Afrika katika Magazeti ya Ujerumani
9 Aprili 2004Walimwengu wamejifunza mambo mengi kufuatia mauaji ya halaiki yaliyofanyika nchini Rwanda miaka 10 iliyopita. Haya ni maoni ya waziri wa dola kwenye wizara ya maendeleo, Bi. Uschi Eid, kama yalivyoandikwa kwenye gazeti la TAGESPIEGEL:
"Rais Kagame wa Rwanda ameituhudu dunia kwamba, ilishindwa kuingilia kati nchini humo ili kuzuia mauaji ya halaiki, na kwa kufanya hivyo walimwengu wamepunguza thamani ya maisha ya binadamu. Je, ni sahihi kusema hivyo? Ni kweli, jumuiya ya kimataifa ilishindwa kuingilia kati. Kamanda mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa mataifa kutoka Kanada, alitoa taarifa kwamba nchini Rwanda kuna hatari ya mauaji ya halaiki. Lakini makao makuu ya umoja wa mataifa mjini New York hayakushughulikia haraka suala hili.
Kwa upande mwingine hata nchi za jirani za Afrika hazikuingilia kati. Zingeweza kabisa kuingilia kati na kuzuia mauji hayo ya halaiki, kama kanuni ya kutoingiliana katika masuala ya ndani isingekuwepo.
Madai ya Kagame yanaweza kutafsiriwa kama vile, umoja wa mataifa haukuingilia kati kwa vile mauaji haya yalihusu maisha ya waaafrika. Tuhuma za aina hii zinapingwa vikali na waziri wa dola kwenye wizara ya maendeleo, Bi. Uschi Eid. Anaema, kulikuwa na mambo mengi nyeti wakati huo, yaliyozuia kuongezwa kwa askari wa kulinda amani nchini Rwanda, na hapohapo kuwapunguza askari hao baada ya Wabelgiji kuliwa. Lakini haya hayamaanishi kwamba, maisha ya binadamu barani Afrika hayana thamani kubwa.
La kujiuliza sasa ni, je, Umoja wa mataifa, Ulaya, Afrika na welimwengu kwa ujumla wamejifunza sasa kwa kutokana na makosa iliyofanya?
Umoja wa mataifa umejifunza mengi. Nchi za magharibi pia, mathalani nchi za Ulaya ziliingilia kati mara moja baada ya kuona Waserbia wameanza kuuwa watu wengine. Bila ya fundisho la Rwanda, hali ingekuwa tofauti.
Afrika imejifunza mengi pia kwa kutokana na makosa hayo: Jumuiya ya zamani ya Afrika imegeuzwa na badala yake Umoja wa Afrika kuanzishwa. Umoja ambao una mamlaka sasa ya kuingilia kati hata kwenye matukio ya mauaji ya halaiki.
Hata hivyo, uamuzi wa kuingilia kati katika nchi fulani utaendelea kuwa mgumu. Ugumu wa kutathmini kwa uhakika mwanzo wa mauaji ya halaiki utaendelea kuwepo. "
Wakulima wa Afrika wanaouza mazao yao kwenye Umoja wa Ulaya wanakabiliwa na hali ngumu, kwani kuanzia mwaka ujao, Januari 2005, Umoja wa Ulaya utaanza kuwadai wakulima wa Afrika kutekeleza kwanza masharti magumu ili mazao yao yaweze kununuliwa.
Gazeti la FINANCIAL TIMES limechambua ugumu utakaowakabili wakulima hohehahe wa Afrika kwa kuangalia mfano wa wakulima wa Kenya.
"Mama Purity Gashamba ana shamba la maharagwe la ukubwa wa hekari 3 hivi kandokando ya mlima Kenya.
