Afrika katika Magazeti ya Ujerumani tarehe 17-12-2004
17 Desemba 2004Jana siku ya Alhamis, rais wa Ujerumani Horst Köhler, alimaliza ziara yake ya siku 10 barani Afrika kwa kuitembelea Jibuti. Siku ya Jumatano iliyopita, alipokuwa mjini Addis Abeba - Ethiopia, alitoa hotuba maalumu mbele ya baraza la Umoja wa Afrika.
Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:
"Rais Köhler ametumia nafasi hii kuzitaka nchi za viwanda, zielewe matatizo ya Afrika na hapohapo kuongeza misaada ya maendeleo. Lakini hapohapo amezitaka nchi za Afrika kuendelea na mwamko mpya wa kujitegemea.
Alipokuwa akihutubia baraza la Umoja wa Afrika mjini Addis Abeba, alisisitiza umuhimu wa kujenga ushirikiano thabiti kati ya nchi tajiri na bara la Afrika. Alisema, ushirikiano huu utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
Rais wa Ujerumani ni miongoni mwa viongozi wachache wa nchi za viwanda ambao hivi sasa wameosimama kidete kulitetea bara la Afrika. Kwenye ziara yake ya kwanza barani Afrika, bwana Horst Köhler amelisifu bara la Afrika kwa kuanza ukurasa mpya kisiasa, hususani kazi zinazofanywa na Umoja waAfrika katika kuleta maendeleo endelevu, demokrasia, haki za binadamu na uongozi bora. Alizipongeza jitihada hizi zinazofanywa kwa pamoja na nchi za Umoja wa Afrika chini ya mpango mpya wa ushirikiano wa kuleta maendeleo, NEPAD.
Alisema, ni vizuri kwamba Umoja wa Afrika uliweka bayana tangu mwanzo, uwezekano wa umoja huu kuingilia kati kwenye nchi inayokiuka haki za binadamu. Aliongezea kwa kusema, mfano mzuri na unaoonyesha kuwajibika kwa Afrika hata kwenye masuala ya usalama, ni uamuzi wa Umoja wa Afrika, kutuma kikosi vya kulinda amani huko Darfur magharibi mwa Sudani."
Hayo yameandikwa kwenye gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG.
Mada nyingine kuhusu ya Afrika iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye magazeti ya Ujerumani wiki hii, ni wimbi la viongozi wa kisiasa wa nchi za magharibi kuitetea Afrika: Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye hapo mwakani atakuwa mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya na mataifa ya G8, amedhamiria kuipa kipaumbele zaidi mikakati ya kupambana na umaskini barani Afrika. Wakati huohuo Rais wa Ujerumani anahimiza ushirikiano kati ya nchi tajiri na nchi za Afrika.
Gazeti la DER SPIEGEL linauliza, kuna uelewa mpya sasa wa matatizo ya Afrika? Wahariri wa gazeti hili wakitafuta jibu la swali hili wamemhoji mwandishi maarufu wa riwaya kutoka Sweden na mtaalamu wa bara la Afrika, bwana Hennig Mankell.
"Bwana huyu ambaye ameishi Msumbiji kwa zaidi ya miaka 15 amesema, yeye amejifunza kuacha kuridhika na maneno matupu bali kungojea kwanza vitendo. Siyo mara ya kwanza kwa wanasiasa wa nchi za viwanda kutoa matamko mazuri ya kuwahurumia watu wa Afrika. Lakini haya yote huwa hayamsaidii mtu kawaida.
Aliendelea kwa kusema kuwa, umuhimu wa bara la Afrika umepungua sana katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Baada ya kumalizika kwa vita baridi, bara la Afrika lilipoteza umuhimu wake kwenye masuala ya kijeshi na kisiasa. Kutoka Afrika, nchi za viwanda hivi sasa zinataka kwenda kuchukua malighafi — na siyo kahawa, tumbaku na madini peke yake, bali hata wacheza mpira na wafanyakazi wengine muhimu kama vile madaktari, alisema bwana Mankell.
Licha ya misaada mingi ya maendeleo kutolewa na nchi za viwanda pamoja na taasisi za fedha za kimataifa, bara la Afrika bado linajikongoja tu. Alipoulizwa, kitu gani kimekwenda mrama barani Afrika, kwa mfano nchini Msumbiji ambako ameishi kwa zaidi ya miaka 15, alisema, Msumbiji kama nchi nyingine barani Afrika ni nchi tajiri, ina mali asili nyingi na vivutio vingi vya utalii. Lakini nchi hii ilivurugwa na kufilisiwa kabisa wakati wa ukoloni, na hali hii bado inaendelea katika sura nyingine. Baada ya msumbiji kujitawala hapo mwaka 1975, haikuwa na wasomi wa kutosha kuweza kuiongoza nchi hii kiuchumi wala kisiasa, wakati huohuo wakitakiwa kutekeleza matakwa tete ya taasisi za fedha duniani.
Misaada ya maendeleo ya Benki ya dunia ilikuwa inatolewa kwa masharti ya kufanya marekebisho ya mfumo wa uchumi – ambapo mara nyingi ilimaanisha kupunguza matumizi kwenye huduma za umma. Bwana Mankell amesema, mageuzi haya yameharibu hata huduma chache zilizokuwa zinatolewa vizuri, kama vile huduma ya afya. Kwa mantiki hii mageuzi haya yamechochea umaskini."