Afrika katika magazeti ya Ujerumani
25 Juni 2021Süddeutsche Zeitung
Gazeti la Süddeutsche juu ya taarifa za Umoja wa Mataifa kuhusu baa la njaa kwenye jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Gazeti hilo limenukuu taarifa za wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaosema kwamba watu wapatao 350,000 wamekumbwa na baa la njaa kwenye jimbo hilo na kwamba wengine milioni 2 wamo hatarini kukumbwa na janga hilo.
Gazeti la Süddetsche linasema waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameeleza tu kwamba anatambua tatizo la jimbo la Tigray bila ya kutoa maelezo jinsi atakavyolitatua tatizo hilo. Gazeti linaeleza kwamba baa la njaa ni matokeo ya vita vya hivi karibuni katika sehemu hiyo na linasema mgogoro wa jimbo la Tigray bado unaendelea na unaweza kuliathiri eneo lote la upembe wa Afrika ambalo limekuwa linayumba! Süddeutsche linasema jimbo la Tigray linaonyesha hatari ya kugawanyika kwa Ethiopia.
Frankfurter Allgemeine Zeitung,
Makala ya gazeti la Frankfurter Allgemine inazungumzia juu ya kuaga dunia kwa kwa mwasisi wa taifa huru la Zambia, Dr.Kenneth Kaunda. Gazeti hilo linasema mara tu baada ya taarifa juu ya kifo cha Kaunda kusikika salamu za rambirambi zilianza kumiminika kutoka barani Afrika kote. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limetilia maanani kwamba hata rika la vijana ambalo lilikuwa bado halijaja duniani wakati wa uongozi wa Kaunda, nalo pia limetoa salamu za rambi rambi.
Frankfurter Allgemeine limeandika kwamba Kaunda alikuwa miongoni mwa waasisi wa kwanza wa mataifa ya Afrika. Alikuwa mpigania uhuru wa nchi yake na alitoa mchango katika harakati za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kaunda alikuwa rais wa kwanza wa Zambia na maarufu siyo tu nchini mwake.
Hata hivyo gazeti hilo linakumbusha kwamba Kaunda alikuwa mtetezi mkubwa wa siasa ya utawala wa chama kimoja na alivipiga marufuku vyama vyote vya upinzani ila hakufika mbali katika hilo gazeti linasema. Kutokana na bei ya shaba kuanguka na kutokana na gharama za maisha kupanda shinikizo dhidi yake liliongezeka.
Hatimaye alikubali mfumo wa siasa wa vyama vingi na baada ya uchaguzi kiongozi wa upinzani Frederic Chiluba alishinda. Gazeti linakumbusha kwamba Dr. Kaunda alikubali kushindwa kwa hadhi na taadhima na ataendelea kukumbukwa kwa hilo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Kaunda atakumbukwa pia kwa juhudi alizofanya ili kuleta amani kwenye maeneo ya migogoro.
die tageszeitung,
Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya kurejea nyumbani kwa Laurent Gbabo aliyekuwa rais wa Ivory Coast kuanzia mwaka wa 2000 hadi 2010. Gazeti hilo linasema Gbagbo alipokewa kwa shangwe na wafuasi wake. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linaeleza kwamba kurejea kwa bwana Gbagbo kunaweza kuleta moja kati ya mambo mawili, ama maridhiano au mgogoro nchini Ivory Coast.
Gazeti hilo linakumbusha kwamba Gbagbo alishindwa katika uchaguzi na mshindani wake Alassane Ouattara mnamo mwaka 2010. Lakini Gbagbo hakuyatambua matokeo ya uchaguzi na aliendelea kujiweka madarakani kwa mabavu. Hata hivyo waasi walioungwa mkono na Ufaransa walimwondoa madarakani kwa nguvu. Gbagbo alikamatwa pamoja na mkewe na baadaye alipelekwa kwenye mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague. Mnamo mwaka 2019 mahakama hiyo ilimfutia Gbagbo tuhuma juu ya uhalifu uliotendwa na wafuasi wake baada ya kukata rufaa. Gazeti la die tageszeitung linasema rais Ouattara na pia bwana Gbagbo hakuna mwenye hamu ya vita. Hata hivyo linatilia maanani kwamba wafuasi wa Gbagbo hawafikirii kwamba amerejea nyumbani ili kuwa mstaafu tu.
Der Tagesspiegel
Gazeti la Der Tagesspiegel linazungumzia juu ya uamuzi wa Ubelgiji wa kurejesha Afrika kazi za sanaa zilizoporwa wakati wa ukoloni. Gazeti hilo limemnukulu naibu waziri wa masuala ya sayansi akisema, kile ambacho kimechukuliwa kinyume cha sheria hakiwezi kuwa chetu! Gazeti la Der Tagesspiegel linasema naibu waziri huyo ametoa kauli hiyo baada ya serikali ya Ubelgiji kupitisha uamuzi wa kurudisha kazi za sanaa zilizoporwa na wakoloni katika nchi za Afrika, ikiwa pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Sanaa hizo zimewekwa kwenye nyumba ya ukumbusho juu ya Afrika iliyoko nchini Ubelgiji. Gazeti hilo linafahamisha kwamba kati ya mwaka 1885 hadi 1960 vitu vya sanaa zaidi ya 80,000 vilichukuliwa kutoka Afrika na kuhamishiwa Ubelgiji kinyume cha sheria. Gazeti la Der Tagesspiegel linafahamisha kwamba mfalme Philippe wa Ubelgiji alimwandikia barua rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi kumwomba radhi juu ya vitendo vya kihalifu vilivyofanywa na wabelgiji nchini Kongo wakati wa ukoloni.
Gazeti la Der Tagesspiegel linatilia maanani kwamba uamuzi wa serikali ya Ubelgiji unatokana pia na shinikizo la kampeni maarufu ya "Black Lives matter", yaani maisha ya watu weusi yana thamani. Dunia bado inakumbuka kwamba maalfu kwa maalfu ya wakongo waliuliwa wakati wa ukoloni wa wabelgiji chini ya utawala wa mfalme Leopold wa pili.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen