Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 3-12-2004
3 Desemba 2004Rais wa Ujerumani Horts Köhler ameitaka serikali ya Ujerumani kuongeza misaada yake ya maendeleo kwa bara la Afrika. Pia amesema ruzuku zinazotolewa katika nchi za viwanda, zinazuia maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.
Gazeti la DIE TAGEZEITUNG limeendelea kwa kuandika:
"Rais wa Ujerumani bwana Köhler alitoa rai hii alipokuwa akihutubia wanafunzi na wahadhiri wa chuo kikuu cha Tübingen kufuatia mwaliko wa mfuko wa maadili ya jamii duniani.
Bwana Köhler ambaye anapanga kuanza ziara ya nchi mbalimbali za Afrika wiki ijayo, alisema, "Hii leo utu wa walimwengu duniani unategemea hatima ya bara la Afrika". Aliongezea kwa kusema: "Watu wote lazima watambue kuwa, wanaishi kwenye dunia moja.
Wakazi wa nchi za viwanda lazima wajione kama washiriki au ndugu za watu hohehahe duniani: vinginevyo hawawezi kuendelea kuishi maisha ya raha na amani."
Kiongozi huyu wa Ujerumani amezitaka nchi za viwanda ikiwa ni pamoja na Ujerumani kuongeza misaada ya maendeleo hadi kufikia asilimia 0.7 ya pato jumla. Alisema nchi tajiri zilizo na utawala bora peke yake ndiyo zinaweza kuhakikishia wakazi wake haki za binadamu na hapohapo kupambana na matatizo mengine kama vile rushwa, uhalifu na UKIMWI."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la DIE TAGEZEITUNG.
Wiki hii siku ya Jumatano na Alhamis, nchini Msumbiji kulifanyika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge. Gazeti la DER SPIEGEL limeendelea kwa kuandika:
"Kinyume na ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, rais Joachim Chissano mwenye umri wa miaka 68 aliyeiongoza nchi hii kwa miaka 18 hakutaka kuwa kiongozi wa maisha. Rais Chisssano atakumbukwa kwa kufanikisha maendeleo makubwa ya kiuchumi.
Baada yake, chama tawala cha ukombozi wa Msumbiji, FRELIMO kimemtuma mfanyabiashara maarufu ARMANDO GUEBUZA kuwania kiti cha uraisa. Kiongozi wa chama cha upinzani RENAMO, bwana ALFONSO DHLAKAMA anagombea uraisi kwa mara ya tatu mfululizo.
Kwa mujibu wa matangazo ya redio ya taifa, mgombea wa FRELIMO bwana GUEBUZA anaongoza kwa kujipatia asilimia 60 ya kura zilizohesabiwa mpaka sasa. Hata hivyo tume ya uchaguzi imetangaza, matokeo kamili ya uchaguzi yatatolewa baada ya siku 7 hivi na kutangazwa rasmi tarehe 17-Disemba."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la DER TAGESSPIEGEL.
Habari nyingine zilizogonga vichwa vya habari kwenye magazeti ya Ujerumani wiki hii ni uvamizi wa Rwanda nchini Kongo. Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:
"Inaonekana wazi kuwa Jeshi la Rwanda limeanza tena mashambulizi dhidi ya waasi wa kihutu wanaoishi nchini Kongo na hivyo kuhatarisha mkataba wa amani kati ya Rwanda na Kongo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Umoja wa Mataifa, siku ya Jumatano wiki hii, takribani askari 100 wa Rwanda walionekana wamevuka mpaka huko karibu na Rutshuru mashariki mwa Kongo. Msemaji wa jeshi la Kongo amenukuliwa akisema, tangu siku kadhaa zilizopita, jeshi la Rwanda linapigana na waasi wa kihutu karibu na hifadhi ya taifa ya Virunga. Rais wa Rwanda Paul Kagame amekiri mashambulio haya kwa pembeni alipokuwa akihutubia kikao cha bunge. Licha ya hivyo wiki iliyopita alimwarifu kwa njia ya barua rais wa Umoja wa Afrika, juu ya mashambulio haya, akidai hayalengi majeshi ya Kongo. Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya umelaani vikali mashambulio haya. Nayo serikali ya mpito ya Kongo imesema, kitendo hiki ni ushari mkubwa na imetangaza kujiandaa kwa kutuma askari 10,000 kwenye eneo hilo. Pia Uganda imeanza kujihami kwa kutuma askari kwenye mpaka wake na Kongo."