Afrika katika magazeti ya Ujerumani, tarehe 24-02-2006
24 Februari 2006Hali ya ukame katika pembe ya Afrika inazidi kuongezeka kwa kutokana na uhaba wa mvua kwa miaka mingi mfululizo. Mashirika ya kimataifa ya misaada yametoa tahadhari ya baa kubwa la njaa. Tathmini ya mashirika haya inaonyesha zaidi ya watu milioni 11 wanahitaji misaada ya chakula.
Kuhusu mada hii gazeti la Kölner Stadt Anzeiger limeandika:
„Ukame mkubwa ulioendelea kwa zaidi ya miaka 10 katika za pembe ya Afrika umesababisha uhaba mkubwa wa chakula na maji. Ukame huu umesababisha kupungua kwa maeneo ya kuchungia mifugo na uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa ujumla.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la chakula duniani, FAO, karibu watu milioni 11 kati ya Eritrea na Tanzania wanakabiliwa na baa la njaa na hivyo wanahitaji msaada wa chakula. Hali kadhalika, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa, maeneo mengi hivi sasa yanashuhudia ukame mkubwa ambao haujawahi kutokea tangu mwaka 1961. Msimu mwingine wa mvua unategemewa katika maeneo mengi hapo mwazi wa April.
Shirika la msalala mwekundu linakadiria asilimia 80 ya mifugo katika eneo hili inaweza kuangamia kwa kutokana na uhaba wa maji na maeneo ya malisho.
Maeneo yaliyoathirika zaidi na ukame huu ni maeneo ya kusini mwa Ethiopia na Somalia. Hali ya mambo nchini Somalia ni mbaya zaidi kuwa kutokana pia na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kwa zaidi ya miaka 15.
Serikali ya Kenya imetangaza hali ya ukame nchini humo kuwa ni janga la kitaifa na imetoa wito wa misaada ya chakula kutoka umoja wa kimataifa ili iweze kuwapatia chakula karibu watu milioni 3.5 katika maeneo ya kaskazini mwa nchi. Taasis ya chakula duniani imeahidi kutoa tani 400,000 za chakula kwa Kenya.“
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER.
Shirika la ushirikiano wa kiufundi la Ujerumani, GTZ, ambalo ndiyo linasimamia miradi mingi ya maendeleo ya wizara ya ushirikiano wa kimataifa, limaridhika na tathmini ya miradi yake.
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika:
„Kwa mujibu wa tathmini ya miradi ya GTZ 261, tathmini iliyofanywa kwa kufuatana na kanuni za shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD, robo tatu ya miradi yote imeonekana kuwa ya mafanikio. Asilimia 5 tu ya miradi inayosimamiwa na shirika hili ndiyo imeonekana kushindwa kufikia malengo yake.
Asilimia 71 ya miradi ya shirika la GTZ iliyokamilika kati ya mwaka 2003 na 2004 huko Afrika, Asia, Amerika ya Kusini na Ulaya ya mashariki, imeonekana kuwa ya mafanikio. Aidha miradi hiyo imefanywa kwa ufanisi mkubwa na ni misaada endelevu.
Mkurugenzi wa shirika la ushirikiano wa kiufundi la Ujerumani, GTZ, bwana Bernd Eisenblätter, amesema, miradi yao ya kusini mwa jangwa la sahara imekuwa na mafanikio zaidi.
Kwa mfano nchini Burkina Faso, wakulima kwa kutumia njia za kijadi, wamefanikiwa kuokoa eneo la hekta 60,000 lililokuwa limeharibiwa kwa kutokana na ukame. Kwa kutokana na mradi huu, hivi sasa wameongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na hivyo kupunguza umaskini na wakimbizi wa kimazingira.
Shirika la GTZ linasimamia hivi sasa zaidi ya miradi 2600 duniani kote.”
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU.
Uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika nchini humo hapo siku ya Alhamis kwa kuvihusisha vyama vingi vya kisiasa, ulipewa uzito mkubwa kwenye magazeti mengi ya Ujerumani wiki hii.
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:
„Siku ya Alhamis iliyopita wapiga kura milioni 10,4 nchini Uganda waliitwa kwenye kupiga kura ya kumchagua rais wa nchi na wabunge. Hii ilikuwa mara ya kwanza kuvihusiha vyama vingi vya kisiasa nchini humo tangu miaka 26 iliyopita. Vyama vya kisiasa viliruhusiwa tena nchini Uganda kufuatia shinikizo la kimataifa. Tangu Rais Yoweri atwae madaraka hapo mwaka 1989, vyama vya kisiasa vilipigwa marufuku.
Hata hivyo uchaguzi huu uligubikwa na njama za kuchafuana majina zaidi na kutupiana lawama kulipo ilani za uchaguzi. Wengine wanajiuliza sasa, kama uchaguzi huu ulikuwa uchaguzi kweli. Kilele za kampeni hizi zilikuwa pale, mke wa kiongozi maarufu wa upinzani Kizza Besigye, alipotishia kumchafulia jina mshindani wa mume wake, rais Museveni. Mama huyu bila shaka ana mengi ya kusema, kwani alikuwa mpenzi wa Museveni wakati wakiendesha vita vya msituni.“