Ili aendelee kuuza maharagwe yake katika nchi za Umoja wa Ulaya -- baada ya masharti magumu kuanza kutekelezwa hapo mwaka kesho mwanzoni -- amelazimika kufanya mambo mbalimbali kwenye shamba lake. Yote haya yatamgharimu kiasi cha Euro 1,500, sawa na pato lake la mwaka. Kwanza anatakiwa kujenga vyoo karibu na mashamba yake. Pili anatakiwa kujenga mabanda ya kuchambulia maharagwe, ambamo wafanyakazi wake watatakiwa kuingia humo wakiwa wamevaa ovaroli na kofia.
Mazao haya yakifika Ulaya, kila punje ya haragwe lazima iweze kufuatiliwa kirahisi imetokana na mbegu gani na imevunwa kutoka wapi na kwenye shamba gani. Makasha machache tu ya maharagwe kutoka nchi fulani yakikutwa na mabaki ya kemikali kupita kiasi, yanaweza kuponza mauzo ya nchi nzima.
Haya ni baadhi tu ya masharti mengi magumu ya Umoja wa Ulaya dhidi ya matunda na mboga kutoka nchi za nje. Wao wanasema, wanafanya hivi ili kujikinga na magonjwa mbalimbali kama vile kichaa cha ng’ombe.
Kwa namna fulani mama Gashamba ana uwezo wa kutekeleza masharti hayo, lakini wakulima wengine wengi hawatamudu gharama hizo, licha ya hivyo hawana hata habari kama kuna utaratibu mpya. Licha ya hivyo kuna ushindani mkali kutoka nchi nyingine kama vile Morocco na Senegal ambazo zina njia rahisi zaidi ya kufikisha mazao katika nchi za Ulaya.
Hili ni pigo kubwa kwa nchi kama Kenya ambako tangu mwaka 1995 kilimo cha matunda, maua na mboga, kimeshamiri kiasi kwamba mauzo yake katika nchi za nje yameongezeka kwa asilimia 70"
Kwa kuhitimisha safu hii ya "Afrika katika Magazeti ya Ujerumani" wiki hii, tugeukie sasa mvutano unaoendelea nchini Kenya kuhusiana na katiba.
Gazeti la TAGESZEITUNG limeandika:
"Wawaziri wa vyama mbalimbali kwenye serikali ya muungano ya Kenya wanatishana kwa maneno makali.Wananchi nao wanashiriki kwenye mjadala huu kwenye vilabu siyo kwa maneno tu, bali kwa ngumi pia.
Mjadala wa katiba ya nchi ndiyo jambo lililopewa uzito mkubwa na serikali ya rais Mwai Kibaki iliyokuja madarakani mwaka 2002. Mambo yaligeuka tangu baada ya tume ya katiba kutoa mapendekezo yasiyolandana na utashi wa serikali, hususani kwenye kuanzisha wadhfa wa waziri mkuu mwenye mamlaka zaidi serikalini.
Katiba ya sasa inampa rais wa nchi madaraka makubwa zaidi: Anateua majaji na viongozi wa mashirika ya umma, anagawa ardhi na ndiye mkiritimba wa maamuzi yote ya kisiasa. Serikali ya sasa ilipokuwa kwenye upande wa upinzani, ilipigania kupunguzwa madaraka ya raisi na kuanzishwa kwa cheo cha waziri mkuu. Hata uwingi mkubwa wa wananchi wa Kenya wanaunga mkono wazo hili, hasa kwa vile rais wa zamani Daniel Arap Moi aliyatumia vibaya madaraka yake.
Kizungumkuti ni kuwa, rais Mwai Kibaki ni Mkikuyu – kabila kubwa nchini humo. Lakini ushindi wake uliwezekana kwa mchango pia wa kabila la Waluo, kabila la tatu kwa ukubwa nchini, likiongozwa na mwanasiasa maarufu Raila Odinga. Kabla ya ushindi, bwana huyu aliahidiwa cheo cha uwaziri mkuu, lakini akaambuliwa uwaziri wa ujenzi wa barabara. Inavyoelekewa Wakikuyu wengi hawako tayari kuona serikali inaongozwa na waziri mkuu kutoka kabila la Waluo."