Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii
10 Juni 2005Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE liliandika kuhusu hatua ya serikali ya Sudan kuitatiza tume ya kulinda amani katika eneo la kusini mwa nchi hiyo. Jeshi la Ujerumani linatakiwa kuwa tayari siku za usoni kufanya kazi katika mataifa ya kigeni.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Peter Sruck alinukuliwa na jarida la Focus akisema Ujerumani inatakiwa kuwa na wanajeshi wake nchini Sudan, na kwamba wanajeshi wa Ujerumani watafanya kazi katika maeneo mengine duniani mbali na Afrika.
Ujerumani ina jeshi lililo mahiri na iwapo umoja wa mataifa utahitaji mchango wa jeshi hilo, haiwezekani kukwepa kujitwika jukumu. Hata hivyo, kwa sasa serikali ya Sudan inaitatiza tume ya kulinda amani.
Gazeti liliandika, kufuatia uamuzi wa bunge la Ujerumani mwishoni mwa mwezi Aprili, wanajeshi 75 wa kulinda amani wanatakiwa kupelekwa katika eneo la kusini mwa Sudan kuhakikisha mkataba wa kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali ya Khartoum unatekelezwa. Lakini serikali imekwepa juhudi za kufikia mapatano, kutatiza ugavi na utoaji visa. Hivi sasa ni wanajeshi wanne tu wa Ujerumani walio nchini Sudan.
Waziri Struck atalijadili swala hili na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan wakati wa ziara yake mjini New York mwishoni mwa mwezi huu, lakini hakuthibitisha ikiwa Ujerumani itasita kuwapeleka wanajeshi wake kusini mwa Sudan.
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU kuhusu madaa hii liliandika kwamba waziri kivuli wa ulinzi wa chama cha FPD, Jürgen Koppelin, alisema wanajeshi wa Ujerumani wanatakiwa kutumwa katika mataifa ya kigeni kushiriki katika shughuli za kulinda amani na wala sio vita.
Struck alitaka matokeo ya hatua ya kuwapeleka wanajeshi wa Ujerumani yajadiliwe, lakini kwa kuwa siasa za hapa nchini ziko katika njia panda, jambo hilo haliwezi kuzungumziwa kwa kina kirefu, liliandika gazeti hilo.
Mada nyengine iliyojadiliwa na gazeti la FRANKFURTER RUNDSHAU ni mauaji ya raia wa Ethiopia, mjini Addis, kufuatia maandamano ya kuyapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika nchini humo mwezi uliopita.
Jumatano iliyopita, watu wengi waliuwawa na wengine wakajeruhiwa vibaya, wengi wao wakiwa vijana, wakati wanajeshi na polisi walipowafyatulia risasi kujaribu kuwatawanya waandamanaji, wakiwemo wanachama wa kundi la kupigania haki za binadamu la nchi hiyo. Waandamanaji waliwashambulia maafisa wa usalama kutumia mawe.
Maandamano yalipigwa marufuku nchini Ethiopia kuanzia tarehe 15 mwezi Mei, wakati waziri mkuu Meles Zenawi alipoichukua polisi na kuiweka chini ya utawala wake. Upinzani nchini humo unailaumu serikali kwa kuidhibiti polisi ya taifa hilo.
Gazeti liliandika pia kuhusu hatua ya wizara ya habari kufutilia mbali vibali vya waandishi habari wanaoripotia redio Deutsche Welle na Sauti ya Marekani, VOA, kwa tuhuma za kuripoti habari za uongo.
Kuhusu machafuko ya mjini Addis Ababa, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE liliandika kuhusu kutiwa mbaroni na polisi kwa wanafunzi 520 wa vyuo vikuu waliokuwa wakiandamana kuyapinga matokeo hayo ya uchaguzi.
Matatizo ya chama cha African National Congress, ANC nchini Afrika Kusini yalizungumziwa katika gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE. Gazeti liliuliza, je mtu anaweza kumfanya nini mwanasiasa mashuhuri ulimwenguni, anayeaminika na ambaye ana nafasi nzuri ya kuwa rais wa taifa katika siku za usoni?
Hilo ndilo tatizo linalokikabili chama cha ANC baada ya mahakama moja mjini Durban kumhukumu makamu wa rais wa taifa hilo, Jacob Zuma, kwa makosa ya wizi wa fedha. Katika kesi hiyo mfanyabiashra na mshauri wa kiuchumi wa Zuma, Shabir Shaik, alipatikana na makosa ya udanganyifu, ufisadi na kukwepa kulipa kodi na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 gerezani.
Chama cha ANC kinakabiliwa na tatizo kubwa kufuatia kesi hii iliyomhusisha bwana Zuma, kwani yeye alitarajiwa kuchukua nafasi ya rais Thabo Mbeki kuwania wadhifa wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2009. Mbeki na Shaik walijipatia euro elfiu 150 katika kashfa hiyo.
Na hatiamye, mawaziri wa ulinzi wa mataifa ya jumuiya ya kujihami ya NATO, walikubaliana mjini Brussels kuzisaidia juhudi za kijeshi katika eneo lililokumbwa na mzozo la Darfur, magharibi mwa Sudan. Hii ni mada nyengine iliyozingatiwa pia na gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE.
Gazeti liliandika kuwa juhudi za mwanzo za shirika hilo la NATO huko Darfur zitakuwa kuwasafirisha wanajeshi wa umoja wa Afrika wanaolinda amani katika eneo hilo. Maafisa kadhaa wa NATO watapelekwa kwenye makao makuu ya umoja wa Afrika huko mjini Addis Ababa, Ethiopia, kusaidia katika maongozi na mipango ya tume ya umoja huo.