Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii
10 Oktoba 2003
"Fursa ya kupatikana amani nchini Burundi" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Süddeutsche Zeitung kwa uchambuzi wake kuhusu makubaliano yaliofikiwa jumanne kuamkia jumatano iliyopita mjini Pretoria,baada ya mazungumzo magumu ya siku tatu mfululizo chini ya upatanishi wa rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki.Gazeti linaandika:
"Katika nchi ya Afrika mashariki iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe,kumezuka matumaini ya kusitishwa mapigano.Kundi kubwa kabaisa la waasi,vikosi vya kupigania demokrasia FDD,limetiliana saini makubaliano ya amani pamoja na serikali ya Burundi katika mji mkuu wa Afrika kusini Pretoria.Makubaliano hayo yamewezekana kutokana na aupatanishi wa rais Thabo Mbeki.Chamaa cha ukombozi wa taifa FLN,kundi la pili muhimu la waasi,linayapinga lakini makubaliano hayo.
Gazeti la Süddeutsche Zeitung limezungumzia ugawanaji madaraka katika serikali ya umoja wa taifa,likimnukulu msemaji wa rais Domitien Ndayizeye akisema pande ehizo mbili zimekubaliana FDD ipatiwe nyadhifa tatu za magavana kati ya mikoa 17 ya nchi hiyo,nyadhifa mbili za ubalozi na viti 15 kati ya 182 vya bunge.
Wamekubaliana pia kugawana dhamana jeshini na waasi wa zamani wa FDD wajumuishwe pia katika jeshi la taifa litakalofanyiwa marekebisho.Gazeti limezungumzia hasara ya maisha ya binadam,watu zaidi ya laki tatu waliouwawa kufuatia miaka kumi ya vita vya wenyewe .Limekumbusha pia makubaliano ya amani yaliyofikiwa hapo awali pamoja na makundi madogo madogo ya waasi.FDD na serikali waliwahi kutiliana saini makubaliano ya kuweka chini silaha december mwaka jana,lakini gazeti la Süddeutsche Zeitung linakumbusha,baadae yakaendewa kinyume.
Gazeti la Neue Züricher Zeitung nalo pia limezungumzia matumaini mepya ya amani yaliyozuka nchini Burundi.Limetaja pia mwito wa rais Domitien Ndayizeye na mwenyekiti wa FDD Pierre Nkurunziza wa kusitishwa haraka mapigano nchini humo.Gazeti lakini linajiuliza kama mwito huo utaitikwa na pande zinazohasimiana.Likakumbusha gazeti hilo kundi jengine la waasi,la pili kwa ukubwa nchini Burundi FNL halikuhusishwa na mazungumzo ya Pretoria na limeshayatia ila makubaliano yaliyofikiwa.
"Bashir amsifu Garang" ndio kichwa cha maneno cha Frankfurter Allgemeine Zeitung kuhusu mazungumzo ya amani ya Sudan yanayoendelea nchini Kenya.Dalili za kumalizika vita vya miaka 20 vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan zinazidi kuongezeka.Mazungumzo ya amani ya Sudan kati ya serikali na chama cha waasi wa kusini SPLA yameanza upya mjini Naivasha nchini Kenya,baada ya pande hizo mbili kufikia "makubaliano ya usalama" september iliyopita.
Makubaliano yanazungumzia juu ya kuhamishwa hatua baada ya hatua vikosi vya serikali toka maeneo ya mapambano kusini mwa nchi hiyo pamoja na kuundwa majeshi mawili katika kipindi cha mpito.Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo ya ana kwa ana kati ya makamo wa rais Ali Osman Taha na kiongozi wa SPLA John Garang.
Haijawahi hata mara moja kushuhudiwa,dhamana wa ngazi ya juu wa serikali kuingilia kati moja kwa moja mazungumzoni.Hali hii ni ishara dhahiri wamedhamiria kweli kweli kukomesha vita.Limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine lililomnukulu rais Hassan al Bachir akimsifu John Garang kama "kiongozi mstahiki".Sifa hizo amezitoa alipokua akihutubia kikao cha ufunguzi cha bunge jumatatu iliyopita mjini Khartoum.
Hotuba yake iliyoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya nchi hiyo inatafsiriwa kama juhudi za kuwatanabahisha wasudan wamtambue John Garang kama dhamana wa kisiasa.Hadi wakati huu kiongozi huyo wa waasi alikua akiangaliwa na wakaazi wa kaskazini mwa Sudan kama "mhalifu".
"Utayarifu wa kufikia amani pamoja na shinikizo la Marekani,vimesababishwa na utajiri wa mafuta katika eneo la kusini mwa Sudan,mafuta ambayo hayataweza kuchimbwa kwa muda wote ule ambao eneo hilo litaendelea kuwa kitovu cha mapigano ya umwagaji damu.Kwa mtazamo wa Marekani, ni muhali kuyaachia pekee yao uwanja makampuni ya mafuta ya Malaysia na China nchini Sudan.Limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine likimaliza kwa kusema "mada tete katika duru hii ya mwisho ya mazungumzo ya amani mjini Naivasha itahusu kwa hivyo namna ya kugawana pato la mafuta kati ya serikali ya Khartoum na waasi wa SPLA.
Tumalizie ukurasa wetu wa afrika katika magazeti ya Ujerumani kwa ripoti ya Frankfurter Allgemeine kuhusu kutunukiwa zawadi ya amani ya Nobel,muandishi vitabu wa Afrika kusini John Maxwell Coetzee."Zawadi hiyo ni hishma na sifa kwa Afrika kusini na bara la Afrika kwa jumla"amesema hayo rais Thabo Mbeki akimpongeza muandishi vitabu huyo,wa pili wa kutoka Afrika kusini kutunukiwa zawadi ya amani ya uandishi sanifu baada ya Nadine Gordimer,miaka kumi kabla ya hapo.Tunzo ya amani ya uandishi sanifu ni fakhari kwa bara la Afrika,na jaza kwa fasihi ya Afrika anasema mchapishaji vitabu wa kutoka Senegal Seydou Nour Ndiaye aliyenukuliwa na gazeti la Neue Züricher Zeitung.