Afrika katika magazeti ya Ujerumani
23 Juni 2006Kufikishwa Charles Taylor mbele ya mahakama ya kimataifa mjini The Hague,juhudi za jumuia ya kujihami ya magharibi NATO barani Afrika,Vita vinaripuka mara moja lakini amani ni shida kuipata –hayo ni miongoni mwa mwa mada zilizochambuliwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii kuhusu bara la Afrika.
Tuanze lakini na kufikishwa rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor mbele ya korti kuu ya kimataifa ya uhalifu wa vita mjini The Hague.
“Katoka kwenye kiti cha rais kaangukia kwenye kiti cha mshitakiwa.Muimla wa zamani wa Liberia,amehamiashwa Sierra Leone na kupelekwa The Hague ,nchini Uholanzi anakokabiliwa na kesi dhidi ya uhalifu wa vita”-hicho ni kichwa cha maneno cha uchambuzi wa gazeti la mjini Berlin-Berliner Zeitung.Mhariri wa gazeti hilo aliyeko mjini Johanesburg, Frank Räther anasimulia jinsi mwanaasiasa huyo anaemtaja kua mwenye haiba alivyoporomoka kichwa chini miguu juu.Anasema kila kwa mara Charles Taylor mwenye umri wa miaka 58 amekua akipanda na baadae kuporomoka vibaya sana.Safari hii ameangukia mbele ya korti maalum ya kimataifa.
Alikua miongoni mwa wanafunzi wa Liberia waliokua uhamishoni ,mapinduzi ya kijeshi mwaka 1980 yaaliyoongozwa na Samuel Doe dhidi ya William Tolbert.Charles Taylor aliyekua kipenzi cha rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan,alikabidhiwa uongozi wa idara kuu ya ununuzi ya Liberia .Aliiba na kukimbia Marekani.Kifungo cha miezi 15 jela nchini Marekani kwasababu ya biashara haramu ya silaha ,hakukimaliza,alifanikiwa kutoroka.Hata nchini Nigeria alikokua akiishi uhamishoni alijaribu kutoroka kishindo cha kumkamata ili afikishwe mahakamni kwa uhalifu wa vita nchini Sierra Leone kilipozidi kukua.
Alikamatwa akiwa ndani ya Landrover ya dhahabu na masanduku mawili yaliyojaa pesa yakiwa na uzito wa kilogram mia moja.Hii leo lakini baada ya kufikishwa The Hague kitanzi kimemkaba Talyor hana njia ya kutoroka tena.
Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema “asiyekuwepo machoni na moyoni hayuko“Gazeti linazungumzia jinsi wanaharakati wa haki za binaadam walivyoshusha pumzi baada ya mtawala wa zamani wa Liberia kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa vita mjini The Hague.”Hakuna si Sierra Leone alikofanya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadam na wala si kwengineko kokote kule barani Afrika,hakuna aliyekua tayari kuandaa keshi dhidi yake.”
.Hata hivyo kwa wakaazi wengi wa Afrika kesi dhidi ya Taylor ni ushahidi timamu na wa kijasiri kwamba hata wababe wa vita wanaohofiwa,hawawezi tena kujinata wamesalimika.”Watu wasipoteze wakati,kesi inabidi ianze haraka” anasema mhariri wa Frankfurter Allgemeine,akimnukuu muendesha mashtaka mkuu Christopher Staker.Lakini mjini The Hague inahofiwa patahitajika miezi hadi kesi hiyo itakapoanza,seuze tena Charles Taylor hata wakili hana,anadai eti hana fedha za kumlipa wakili.
“Mbabe wa vita,mwizi na muaji”-hicho ni kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Bonn-General Anzeiger linalochambua maisha ya Charles Taylor tangu alipozaliwa kutoka katika familia masikini katika kijiji kimoja nje ya mji mkuu wa Liberia-Monrovia,hadi alipokwenda kusoma Marekani na kupanda kileleni,baada ya muimla mwengine Samuel Doe kupinduliwa na kuuliwa.
Nyota iliyomfikisha madarakani hakuisomea badala yake alikabwa na kiu cha kujitajirisha.Kiu hicho hicho ndio chanzo cha kuchochea vita katika nchi jirani ya Sierra Leone yenye utajiri wa dhahabu na almasi.Hata watoto wadogo hakuchelea kuwatumia kama wanajeshi .Linaandika gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn.
“Jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO inakwenda Afrika kwa masilahi yake wenyewe” linaandika gazeti la Tageszeitung.Vikosi vya kuingilia kati haraka barani Afrika imekua fashion hivi sasa.Makundi makubwa makubwa ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa nchini Liberia,Kongo na Sudan;kikosi cha Umoja wa Ulaya katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,vikosi vya Ufaransa nchini Ivory Coast,vikosi vya kigeni inaonyesha haviepukiki vinakutikana kila mahala katika juhudi za kulinda amani barani Afrika.
Na hata wanajeshi wa kuingilia kati haraka kutoka jumuia ya kujihami ya NATO,wanaandaliwa ili waweze kutumwa Afrika.Wanajeshi elfu sabaa wanafanya mazowezi katika visiwa vya Cape Verde,kusaba mbinu za kumaliza vita vya kuania mali ghafi barani Afrika.Na katika makao makuu ya NATO mjini Brussels kilichoingia midomoni mwa viongozi ni namna ya kudhamini nishati barani Afrika.
Ujerumani inakamata mstari wa mbele katika juhudi hizo za kulinda amani.Juhudi za kuligeuza jeshi la shirikisho Bundeswehr liweze kuwa jeshi la kuingilia kati mizozo inapozuka,zimeshaingia njiani na kuna hata mikakati ya jinsi ya kutetea masilahi katika sekta ya kibiashara, mali ghafi na kaadhalika.
Tume ya umoja wa ulaya katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo inaongozwa na Ujerumani na hata katika juhudi za vikosi vya NATO vya kuingilia kati haraka,Ujerumani itakua na mchango usio mdogo.