Afrika katika magazeti ya Ujerumani; tarehe 19.05.2006
19 Mei 2006Jiko jipya la kupikia linalotumia mafuta ya mimea hata mimea pori, bora zaidi na lisolotoa moshi, limetengenezwa na kampuni la BOSCH SIEMENS hapa Ujerumani. Baada ya kufanya majaribio husianifu kwa muda mrefu nchini Phillipines, wahusika wanataka kuendelea na majaribio haya nchini Tanzania.
Gazeti la KÖLNER STADT-ANZEIGGER limeendelea kwa kuandika.
„Zaidi ya watu bilioni 2.5 duniani wanapika chakula kwa kutumia jiko la mafiga matatu kwa vile hawana huduma za umeme na kwa vile kuni zinapatikana kwa bei nafuu kuliko mafuta au gesi. Lakini mtu anayepika kwa kuni kwenye jiko la mafiga matatu anavuta hewa chafu inayoathiri afya yake, sawa na kuvuta sigara 250 kwa siku.
Shirika la Afya ulimwenguni linakadiria watu milioni 1.6 wanakufa kila mwaka kwa kutokana na gesi za sumu wanazovuta wakati wa kupika. Hata kwa upande wa mazingira kuna athari kubwa, kwani familia ya wastani ya watu 6 inatumia kilo 700 za kuni kila mwaka. Misitu inateketea, mmommonyoko wa udongo unatokea na maji yanazidi kuadimika.
Kampuni la BOSCH SIEMENS limetengeneza jiko linalotumia mafuta ya mimea peke yake. Kwa muda wa miaka miwili wahusika wamefanya majaribio ya kutumia jiko hili katika miji 100 nchini Phillipines. Mpaka sasa wananchi wameridhika sana na jiko hili kwani wanaweza kupika haraka zaidi, kwa gharama ndogo na bila moshi wa sumu. Jiko hili linagharimu EURO 30 hivi na linaweza kutumia mafuta ya mimea mbalimbali yanayoweza kukamuliwa na wanakijiji wenyewe.
Kwa kampuni la BOSCH SIEMENS, huu si mradi wa kujipatia faida, bali mchango wao kwenye mkakati wa kupunguza ufyekaji wa misitu. Hivi sasa wamepanga kuendelea na majaribio ya jiko hili nchini Tanzania kwa kutumia mbegu za mimea pori iitwayo kwa Kiingereza Jatropha.“
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER.
Pamoja na kupungua kwa misaada ya maendeleo, kwa ujumla ustawi wa uchumi barani Afrika unatia moyo. Habari hizi za kutia moyo zimetolewa na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika AEB hivi karibuni.
Gazeti la GENERAL ANZEIGER limeandika:
„Ustawi wa uchumi wa kontinenti la Afrika mwaka uliopita, 2005, ulikuwa asilimia 4.9 ambao ni sawa na ustawi wa uchumi wa asilimia 3 hivi kwa kila mtu. Hata mwaka 2006 na mwaka 2007, taasisi hizi mbili zinategemea uchumi wa Afrika utastawi kwa kasi kuliko miaka ya 90 mpaka mwaka 2003. Hata hivyo, maendeleo haya yatafikiwa iwapo tu Afrika haitakumbwa na ukame wala mizozo mipya ya kivita.
Gazeti la GENERAL ANZEIGER limeandika; Ustawi mzuri wa uchumi barani Afrika unatokana kwa upande mmoja na kupanda kwa bei za mali-ghafi na mafuta, pia kwa kupungua kwa ukame katika nchi nyingi za Afrika. Lakini kiini kikubwa cha maendeleo haya ni utulivu wa kisiasa na kusita kwa mizozo ya kivita katika nchi mbalimbali za Afrika.
Kwa ujumla nchi zinazotoa mafuta na malighafi nyinginezo zinaendelea kwa kasi zaidi kuliko nchi zisizo na nafasi hiyo zinazonunua mafuta kutoka nje. Changamoto kubwa hivi sasa, ni nchi zinazotoa mafuta na madini, kutumia sehemu ya mapato yao kwa ajili ya kujenga miundo mbinu, hususani njia za usafiri kama vile reli, barabara za lami na bandari za ufanisi mkubwa. Pia kuna umuhimu wa kuboresha maisha ya wananchi na kubuni miradi mingine ili kuacha kutegemea sekta moja chache tu za uchumi.
Nchi za Afrika zisizo na utajiri wa mafuta zina mtihani mgumu wa kudhibiti mfumko wa bei unaochochewa na kupanda kwa bei ya mafuta.“
Hayo yamendikwa kwenye gazeti la GENERAL ANZEIGER.
Hispania imetangaza mikakati mipya ya kupunguza wimbi la wakimbizi wasio halali wanaojaribu kila mara kuingia Ulaya magharibi kupitia nchini humo.
Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG limeandika:
Miongoni mwa mikakati hii ni matumizi ya ndege na boti kwenye maeneo ya pwani, kuongeza vituo vya kulinda mpaka na hapohapo kuziomba nchi husika kuwapokea wakimbizi wa kughushi wanaporudishwa makwao. Ili kufanikisha zoezi hili, Hispania imeomba pia msada kutoka kwenye Umoja wa Ulaya. Mwanzoni mwa mwaka wakimbizi 1400 walijaribu kuingia Ulaya kwa kupitia kwenye visiwa vya Hispania.
Kwa maelezo hayo yaliyoandikwa kwenye gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG ndiyo tunahitimisha udondozi wa „Afrika katika magazeti ya Ujerumani“.