kwenye jimbo la Ituri huko mashariki mwa Kongo. Gazeti la Süddeutsche linaeleza kuwa wanajeshi hao wa Uganda pia walipora madini ya nchi hiyo.
Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa inayoamua mizozo baina ya mataifa ilifikia uamuzi kwamba mnamo mwaka 2005, Uganda ilikiuka sheria za kimataifa kwa kupeleka majeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kölner Stadt-Anzeiger
Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linaelezea wasi wasi huenda Mali ikawa nchi iliyoanguka. Gazeti hilo linasema hayo baada ya wanajeshi kupora mamlaka. Linasema wasi wasi unaongezeka juu ya Mali kusambaratika. Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linaeleza kuwa wanajeshi wa Ujerumani wamekuwapo nchini Mali ili kuisaidia nchi hiyo kupambana na magaidi. Hata hivyo linauliza iwapo litakuwa jambo la manufaa kwa wanajeshi hao kuendelea kuwamo nchini Mali baada ya wanajeshi kuiangusha serikali.
Gazeti limemnukulu naibu waziri wa Ujerumani anayeshughulikkia sera za nje Katja Keul akisema kuwa hali ya nchini Mali imekuwa mbaya baada ya wanajeshi kupora mamlaka na kuisimamisha katiba.
Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linasema utawala wa kijeshi nchini Mali unapaswa kutayarisha mpango wa kuirejesha nchi kwenye uongozi wa kidemokrasia. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba ni hatua ya kutia moyo kwamba, Umoja wa Afrika umeingilia kati na linaeleza kuwa wanajeshi wa Ujerumani wamekuwa wanatoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali chini ya mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuisaida Mali katika juhudi za kupambana na magaidi.
Die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linazungumzia uvumi juu ya njama za kuiangusha serikali ya rais Felix Tshisekedi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya mshauri wake wa maswala ya usalama kukamatwa. Gazeti linasema tuhumua hizo zinaelekezwa pia kwa rais wa hapo awali Joseph Kabila.
Gazeti linaeleza kwamba mshauri huyo wa rais, bwana Francois Beya alikuwa afisa wa ngazi ya juu wakati wa utawala wa Joseph Kabila, ambaye aliendelea kuwamo katika serikali ya sasa ya rais Felix Tshisekedi. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kwamba rais Tshisekedi alifanya mabadiliko kwa kuwaondoa wafuasi wengi wa Joseph Kabila lakini alimwacha bwana Beya katika serikali yake. Gazeti hilo linakumbusha kuwa Tshisekedi aliingia madarakani kutokana na hisani ya rais wa hapo awali.
Hatahivyo aliamua kuwatimua watu wa Kabila. Lakini uamuzi wa Tshisekedi kuwaalika wanajeshi wa Uganda kushiriki katika mapigano dhidi ya kundi la waasi wa ADF umewashtua watu hao wa Kabila waliotimuliwa. Sababu ni kwamba ikiwa majeshi ya Uganda yatafanikiwa kuwashinda waasi wa ADF biashara wanazofanya na waasi hao zitafichuka. Jee serikali ya Tshisekedi imo hatarini kupinduliwa linauliza gazeti la die tageszeitung.
Die Welt.
Makala ya gazeti la Die Welt inazungumzia juu ya Umoja wa Ulaya kunasa kwenye mtego wa uhamiaji. Sababu ni kwamba mikataba ambayo ingeweza kuepusha mtego huo ni dhaifu.
Gazeti linasema maalfu ya wahamiaji barani Afrika wanasubiri kuvuka bahari ya Mediterania na kwenda barani Ulaya. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba watu zaidi ya 4,400 walikufa hivi karibuni wakiwa njiani kwenda Uhispania na linauliza jee serikali mpya ya Ujerumani inapaswa kuleta mabadiliko katika sera ya uhamiaji? limemnukulu waziri wa mambo ya nje Annalena Baerbock akisema kwamba mpango mpya maalumu unahitajika. Amesema sera juu ya uhamiaji inayotumika sasa ina mapungufu.
Gazeti la Die Welt linasema mikataba juu ya uhamiaji iliyofikiwa na nchi za Afrika haina mashiko madhubuti na kutokana na hali hiyo gazeti linasema hautapita muda mrefu kabla ya kuyaona mawimbi mengine ya wakimbizi ikiwa sera sahihi hazitawekwa!
Vyanzo: Deutsche Zeitungen