Afrika katika magazeti ya Ujerumani
25 Agosti 2006Tukianzia nchini Afrika Kusini, gazeti la Neue Zürcher, liliripoti juu ya shinikizo linalomkabili waziri wa afya wa Afrika Kusini la kumtaka ajiuzulu kutoka kwa wadhifa wake. Mnamo Jumatatu wiki hii kiongozi wa chama cha upinzani cha Independent Democrats, Patricia de Lille, alitaka waziri Manto Tshabalala Msimang ang´atuke baada ya shirika la kupigania matibabu ya ukimwi, TAC, nchini humo pia kumtaka waziri huyo ajiuzulu.
Mwito wa kujiuzulu waziri Tshabalala ulitolewa mara tu ujumbe wa Afrika Kusini ulipowasili kutoka mkutano wa kimataifa wa 16 kuhusu ukimwi uliofanyika mjini Toronto, Canada. Kwenye mkutano waziri Tshabalala alitangaza kwa wajumbe kwamba viazi sukari, mafuta ya zabibu na kitunguu thumu ni dawa ya kupunguza makali ya ukimwi na kupuuza dawa zinazotengezwa na wataalamu za ARV.
Msimamo wa serikali ulikuwa kuzipa nafasi ya mwanzo dawa wa ukimwi, hivyo matamshi ya waziri Tshabalala katika mkutano wa Toronto yalikosolewa vikali.
Mjumbe maalumu wa ukimwi wa Umoja wa Mataifa, Stephen Lewis, amesema sera ya ukimwi ya waziri Tshabalala ni porojo na ni ishara ya ukosefu wa elimu. Mhariri alisema Afrika Kusini ni nchi pekee barani Afrika ambayo haijapiga hatua yoyote katika vita dhidi ya ukimwi.
Mada ya pili ilihusu azma ya Afrika Kusini kutaka kuharakisha mabadiliko ya sheria za kumiliki ardhi. Mhariri wa gazeti la Neues Deutschland, alisema Afrika Kusini inaweza kumpokonya ardhi mkulima mzungu kufikia mwaka wa 2007. Sheria ya muuzaji wa hiari na mteja wa hiari, inaenda mwendo wa kinyonga kushinda mipango ya serikali ya kutaka kuwapa mashamba waafrika weusi.
Gazeti lilimnukulu waziri wa ardhi wa Afrika Kusini, Lulu Xingwana, akisema mjini Polokwane, mji mkuu wa jimbo la Limpopo, kuwa mazungumzo yataendelea kwa miezi sita kabla mzungu wa kwanza kupokonywa shamba. Rais Thabo Mbeki amemruhusu waziri wake kurekebisha sheria za ardhi kufikia mwaka wa 2008.
Gazeti la Rheinische Post, lilisema mhandisi wa kijerumani, Guido Sollinger Schiffarth, aliyezuiliwa na waasi wa eneo la Niger Delta nchini Nigeria kwa zaidi ya wiki mbili, aliachiliwa huru. Mhariri alimnukulu dadake Sollinger, Ursula Beier, akisema ilikuwa bahati ya mtende kwa kakake kuachiliwa.
Alisema pia kake ni mkarimu na anawapenda raia wa Niger Delta ndio maana hajawacha kufanya kazi ijapo alitaka kuwacha kazi mwishoni mwa mwaka jana apumzike. Sollinger, mfanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya Bilfinger-Berger alitekwa nyara mnamo Agosti 3 lakini haijulikani mpaka sasa ikiwa kuna fedha zozote zilizolipwa waasi kabla kuachiliwa huru.
Mada ya nne ilihusu Somalia kupata serikali mpya. Gazeti la Neue Zürcher lilisema waziri mkuu, Ali Mohamed Gedi, aliteua baraza jipya la mawaziri lakini bado mji wa Mogadishu unamilikiwa na wanamgambo wa kiislamu. Wanamgambo hao pia wanaongeza udhibiti wao wa eneo la kaskazini, na wameendelea kukataa mazungumzo ya aina yoyote na serikali ya mpito ikiwa wanajeshi wa Ethiopia wataendelea kubakia Somalia. Mhariri alisema muungano wa IGAD unataka kutuma kikosi cha kulinda amani nchini Somalia kuisaidia serikali ya mpito.
Gazeti la Neues Deutschland liliripoti juu ya hatua ya wanamgambo wa kiislamu kutaka kupambana na maharamia wa kisomali wanaoziteka nyara meli katika pwani ya Somalia. Mhariri alisema pwani ya Somalia ni hatari zaidi kwa mabaharia wa mataifa ya magharibi huku maharamia wakitumia hali ya kisiasa ya Somalia kama kisingizio cha kufanya mashambulio yao. Wakitumia vifaa vya kisasa vya satelaiti, maboti ya injini na silaha nzito za kisasa, meli zinavamiwa na kushambuiliwa.
Maharamia huzishambulia pia meli za Umoja wa Mataifa, alisema mhariri wa gazeti la Neues Deutschland. Tangu mwezi Machi mwaka jana, visa 37 vya utekaji nyara vimeripotiwa. Somalia haina jeshi lake la majini linaloweza kuilinda pwani yake.
Shirika la kimatafa la usafiri wa meli na kituo cha kupambana na uharamia, hakina mawasiliano ya kila mara na maofisa wa bandari za Somalia. Maofisa wake hukaa takriban maili 200 kutoka pwani ya Somalia.