Afrika katika magazeti ya Ujerumani
6 Novemba 2020Süddeutsche Zeitung
Gazeti la Süddeutsche linasema waziri mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed aliyetunukiwa nishani ya amani ya Nobel sasa amegeuka kuwa kamanda wa kuandaa majeshi tayari kutumia nguvu kwenye jimbo la Tigray. Gazeti hilo linakumbusha kuwa ni mwaka mmoja tu uliopita ambapo mwanamageuzi huyo alitunukiwa nishani hiyo lakini sasa amejikuta katika hali ambapo analazimika kulitumia jeshi.
Gazeti la Süddeutsche limemnukulu Waziri Mkuu Abiy akisema kwamba amechukua hatua hiyo ili kuiepusha Ethiopia na hatari ya kutumbukia katika vurumai. Bwana Abiy anawalaumu viongozi wa jimbo la Tigray kwa kusababisha mazingira yanayoweza kuleta vita vya nchini Ethiopia. Abiy ameeleza kuwa kituo cha jeshi la serikali kiilivamiwa ambapo wavamizi walijaribu kuteka silaha nzito. Kiongozi huyo amesema jambo hilo haliwezi kuvumiliwa.
Hata hivyo gazeti la Süddeutsche linasema waziri mkuu Abiy Ahmed aliyemwagiwa sifa maridhawa sasa anakabiliwa na mtihani mkubwa tangu alipoingia madarakani na kuanza kuleta mageuzi. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba tangu mwanzoni kabisa yalikuwapo mashaka juu ya waziri Mkuu Abiy Ahmed kuweza kuyatekeleza mageuzi aliyoyaanzisha kutokana na mvutano kati ya serikali kuu ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Jimbo hilo linahisi kutengwa na serikali kuu ya mjini Addis Ababa.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya ushindi wa rais Alassane Ouattara katika uchaguzi mkuu wa nchini Ivory Coast. Die tageszeitung linasema ushindi huo hata haupendezi. Rais Ouattara alishinda kwa kupata asilimia 94.27 ya kura. Watu milioni 3 na laki tatu walimpigia kura. Gazeti linasema, idadi hiyo inawakilisha asilimia 53.9 ya watu wote waliojitokeza kupiga kura. Wapinzani hawayatambui matokeo hayo.
Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba mkakati wa wapinzani kususia uchaguzi haukuwa mzuri. Gazeti linasema wapinzani wameunda baraza la serikali ya kitaifa ya mpito, lakini gazeti linasema hakuna anayejua kwa uhakika malengo ya baraza hilo. Hata hivyo baraza hilo limetoa mwito wa kutoitii serikali ya Ouattara na kufanya maandamano lakini serikali imeshapiga marufuku maandamano.
Gazeti hilo la die tageszeitung limewanukulu waangalizi wa uchaguzi wakisema kwamba utaratibu wa upigaji kura haukuwa mzuri. Waangalizi hao wamesema katika muktadha wa kisiasa unaojiri nchini Ivory Coast ilikuwa vigumu kwa uchaguzi kuwa huru na wa haki. Hata hivyo gazeti hili limeunukulu Umoja wa Afrika ukisema kwa jumla uchaguzi ulienda vizuri licha ya mazingira yaliyokuwapo. Bora uchaguzi mbaya kuliko kumwagika damu!
Frankfurter Allgemeine Zeitung
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya machafuko yaliyotokea nchini Nigeria kwa muda wa wiki kadhaa sasa. Watu wamekuwa wanafanya maandamano kupinga ukatili wa kikosi maalumu cha polisi SARS kilichoundwa kwa ajili ya kupambana na majambazi. Gazeti hili limechapisha mahojiano na mwanasheria mmoja anayefanya kazi mjini Lagos, Adunni Jonas.
Mwanasheria huyo ameliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba watu nchini Nigeria wanapinga hasa njia zinazotumiwa na polisi hao dhidi ya wananchi. Adunni Jonas ameeleza kwamba polisi hao wanamkatama mtu wakimwona amevaa saa nzuri ama akiwa anaendesha gari la kifahari kwa kumtuhumu kwamba ameiba.
Jonas ameliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba polisi hao wakati mwingine wanawabana watu wawape fedha. Lakini vibaya zaidi amesema polisi hao wanatumia nguvu. Watu wengi waliokamatwa na hawajarudi makwao muda mrefu sasa umepita. Mwanasheria huyo ameliambia gazeti hilo kwamba maandamano ya kukipinga kikosi hicho cha polisi yamefanyika wakati Nigeria inaadhimisha miaka 60 tangu ijipatie uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Uingereza. Watu wameambatanisha maandamano dhidi ya polisi na swali, juu ya kile kilichofanyika katika miaka hiyo 60.
Die Welt
Gazeti la Die Welt linauliza kwa nini bara la Afrika halikuathirika na janga la corona kama ilivyohofiwa hapo awali? Gazeti hilo linasema nchi 54 barani Afrika zimeepuka maafa makubwa, linasema hapo awali palikuwapo na wasi wasi mkubwa kutokana na mifumo dhaifu ya huduma ya afya na hasa kwenye sehemu za vijijini.
Gazeti hilo linasema asilimia 17 ya watu duniani kote wanaishi barani Afrika lakini mpaka sasa watu waliokufa barani humo kutokana na janga la corona ni asilimia 3.5 ya jumla ya watu wote waliokufa duniani. Gazeti la Die Welt linalitia maanani kwamba, miezi sita tu baada ya kuzuka janga la corona, nchi kadhaa za Afrika hata zimeweza kupokea watalii kutoka nje ikiwa pamoja na kutoka Ujerumani.
Gazeti hilo limewanukulu wataalamu wakieleza kwamba miongoni mwa sababu za idadi ndogo ya vifo barani Afrika kuwa ni umri wa watu wake. Wakati nchini Ujerumani umri wa wastani ni miaka 47, nchini Kenya kwa mfano, umri wa wastani ni miaka 20.
Vyanzo: Deutsche Zeitungen