Afrika katika magazeti ya Ujerumani
17 Oktoba 2003
Magazeti takriban yote mashuhuri humu nchini yamechambua hali nchini Liberia na kuingia madarakani rais wa mpito Gyude Bryant."Bryant atwaa hatamu za uongozi katika wakati ambapo Charles Taylor anapaza sauti" hicho kilikua kichwa cha maneno cha Frankfurter Allgemeine huku Tageszeitung likiandika "Liberia inategemea maadini yake".Tuanze lakini na Frankfurter Rundschau linalosimulia jinsi kiongozi mpya wa Liberia Gyude Bryant alivyopokelewa kwa shangwe alipowasili mjini Monrovia akitokea Ghana.
"Tunataka amani" ndio mwito wa wananchi kwa kiongozi wao mpya.Sherehe za kuapishwa kwake chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa zilikua na walakini,linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine likizungumzia kushindwa bunge jipya kumteuwa kwa wakati spika wake."Hayo si muhimu lakin","muhimu linahisi gazeti la Frankfurter Rundschau ni ile hali kwamba wababe wote wa kisiasa wa eneo hilo,rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria,rais John Kufuor wa Ghana na rafiki wa muda mrefu wa Taylor,rais wa Burkina Fasso Blaise Compaore walihudhuria sherehe hizo wakiunga mkono juhudi za amani katika nchi hiyo ndogo jirani."Gazeti linaonyesha mapokezi ya shangwe yasiangaliwe kama dalili ya kupatikana amani ya kudumu-likikumbusha hata Taylor alisahangiriwa aliposhinda uchaguzi katika mwaka 1997.
Süddeutsche Zeitung linasema mtihani mkubwa kwa serikali ya mpito ya Liberia utakua kuwapokonya silaha wanamgambo 45 elfu wa mtawala wa zamani Charles Taylor,licha ya kwamba,kama linavyoandika Frankfurter Allgemeine, Taylor akiwa uhamishoni nchini Nigeria ameshatamka anaunga mkono juhudi za amani na hata mkewe alifika Monrovia kushuhudia kuapishwa rais mpya.
Gazeti la Die Tageszeitung linahisi jukumu linaloikabili serikali mpya ya vyama vyingi ya Liberia chini ya uongozi wa rais wa mpito Gyude Bryant ni kubwa mno kupita kiasi;ujenzi wa nchi iliyoteketezwa vibaya sana kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 14.Limemnukulu muakilishi wa Umoja wa mataifa Jacques Klein akisema Liberia inahitaji mpango wa kimataifa wa miaka mitano hadi kumi kuweza kuijenga upya.
Nchi hiyo yenye wakaazi milioni tatu ni tajiri kwa maadini:almasi na dhahabu imesheheni katika eneo la Lofa River kaskazini magharibi ya Monrovia,yakiwepo pia madini adimu aina ya shaba inayotumika kutengenezea zana za elektronik-maadini ya kolt yanayopatikana pia katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kong na kadhalika.Jacques Klein anaamini uwezekano wa kuwahui wananchi wa Liberia kutokana na mali asili waliyo nayo upo hivi sasa,kinyume na ilivyokua tangu jamahuri ya Liberia ilipotangazwa katika mwaka 1847 hadi hii leo.Gazeti la Tageszeitung linasema kinachohitajika ni usimamizi bora wa mali asili kuhakikisha wananchi wote wa Liberia wanafaidika na sio peke yao familia 14 zinazotokana na vizazi vya watumwa waliohamishiwa Liberia mnamo nusu ya kwanza ya karne ya 19.
Mada nyengine iliyodhukuriwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii ni namna ya kupambana na ukosefu wa chakula barani Afrika.Gazeti la Frankfurter Allgemeine limechapisha mahojiano pamoja na waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani bibi Heidemarie-Wieczorek-Zeul na waziri wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa André Wiltzer.Wote wawili wanakubaliana kuna njia za maana za kupambana na balaa la njaa barani Afrika .
Nchi hizi mbili anasema waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani zimeamua kushirikiana kupambana na kitisho cha watu kufaa kwa njaa.Kwa mujibu wa tarakimu za shirika la umoja wa mataifa la mpango wa chakula ulimwenguni,watu milioni 38 wanakabiliwa na balaa la kufa kwa njaa mwaka huu barani Afrika.Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul amesema kupitia mahojiano pamoja na Frankfurter Allgemeine Zeitung Ujerumani na Ufaransa zinatanguliza mbele bidhaa zinazopatikana katika eneo husika badala ya kumimina ngano au mahindi kutoka nje.Kwa namna hiyo shughuli za kiuchumi za eneo zima zinaimarika.Wanalaani wanasema misaada ya chakula kutumiwa kama njia ya kutupa mazao ziada au kujitafutia masoko mepya.
Tumalizie ukurasa wetu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani kwa ripoti ya gazeti la mji mkuu Berliner Zeitung ."Jumuia ya nchi za Afrika mashariki imeungana upya mjini Berlin" limeandika gazeti hilo likizungumzia juu ya kuhamia mjini Berlin ofisi za ubalozi wa Tanzania,Kenya na Uganda.Berliner Zeitung limesifu uamuzi wa Kenya kujijengea wenyewe ofisi yake mpya ya ubalozi.Kenya na Afrika kusini ndio nchi pekee za kusini mwa jangwa la Sahara kujenga ofisi mpya za ubalozi mjini Berlin.,limemaliza kuandika gazeti hilo likisifu uamuzi wa Kenya mmojawaapo wa washirika wakubwa wa kibiashara wa ujerumani katika Afrika mashariki.