Afrika katika magazeti ya Ujerumani
6 Machi 2020die Tageszeitung
Gazeti la Die Tageszeitung linaeleza kwamba watu nchini humo wanasema wadau ni wale wale ila mazingira yamebadilika kidogo. Wahusika wakuu, rais Salva Kiir na hasimu wake ambaye ni kiongozi wa upinzani, Riek Machar walikutana mwishoni mwa mwezi Februari na walizindua serikali ya umoja wa kitaifa ya Sudan Kusini. Rais Salva Kiir alikaririwa akisema hatua hiyo maana yake ni kumalizika kwa vita nchini humo.
Hata hivyo bado hawajakubaliana juu ya kugawana nyadhifa za mawaziri. Gazeti la die Tageszeitung linasema mzizi wa fitina ni idadi ya majimbo. Rais Salva Kiir aliigawanya Sudan Kusini katika majimbo 32 ili kuweza kuwapa mamlaka watu wake wa kabila la Wadinka na hivyo kuimarisha utawala wake. Kabla ya hapo Sudan kusini iligawanyika katika majimbo 10 tu. Utaratibu huo ndiyo sasa unaotarajiwa kurejeshwa chini ya serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo huenda mambo yakawa magumu kwa sababu Rais Kiir na mpinzani wake Riek Machar hawagombei mamlaka tu bali pia utajiri wa mafuta uliopo kwenye baadhi ya majimbo.
Süddeutsche
Gazeti la Süddeutsche wiki hii linatupeleka Djibouti nchi iliyoko kwenye pembe ya Afrika. Jee kunatokea nini huko? Gazeti hilo linasema hapo ni mahala ambapo Wamarekani, Wachina, Warusi na wawakilishi kutoka nchi za Ulaya magharibi wanakutana -vurugu mechi kwa lugha ya mitaani.! - Djibouti inanufaika kifedha kutokana na watu kukutana kutoka mataifa hayo mbalimbali. Nchi hiyo, iliyoko kwenye pembe ya Afrika, inafanya biashara ya kukodisha ardhi yake kwa majeshi ya nchi za nje. Majeshi hayo yanatumia ardhi ya Djibouti kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kijeshi.
Gazeti la Süddeutsche linasema nchi hizo zinalenga maslahi makubwa zaidi. Shabaha ni kuweza kuudhibiti mlango wa kuingilia barani Afrika na linakumbusha kwamba baada ya kutokea mashambulio ya kigaidi mwezi Septemba mwaka 2001, Marekani ilipeleka wanajeshi wake 4000 nchini Djibouti ambako wamejenga kituo kikubwa cha kijeshi.
Neue Zürcher
Gazeti la Neue Züzcher linaeleza kwamba sehemu nyingine za Afrika zimo katika hatari ya kupoteza misitu kutokana na kukata miti kwa ajili ya kilimo na biashara. Gazeti hilo linasema kilimo cha kukidhi mahitaji ya chakula kimesababisha ukataji wa miti, katika nchi zenye misitu mikubwa na kusababisha misitu hiyo izidi kupungua na linaeleza zadi kwamba misitu ya bonde la Kongo iko kwenye sehemu yenye ukubwa wa karibu hekta milioni 170.
Misitu hiyo ya mvua ni ya pili kwa ukubwa duniani baada ya ile ya Amazon, katika Amerika ya Kusini. Misitu hiyo ni maskani ya watu na wanyama na pia inahifadhi hewa ya ukaa lakini inatoweka. Hadi mwanzoni mwa mwaka wa 1900 Afrika ilikuwa na hekta milioni 350 za misitu lakini sasa thuluthi moja imeshapotea.
Gazeti la Neue Zürcher linasema mpaka sasa ni wakulima wa ndani ambao wamekuwa wanakata misitu kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya chakula lakini sasa wawekezaji wa kimataifa wanaikodolea macho misitu ya Afrika na serikali za Afrika nazo zinayauza maeneo makubwa kwa wafanyabiashara kutoka nje.
die tageszeitung
Makala nyingine ya gazeti la die Tageszeitung inatupasha habari za kutia moyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Gazeti hilo linatuelezajuu ya mgonjwa wa mwisho aliyekuwa anaugua maradhi ya homa ya Ebola, ametolewa hospitali baada ya kutibiwa kwa mafanikio. Mwisho wa kipindi cha mashaka unakaribia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maradhi ya homa ya Ebola yaliyoikumba nchi hiyo miaka miwili iliyopita yalisababisha vifo vya watu 2264. Ilikuwa siku ya furaha kubwa katika mji wa Beni mashariki mwa Kongo kumwona mama mmoja aliyekuwa na homa ya Ebola akitoka hospitali akiwa amepona. Habari hizo za kufurahisha zilithibitishwa na wawalikishi wa shirika la Afya duniani WHO.
Vyanzo:Deutsche Zeitungen